Sunday, 4 September 2011

WANANCHI WENYE HASIRA LUGARAWA WAKATA MABOMBA YA MAJI YA PAROKO, NI BAADA YA MWENYEKITI WAO KUMPIGIA MAGOTI BILA MAFANIKIO.


LUDEWA

WANANCHI na watumiaji wa maji katika Kitongoji cha Luafyo Juu Lugarawa wilayani Ludewa jana walijawa jazba na kuamua kuyakata kwa mapanga mabomba ya maji yanayotumika pia na Kanisa Katoliki kwa madai kuwa Paroko wao amewanyima maji bila sababu.
Awali August 23 na 24 mwaka huu Mwenyekiti wa Kijiji cha Lugarawa Bw. Erasto Mhagama akiwa na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Luafyo Juu walikwenda kumpigia magoti Padri Jordan Mwajombe ili afute msimamo wake na badala yake atoe maji kwa wananchi, lakini alikataa kabisa na kuwafokea kama watoto wadogo viongozi hao.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Luafyo Juu Mzee Thadei Exavery Mwinuka (70) kwa upande wake alisema anayo miaka zaidi ya thelathini katika eneo hilo na muda wote wananchi wake wamekuwa wakitumia maji hayo yaliyoletwa kwa ushikiano wa wenyeji na wamisionari wazungu.
Mzee Mwinuka alisema sababu za wananchi kukata mabomba haya ni kunatokana na ukatili wa Paroko wa Parokia ya Lugarawa Padri Jordan Mwajombe kuwakatia wananchi maji bila kuwasiliana nao huku akitumia ukali kila anapofuatwa kutoa maji. Hata hivyo alimtaka na kumsisitizia Paroko kufungua maji yatumike na wananchi wote kama zamani.
Baadhi ya wananchi waliokutwa katika eneo yalipokatwa mabomba hayo Bathlomeo Mgina, John Haule (75), Benjamin Chengula, Pangista Mtweve na Vestina Mtweve walisema wanalazimika kuchota maji yasiyosalama mtoni kwa sababu Paroko amefunga maji na kwamba asipofungua maji mgogoro utakua mkubwa sana.
Aidha, wananchi hao walimrushia lawama Paroko na mafundi wake waliotajwa kwa jina mmoja mmoja kama John na Mligo ambao amewagawia maji kwa manufaa binafsi bila mawasiliano na kwamba Paroko huyo amekuwa mkali kila anapofuatwa na viongozi.
Awali, akizungumza kwa njia ya simu na mwandishi  kutaka kujua kiini cha tatizo Pd. Jordani Mwajombe kwa upande wake alisema hajawahi kumwona mtu yeyote akienda kwake kuomba maji na kwamba huo ni unafiki wa watu na hakutaka kutoa maelezo zaidi.
Erasto Mhagama ni Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Lugarawa alisema ameenda kwa Paroko mara kadha na kuamua kumpigia magoti mwenyewe, ili awape wananchi maji wananchi kumaliza mgogoro, lakini ilishindikana kutokana na kauli za ukali anazotumia mchunga kondoo huyo.
Bw. Mhagama alitoa wito kwa mchungaji huyo wa kiroho kuacha ubabe badala yake akubali kukaa na wananchi ili kumaliza mgogoro. Akaongeza kuwa “Kama Paroko atakataa kukaa na wananchi siku ya Ijumaa August 26 na kufanya makubaliano mimi sitajihusisha na sakata hilo tena,” alisema Mhagama.
Hata hivyo, baada ya wananchi hao kumbana na kuonesha msimamo wao Pd. Mwajombe alikubali kuhudhuria mkutano wa hadhara uliofanyika August 26 katika Kitongoji cha Luafyo Juu alipobanwa na kuambiwa ukweli na akasalimu amri na kuahidi kutoa maji kwa wanakijiji hao.
Chanzo cha maji hayo ni Idokonya ambako ndiko shambani kwa mwenyekiti wa kitongoji cha Luafyo Juu na kwamba wananchi wake walishiriki kwa kuchimba mtaro na wazungu walipokuwa wakijenga Mission ya Lugarawa.
Mwisho

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...