MAHABUSU 87
kutoka Ethiopia wanaoshikiliwa na Idara ya Uhamiaji katika Gereza la Ibihi
lililoko nje kidogo ya mji wa Ludewa wamegoma tena kula siku ya nne sasa huku
wengine watatu wakitundikiwa madripu ya maji na chakula katika Hospitari ya
Wilaya ya Ludewa.
Mkuu wa Gereza
hilo Mrakibu wa Magereza (ASP), Babilas Masimo kwa upande wake alikiri kutokea
kwa mgomo huo kwa mara ya tatu tena, lakini hakuwa tayari kuzungumzia suala
hilo kwa kusema kuwa yeye alikwisha kuwajulisha wanaohusika na maamuzi.
Mganga Mkuu wa
Hospitari ya Wilaya ya Ludewa, Dkt. Happines Ndosi alikiri kuwapokea mahabusu
watatu wakiwa wamedhoofu kwa njaa ambapo miongoni mwao mmoja alikutwa na Malaria
ingawa siyo ugonjwa uliomfikisha hospitalini hapo.
Dkt. Ndosi
amelalamikia kitendo cha kuendelea kuwashikilia mahabusu hao kuwa kinawamalizia
dawa kwa sababu hawamo kwenye bajeti waliyonayo na kwamba analazimika kuchukua
dripu za akina mama wajajwazito na wagonjwa wengine bila sababu ya msingi.
Mganga Mkuu
huyo aliishauri serikali kama haina mpango wa kuwarejesha makwao au kuwaacha
waendelee na safari ni afadhali waje wachukuliwe na kuwekwa katika gereza la mkoa
kwa sababu kule watapata huduma kwa urahisi.
Mwezi uliopita
mahabusu hawa waligoma wengi tulilazimika kutumia hata dripu na madawa ya akiba
sasa kama hali itaendelea kama ilivyo tutashindwa kuwahudumia wananchi
wanaokuja kutibiwa kwa magonjwa mbalimbali.
Wahabeshi hao
wamewaambukiza mahabusu wa Kitanzania kugoma ambapo Julai 2 mwaka huu waligoma
kuondoka mahakamani wakitaka kuonana na Mkuu wa Wilaya ili waweze kumweleza
kero zao na kusababisha taflani mahakamani hapo.
Ludewa imekuwa
ndiyo kichochoro rahisi cha kupita wahamiaji haramu kutoka Ethiopia ambapo
katika kipindi cha mwaka mmoja tu wakimbizi zaidi ya mia moja hamsini
wamekamatwa Manda mwambao wa Ziwa Nyasa wakiwa na boti kuelekea Malawi na
Afrika Kusini.
MKUU wa Wilaya
ya Ludewa mkoani Iringa Bi. Georgina Bundala amepuuza maazimio na agizo la
Baraza la Madiwani lililomtaka kuwakutanisha na Kamishna wa Madini Kanda ya
Mbeya ili kujua sababu zinazopelekea wachimbaji na watafiti kuvamia maeneo
mbalimbali ndani ya Wilaya hiyo bila wananchi kujulishwa na badala yake
amemleta kamishna huyo kimyakimya na kuanza kumtembeza na kufanya mikutano ya
hadhara kwa badhi ya Kata tu.
Katika Baraza
Kuu la Madiwani (Fully Council) lililofanyika Ijumaa Julai 15 mwaka huu madiwani
waliazimia na kuitaka ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi kumwandikia barua
kamishina wa madini kanda ya Mbeya kufika Ludewa na kukutana kwanza na madiwani
hao ili kujua nini kinaendelea wilayani mwao, sheria za madini zinasemaje
kuhusu stahili na haki za mwananchi kwa watafiti na wachimbaji madini.
Katika Baraza
hilo la madiwani Bi. Georgina Bundala alikuwa mgeni rasmi na baada ya kufungua
baraza hilo aliondoka na kuwakilishwa na Afisa tawala wa Wilaya Bw. John Mahali
na alitoa taarifa kuwa ofisi ya Mkuu wa Wilaya imewasiliana na madini kanda ili
aje kutoa elimu kwa madiwani na baadaye kwa wananchi na baada ya elimu hiyo
wananchi wataelewa haki zao.
Maazimio na
maagizo ya madiwani hao yanatokana na madiwani hao chini ya mbunge wao kufanya
ziara ya kushtukiza katika Kata ya Iwela ambako wananchi walilalamikia hatua ya
watafiti na wachimbaji madini kuingia eneo hilo na mitambo bila taarifa jambo
lililoleta usumbufu kwa wananchi.
Kamishna
Msaidizi wa Madini Kanda Bw. John Shija alisema Sheria na Kanuni za Madini ziko
wazi, kwamba mtu anapopewa shughuli ya utafifiti au uchimbaji, lazima aende
kwenye mamlaka husika, kwa Mkuu wa Wilaya ambaye humpeleka kwa Mkurugenzi wa
Halmashauri husika, naye kuwafikisha na kuwatambulisha mpaka ngazi ya kijiji au
eneo husika ili kuondoa migongano.
Bw. Shija
aliongeza kuwa baada ya mtafiti au mchimbaji huyo kufika katika Serikali ya
Kijiji husika ndipo wanakaa pamoja na kuangalia na kuainisha ni lini shughuli
za utafiti au uchimbaji zitaanza na hatimae kuwajulisha wananchi na mtu asiyepiga
hodi kwa mwenyeji huyo ni mvamizi.
“Hao watu
waliokuja kutafiti katika Kata ya Iwela walifika ofisi ya kanda tukawapa barua
ya kuwatambulisha kwa Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, sasa kilichoendelea huko sisi
hatuhusiki kabisa kwa sababu hiyo ni mamlaka nyingine,” alisema Bw. Shija kwa
msisitizo.
