Saturday, 10 September 2011

TABIA YA KUKAA KIJIWENI INAPUNGUA






Na Gustav Chahe, Tanga.

ILE tabia ya baadhi ya wanachi kupenda kukaa vijiweni kucheza bao na kunywa kahawa kwa kigezo cha umwinyi imeelezwa kupungua siku hadi siku hatua ambayo ni ishara njema kwa uchumi wa Tanga na ustawi wa Taifa.

Akifungua hoteli ya NYUMBANI HOTELS and RESORTS tawi la Tanga iliyopo mtaa wa Uhuru, Waziri wa uchukuzi,  mawasiliano na Mbunge wa Tanga mjini Mhesh. Omari Nundu amewataka wawekezaji kutambua fursa za uchumi ikiwemo utalii ili kuendeleza jiji hilo.

Waziri Nundu alisema kwa kuboresha vituo hivyo kutaleta pia ushindani wa utalii nchini na kuongeza fursa za ajira kwa wazawa hususani vijana ambao wengi wao sasa wamekuwa na muamko wa kujituma, wakulima pamoja na uboreshaji wa miundombinu.

Awali Mkurugenzi mtendaji wa hoteli hiyo John Kessy akiongea na waandishi wa habari hotelini hapo amewataka wananchi kutambua huduma zitolewazo hotelini hapo pamoja na kuzitumia ili kukuza soko la bidhaa zao yakiwemo mazao kwa kuzingatia hoteli hiyo itakuwa ikitoa huduma zinazotokana na mazao yao wenyewe.

Kassy amewaomba wananchi kupeleka mazao yao ya mashambani kwa ajili ya kujipatia kipato na kwamba hoteli hiyo itakuwa ikizingatia utoaji wa ajira kwa wazawa ambapo hadi kukamilika wanatarajia kutoa ajira 56.

Hoteli ya jiji la Tanga ni ya tatu ikifuatia kwa ya pili ambayo ipo Moshi mkoani Kilimanjaro wakati ya kwanza ikiwa jijini Mwanza ambapo ya Tanga ujenzi wake umegharimu bilioni nne hadi kukamilika ikiwa na vyumba ishirini na vinane vya kulala wageni, kumbi mbalimbali za mikutano na sehemu za kuogelea.






