MAHABUSU 87
kutoka Ethiopia wanaoshikiliwa na Idara ya Uhamiaji katika Gereza la Ibihi
lililoko nje kidogo ya mji wa Ludewa wamegoma tena kula siku ya nne sasa huku
wengine watatu wakitundikiwa madripu ya maji na chakula katika Hospitari ya
Wilaya ya Ludewa.
Mkuu wa Gereza
hilo Mrakibu wa Magereza (ASP), Babilas Masimo kwa upande wake alikiri kutokea
kwa mgomo huo kwa mara ya tatu tena, lakini hakuwa tayari kuzungumzia suala
hilo kwa kusema kuwa yeye alikwisha kuwajulisha wanaohusika na maamuzi.
Mganga Mkuu wa
Hospitari ya Wilaya ya Ludewa, Dkt. Happines Ndosi alikiri kuwapokea mahabusu
watatu wakiwa wamedhoofu kwa njaa ambapo miongoni mwao mmoja alikutwa na Malaria
ingawa siyo ugonjwa uliomfikisha hospitalini hapo.
Dkt. Ndosi
amelalamikia kitendo cha kuendelea kuwashikilia mahabusu hao kuwa kinawamalizia
dawa kwa sababu hawamo kwenye bajeti waliyonayo na kwamba analazimika kuchukua
dripu za akina mama wajajwazito na wagonjwa wengine bila sababu ya msingi.
Mganga Mkuu
huyo aliishauri serikali kama haina mpango wa kuwarejesha makwao au kuwaacha
waendelee na safari ni afadhali waje wachukuliwe na kuwekwa katika gereza la mkoa
kwa sababu kule watapata huduma kwa urahisi.
Mwezi uliopita
mahabusu hawa waligoma wengi tulilazimika kutumia hata dripu na madawa ya akiba
sasa kama hali itaendelea kama ilivyo tutashindwa kuwahudumia wananchi
wanaokuja kutibiwa kwa magonjwa mbalimbali.
Wahabeshi hao
wamewaambukiza mahabusu wa Kitanzania kugoma ambapo Julai 2 mwaka huu waligoma
kuondoka mahakamani wakitaka kuonana na Mkuu wa Wilaya ili waweze kumweleza
kero zao na kusababisha taflani mahakamani hapo.
Ludewa imekuwa
ndiyo kichochoro rahisi cha kupita wahamiaji haramu kutoka Ethiopia ambapo
katika kipindi cha mwaka mmoja tu wakimbizi zaidi ya mia moja hamsini
wamekamatwa Manda mwambao wa Ziwa Nyasa wakiwa na boti kuelekea Malawi na
Afrika Kusini.
No comments:
Post a Comment