WAKALA wa hifadhi ya chakula nchini (SGR) pamoja na kuanza kununua mahindi mjini Ludewa wiki iliyopita sasa inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukosa vibarua kwa ajili ya shughuli hiyo.
Akizungumza na Nipashe jana msimamizi mkuu wa kituo hicho Bw Ajib Mpunga alisema kuwa yeye aliwachukua makuli watano tu kutoka katika Chama cha Makuli Makambako kwa matumaini kuwa angepata makuli na vibarua wengine Ludewa, lakini hali imekuwa kinyume na matarajio.
Mpunga alisema kituo cha Ludewa mjini kimefunguliwa Ijumaa Septemba 2 mwaka huu na kutangaza nafasi za kazi mbalimbali ikiwemo makuli, washonaji magunia na wale wakupepeta mahindi, lakini mwitikio ni mdogo sana kwani hata wale wanaokuja hutoroka hata kabla ya muda.
Alisema kwa sasa wanalazimika kuwatumia wanawake na watoto wadogo kushona magunia kwa sababu vijana wengi mjini hapo wanapenda starehe zaidi kabla ya kufanya kazi na ndiyo maana wamekuwa wakikimbia kazi na kwenda kunywa pombe.
Akifafanua kuhusu bei za vibarua Mpunga alisema kwa kibarua aliyeko kwenye mizani hulipwa Shilingi 3,500/- kwa siku sanjari na kibarua anaye hamisha gunia kutoka juu ya mizani ambapo kuchekecha gunia moja ni shilini 150 na kushona Shilingi 20/- kwa gunia na kwamba bei hizo ni za kitaifa.
Bw. Mpunga aliongeza kuwa katika kuhakikisha wanapunguza malalamiko yasiyo ya lazima kwa wakulima wameamua kutoa elimu juu kujua kusoma mzani na kupima kwa wakulima wote wanaopeleka mazao yao kituoni.
Kiongozi wa makuli mjini Ludewa Bw. Ali Mwinuka kwa niaba ya wenzake alisema kuwa malipo wanayolipwa na wakala huyo ni madogo na kwamba haiwezekani uanze kazi tangu Saa mbili asubuhi hadi Saa 12 jioni unaambulia 3,500 vijana wanakimbia.
Naye Bw. Benito Mgimba mkulima aliyepeleka mazao kuuza katika kituo hicho aliipongeza hatua ya wakala hao kuweka wazi kila kitu kinachofanyika ikiwa pamoja na kutoa elimu kwa wakulima kusoma mizani wenyewe.
Mgimba akiwa mtu wa awali kabisa kupata elimu hiyo na wenzake aliongeza kuwa kama utaratibu unaotumika Ludewa ungetumika na sehemu zingine nchini mvutano kati ya wakulima na wakala usingekuwepo kabisa.
Taji Haule mkulima wa Ludewa vijijini aliwapongeza wafanyakazi wa wakala wa hifadhi ya chakula nchini kituo cha Ludewa kwa kufanyakazi kwa uwazi na kuepusha malalamiko kabisa kwa wakulima.
Hadi kufikia sasa kituo hicho kilichopo mjini Ludewa kimeshafikisha tani 300 za mahindi na kwamba hakuna malengo yaliyowekwa isipokuwa mahindi yataendelea kununuliwa mpaka watakapo amuliwa na makao makuu kwa sababu bado wananchi wanavuna mahindi.
No comments:
Post a Comment