WAKALA WA HIFADHI YA CHAKULA WAPATA CHANGAMOTO LUDEWA, MAKULI WAKIMBIA KAZI, WATOTO NA AKINA MAMA WAZIBA PENGO

Ludewa
 
WAKALA wa hifadhi ya chakula nchini (SGR) pamoja na kuanza kununua mahindi mjini Ludewa wiki iliyopita sasa inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukosa vibarua kwa ajili ya shughuli hiyo.
Akizungumza na Nipashe jana msimamizi mkuu wa kituo hicho Bw Ajib Mpunga alisema kuwa yeye aliwachukua makuli watano tu kutoka katika Chama cha Makuli Makambako kwa matumaini kuwa angepata makuli na vibarua wengine Ludewa, lakini hali imekuwa kinyume na matarajio.
Mpunga alisema kituo cha Ludewa mjini kimefunguliwa Ijumaa Septemba 2 mwaka huu na kutangaza nafasi za kazi mbalimbali ikiwemo makuli, washonaji magunia na wale wakupepeta mahindi, lakini mwitikio ni mdogo sana kwani hata wale wanaokuja hutoroka hata kabla ya muda.
Alisema kwa sasa wanalazimika kuwatumia wanawake na watoto wadogo kushona magunia kwa sababu vijana wengi mjini hapo wanapenda starehe zaidi kabla ya kufanya kazi na ndiyo maana wamekuwa wakikimbia kazi na kwenda kunywa pombe.
Akifafanua kuhusu bei za vibarua Mpunga alisema kwa kibarua aliyeko kwenye mizani hulipwa Shilingi 3,500/- kwa siku sanjari na kibarua anaye hamisha gunia kutoka juu ya mizani ambapo kuchekecha gunia moja ni shilini 150 na kushona Shilingi 20/- kwa gunia na kwamba bei hizo ni za kitaifa.
Bw. Mpunga aliongeza kuwa katika kuhakikisha wanapunguza malalamiko yasiyo ya lazima kwa wakulima wameamua kutoa elimu juu kujua kusoma mzani na kupima kwa wakulima wote wanaopeleka mazao yao kituoni.
Kiongozi wa makuli mjini Ludewa Bw. Ali Mwinuka kwa niaba ya wenzake alisema kuwa malipo wanayolipwa na wakala huyo ni madogo na kwamba haiwezekani uanze kazi tangu Saa mbili asubuhi hadi Saa 12 jioni unaambulia 3,500 vijana wanakimbia.
Naye Bw. Benito Mgimba mkulima aliyepeleka mazao kuuza katika kituo hicho aliipongeza hatua ya wakala hao kuweka wazi kila kitu kinachofanyika ikiwa pamoja na kutoa elimu kwa wakulima kusoma mizani wenyewe.
Mgimba akiwa mtu wa awali kabisa kupata elimu hiyo na wenzake aliongeza kuwa kama utaratibu unaotumika Ludewa ungetumika na sehemu zingine nchini mvutano kati ya wakulima na wakala usingekuwepo kabisa.
Taji Haule mkulima wa Ludewa vijijini aliwapongeza wafanyakazi wa wakala wa hifadhi ya chakula nchini kituo cha Ludewa kwa kufanyakazi kwa uwazi na kuepusha malalamiko kabisa kwa wakulima.
Hadi kufikia sasa kituo hicho kilichopo mjini Ludewa kimeshafikisha tani 300 za mahindi na kwamba hakuna malengo yaliyowekwa isipokuwa mahindi yataendelea kununuliwa mpaka watakapo amuliwa na makao makuu kwa sababu bado wananchi wanavuna mahindi.
             




KESI YA PEMBEJEO KATI YA AFISA MTENDAJI NA KATIBU WA CCM LUGARAWA YAAHIRISHWA TENA


Ludewa

KESI ya wizi wa mbolea ya pembejeo yenye thamani ya zaidi ya milioni sita inayowakabili Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Mdilidili Bw Otmari Kayombo Komnfoti, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Lugarawa Bw Yohanes Mhagama Muafaka na wenzake imeahirishwa tena.
Akiahirisha kesi hiyo mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Ludewa Emanuel Mwambeta, Mwendesha Mashtaka Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Mtikamtika alimwambia hakimu kuwa mshtakiwa namba moja ametoa taairifa ya kuumwa.
Bw. Mtikamtika alikuwa amefika na mashahidi watatu akiwemo Askari Polisi Kitengo cha Upelelezi Bw. Kelvin Kapinga, Afisa kutoka Ofisi ya TAKUKURU Bw. Lucas Swebe na mkazi mmoja wa kijiji cha Mdilidili kwa jina la  Bonifasi Mlowe.
Katika kesi hiyo yumo pia wakala wa mbolea katika kijiji hicho Bw. Anazet Mlelwa na mwenyekiti wa pembejeo wa kijiji hicho Bi. Grace Komba ambao wote walikuwepo mahakamani hapo.
Kesi hiyo imekuwa na mvuto wa pekee kuliko kesi zingine mahakamani hapo kutokana na wananchi wengi kuguswa, kuchoshwa na unyanyasaji wanaopata kutoka kwa viongozi wa vijiji na mawakala kuhusu mbolea ya ruzuku katika maeneo yao.
Katika hati ya mashtaka washtakiwa walitenda kosa hilo Januari 5 mwaka huu majira ya saa kumi za jioni na kwamba kwa udanganyifu walikula njama na kuiba jumla ya shilingi 6,966,000/- kwa njia ya kugushi kwa kuandika majina hewa wakiwemo waliokufa, wagonjwa na watoto wadogo.
Washtakiwa wanakabiliwa na makosa mia tatu kulingana na idadi ya wananchi waliokosa na kutapeliwa mbolea katika kijiji cha Mdilidili katika Kata ya Lugarawa.
Katika kesi hiyo kosa la kwanza linaloangukia katika kifungu cha 306 linawakabili washtakiwa wote wanne ambapo kosa la pili la kugushi linawakabili Bw. Komnfoti mtendaji wa kijiji na Bi Komba chini ya vifungu vya 333,335(a) na 337 sura ya 16 inayosema Januari 5 mwaka huu washtakiwa waligushi vocha 300 za mbolea ya ruzuku.
Kesi hiyo yenye jumla ya mashahidi sita wa upande wa mashtaka imeahirishwa hadi Octoba 12 mwaka huu ambapo itakuja kwa kusikilizwa na hakimu kuagiza washtakiwa wote kuhudhuria siku hiyo bila kukosa.
Mwisho

