Katika jitihada za kuboresha mazingira ya
biashara na kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari, Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) mkoa wa Iringa imezindua rasmi Dawati Maalum la Uwezeshaji Biashara.
Hatua hii ni sehemu ya mkakati mpana wa kuimarisha ushirikiano kati ya serikali
na sekta binafsi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi uliofanyika katika
viwanja vya Garden, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa mnamo 9 Septemba 2025,
Meneja wa TRA mkoa wa Iringa, Bw. Peter Jackson, alisema dawati hilo litatoa
huduma mbalimbali ikiwemo elimu ya kodi, ushauri wa kisheria pamoja na msaada
katika kutatua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara katika ngazi zote.
“Dawati hili siyo tu sehemu ya kupata taarifa,
bali ni jukwaa la mazungumzo ya moja kwa moja kati ya wafanyabiashara na TRA.
Lengo letu ni kukuza uelewa wa pande zote na kuendeleza utamaduni wa ulipaji
kodi kwa hiari,” alieleza Jackson.
Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Bw. Benjamin Sitta,
aliwahimiza wafanyabiashara kulitumia vyema dawati hilo, akibainisha kuwa
serikali ipo tayari kusikiliza na kushughulikia changamoto zao, lakini pia
inatarajia ushirikiano katika kutimiza wajibu wa kulipa kodi.
Uzinduzi huo uliongozwa na Mkuu wa Mkoa wa
Iringa, Bw. Kheri James, ambaye aliipongeza TRA kwa kuanzisha mbinu bunifu ya
kuwasogezea karibu walipakodi huduma. Alisema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati
wa kitaifa wa kuboresha urahisi wa kufanya biashara nchini Tanzania.
Aidha, Bw. James aliwataka wananchi kudai risiti
kila wanaponunua bidhaa au huduma, akisema utaratibu huo unaleta uwazi katika
mapato na kuchangia maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho la
Wafanyabiashara Wadogo Tanzania (SHIUMA) mkoani Iringa, Bw. Kessy Ndandu,
alisema uzinduzi wa dawati hilo ni hatua mpya kwa wafanyabiashara wadogo kwani
utawasaidia kupata uelewa wa haki na wajibu wao wa kikodi, sambamba na mbinu za
kukuza biashara zao kwa kuzingatia sheria.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa serikali,
wawakilishi wa taasisi za umma na binafsi, vyama vya wafanyabiashara, viongozi
wa masoko pamoja na wakazi kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Iringa.