Bi. Monica
Mchiro Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri Wilaya ya Ludewa, ambaye pia ni Diwani
wa Kata ya Ludewa aliwaambia wananchi kuwa suala la kuingia watafiti na
wachimbaji madini hata madiwani hawana taarifa ndiyo maana waliingia gharama na
kwenda kujionea hali halisi kule Iwela. “Kama utaratibu huu ungefuatwa
Halmashauri isingeingia gharama ya kuwasafirisha madiwani wote 34 na wabunge
wawili kwenda eneo la tukio huu ni uzembe” alisikitika Monica.
Nao wananchi
waliohudhuria mkutano huo wa hadhara katika viwanja vya stendi walisema tatizo
siyo watafiti na wachimbaji tatizo liko kwa Mkuu wa Wilaya kuwakumbatia
wawekezji hao kwa maslahi binafsi, kwanini hawakufuata utaratibu kama
alivyoelekeza kamishna wa madini Bw. Shija ambaye ni muwazi.
“Mkuu wa
Wilaya na Mkurugenzi wao ni wapita njia tu wanafanya haya kwa maslahi yao
binafsi ili baadaye tutakapokuwa tumeanza mvutano kati ya mwekezaji na wananchi
wao watakuwa wameshahama” alilalamika Mzee Timothy Mtitu.
Hata hivyo
pamoja na kamishna wa madini kanda kuanika utaratibu unaotakiwa kufuatwa Mkuu
wa Wilaya aligeuka bubu na kushindwa kueleza lolote kuhusu alichokifanya kwa
watafiti wa Kata ya Iwela, alichokumbuka ni kumfukuza mwandishi wa habari
asipige picha mkutanoni hapo kana kwamba kulikuwa na usiri wowote.
“Mimi swali
langu ni moja tu kwako Mkuu wa Wilaya naomba ujibu tujue wote kama kweli wewe
unatenda kazi zako kwa haki, taratibu na sheria kwanini umemkataze mwandishi wa
habari kufanyakazi yake katika mkutano huu wa hadhara,” aliuliza kwa jazba Bw.
Amani Chaula.
Kwa mujibu wa
kamishna wa madini maeneo mengi katika Wilaya ya Ludewa yamepewa vibali vya
utafiti, lakini hadi sasa hakuna aliyeanza kuchimba na kuongeza kuwa
kilichelewesha kuchimba makaa ya mawe ni kutokana na madini hayo kutegemeana,
ndiyo maana serikali imeamua mwekezaji anayetaka makaa lazima awekeze pia
katika chuma ili kwenda sambamba.
HAKUNA haja ya
kuendekeza makundi kwa lengo la kuibomoa chama ambacho msingi wake ni umoja,
mshikamano na kuinuana kwa waandishi.
Hayo yalisemwa na
aliyemaliza muda wake Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoani Iringa
(IPC), Keneth Simbaya wakati wa uchaguzi wa viongozi wapya uliofanyika
mwishoni mwa wiki mkoani hapa.
Simbaya alisema kuwa
kumekuwa na baadhi ya wananchama kuamua kuunda kundi lao kwa kudanganyana
wengine na kusababisha baadhi ya wanachama na kuwasihi wanachama kujenga imani ndogo
ndani ya chama na kusababisha wengine kuamua kutojiunga na chama.
Alisema kuwa hakuna mtu
aliye bora kuliko mwingine ni lazima kila mwananchma kujishusha na kukubaliana
kwa lengo moja la kuwasaidia walio chini ili wafike wanapostahili kwa kuwapatia
mafunzo na uzoefu zaidi mbali na elimu aliyoipata shuleni.
“Mungu aliumba watu wa
aina mbalimbali na aliwapenda sana walio wanyonge na hata akawaumba wakawa
wengi pia aliwapenda kuliko wengine ni dhahiri na sisi kufuata mfano wa Mungu,”
alisema.
Vile vile, alisema kuwa katika uchaguzi huu ni lazima
kila atakayekuwa kiongozi ni lazima awe na hekima na busara kwani sisi tulioko ndani
hatuweza kujua mema mabaya yanaonekana nje wanawapokea kwa namna gani.
Hata hivyo, alisema kuwa
kila kiongozi ajue kuwa hiki ni chombo chetu sote katika kuijenga kwa kushirikiana
kwani mkiwa wamoja kwa wanachama na viongozi ni lazima tusonga mbele zaidi na
kumtakuwa na ongezeko la wananchama.
“Kiongozi mzuri ni yule
anayejifunza kila mara hivyo ni wakati sasa wa kuunganisha akili zetu
zitasaidia kuliko kutegemea akili ya mtu moja,” alisema Simbaya.
Aidha, alisema kuwa
fikra za mwananchma ni lazima zitumike katika kupata viongozi bora na pia uwe
na maamuzi sahihi ya kufikiria kuwa baada ya uchaguzi ni nini kitatokea ili kuendeleza
chama.
Uchaguzi wa Chama cha
Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa kikatiba unafanyika mara baada ya miaka 3
ambayo katika uchaguzi huo umefanyikiwa kupata viongozi wengine katika nafasi
za Mwenyekiti, Mwenyekiti Msaidizi, Katibu, Katibu Msaidizi , Mweka
hazina, Mweka hazina msaidizi.
Matokeo ni kwamba
Mwenyekiti alichaguliwa Daudi Mwangozi, Makamu Mwenyekiti Zulfa
Shumary, Katibu Mtendaji Frank Leonard, Makamu Fransic Godwin,
Mweka hazina Selemani Boki na makamu Vicky Macha.