NYAMA YA NG’OMBE NA NGURUWE BEI JUU LUDEWA

















Ludewa


KUPANDA kiholela kwa bei za bidhaa mbalimbali wilayani Ludewa kunatokana na idara kadhaa ndani ya Halmashauri ya wilaya hiyo kutofanyakazi kwa ufanisi sanjari na ushirikiano hafifu uliopo kati ya idara na idara. 

Hayo yamethibitika kufuatia wafanyabiashara ya nyama ya ng’ombe na nguruwe mjini hapa kupandisha bei ya bidhaa hiyo kiholela huku mamlaka zinazohusika zikifumbia macho suala hilo kwa madai kuwa hazina taarifa na wakati mwingine kutupiana mpira juu ya nani awajibike.
Kwa mujibu wa wananchi na watumiaji wa bidhaa hiyo muhimu waliokutwa katika mabucha yaliyoko mjini hapa jana, walisema kilo moja ya nyama ya ng’ombe mchanganyiko imefikia shilingi 5,000 badala ya 4,000 ambapo steki ni shilingi 6,000 badala ya shilingi 5,000 na kwamba bei hizo zimeanza August 3 mwaka huu.
Kwa upande wake Afisa Biashara wilayani Ludewa Bi Martha Mfugale alipotakiwa kueleza ni kwanini bei imepande ghafla na kwa kiwango kikubwa alisema yeye mara ya mwisho alinunua nyama siku ya Sikukuu ya Eid el Fitr  kwa bei ya shilingi elfu nne.
Hata hivyo alisema kama ni kweli, kiwango kilichopandishwa ni kikubwa mno na kwamba hajui wachinjaji hao wametumia vigezo gani kufikia bei hiyo, lakini aliahidi kufuatilia suala hilo. Wafanyabiashara za chakula wamelalamikia bei hizo na kusema kuwa inawezekana hakuna serikali ndiyo maana watu wanaweza kuamuka asubuhi na kujipangia bei huku wananchi wenye kipato kidogo wasio na jukwaa la kusemea wakiendelea kuumia.
Afisa Mifugo Wilaya ya Ludewa  Bw Marco Mhagama yeye amekilaani kitendo kilichofanywa na wafanyabiashara hao wa nyama na kusema kuna haja ya idara ya biashara na idara ya mifugo kufanya kazi kama timu kwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara. Akifafanua kuhusu tozo na ushuru kwa wachinja nyama hao Bw Mhagama alisema kwa sasa ushuru wa Halmashauri ni shilingi elfu nne na mia tano kwa mchanganuo kuwa ushuru wa machinjio ni 2,000,ada ya mkaguzi yaani mtaalam ni shilingi 2,500 na serikali kuu shilingi 1,000.
Kwa upande wa nyama ya nguruwe Bw Mhagama alisema wao hawapaswi kupandisha bei kwa sababu ushuru huo hauwagusi wao kwa kuwa hawana machinjio maalum na kwamba hawarusiwi kutoa nguruwe nje ya kijiji kwa hiyo hakuna gharama.
Wakitoa mapendekezo yao wananchi wameitaka serikali kutoa bei elekezi kwa wachinjaji hao lakini wakawalaumu maafisa biashara na wale wa mifugo kuacha kung’ang’ania kukaa maofisini na kusubiri mishahara badala yake wafanye ukaguzi wa mara kwa mara siyo kwa wachinjaji tu bali na katika bidhaa zingine.
Wafanyabiashara hao wa mjini Ludewa wamejipandishia bei kiholela huku wakilaumiwa na wateja wao kwa kuchakachua mizani inayotumika katika mabucha, huku wakitumia mikokoteni kusafirishia nyama toka machinjoni. 

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...