Katika Baraza
Kuu la Madiwani (Fully Council) lililofanyika Ijumaa Julai 15 mwaka huu madiwani
waliazimia na kuitaka ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi kumwandikia barua
kamishina wa madini kanda ya Mbeya kufika Ludewa na kukutana kwanza na madiwani
hao ili kujua nini kinaendelea wilayani mwao, sheria za madini zinasemaje
kuhusu stahili na haki za mwananchi kwa watafiti na wachimbaji madini.
Katika Baraza
hilo la madiwani Bi. Georgina Bundala alikuwa mgeni rasmi na baada ya kufungua
baraza hilo aliondoka na kuwakilishwa na Afisa tawala wa Wilaya Bw. John Mahali
na alitoa taarifa kuwa ofisi ya Mkuu wa Wilaya imewasiliana na madini kanda ili
aje kutoa elimu kwa madiwani na baadaye kwa wananchi na baada ya elimu hiyo
wananchi wataelewa haki zao.
Maazimio na
maagizo ya madiwani hao yanatokana na madiwani hao chini ya mbunge wao kufanya
ziara ya kushtukiza katika Kata ya Iwela ambako wananchi walilalamikia hatua ya
watafiti na wachimbaji madini kuingia eneo hilo na mitambo bila taarifa jambo
lililoleta usumbufu kwa wananchi.
Kamishna
Msaidizi wa Madini Kanda Bw. John Shija alisema Sheria na Kanuni za Madini ziko
wazi, kwamba mtu anapopewa shughuli ya utafifiti au uchimbaji, lazima aende
kwenye mamlaka husika, kwa Mkuu wa Wilaya ambaye humpeleka kwa Mkurugenzi wa
Halmashauri husika, naye kuwafikisha na kuwatambulisha mpaka ngazi ya kijiji au
eneo husika ili kuondoa migongano.
Bw. Shija
aliongeza kuwa baada ya mtafiti au mchimbaji huyo kufika katika Serikali ya
Kijiji husika ndipo wanakaa pamoja na kuangalia na kuainisha ni lini shughuli
za utafiti au uchimbaji zitaanza na hatimae kuwajulisha wananchi na mtu asiyepiga
hodi kwa mwenyeji huyo ni mvamizi.
“Hao watu
waliokuja kutafiti katika Kata ya Iwela walifika ofisi ya kanda tukawapa barua
ya kuwatambulisha kwa Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, sasa kilichoendelea huko sisi
hatuhusiki kabisa kwa sababu hiyo ni mamlaka nyingine,” alisema Bw. Shija kwa
msisitizo.
Bi. Monica
Mchiro Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri Wilaya ya Ludewa, ambaye pia ni Diwani
wa Kata ya Ludewa aliwaambia wananchi kuwa suala la kuingia watafiti na
wachimbaji madini hata madiwani hawana taarifa ndiyo maana waliingia gharama na
kwenda kujionea hali halisi kule Iwela. “Kama utaratibu huu ungefuatwa
Halmashauri isingeingia gharama ya kuwasafirisha madiwani wote 34 na wabunge
wawili kwenda eneo la tukio huu ni uzembe” alisikitika Monica.
Nao wananchi
waliohudhuria mkutano huo wa hadhara katika viwanja vya stendi walisema tatizo
siyo watafiti na wachimbaji tatizo liko kwa Mkuu wa Wilaya kuwakumbatia
wawekezji hao kwa maslahi binafsi, kwanini hawakufuata utaratibu kama
alivyoelekeza kamishna wa madini Bw. Shija ambaye ni muwazi.
“Mkuu wa
Wilaya na Mkurugenzi wao ni wapita njia tu wanafanya haya kwa maslahi yao
binafsi ili baadaye tutakapokuwa tumeanza mvutano kati ya mwekezaji na wananchi
wao watakuwa wameshahama” alilalamika Mzee Timothy Mtitu.
Hata hivyo
pamoja na kamishna wa madini kanda kuanika utaratibu unaotakiwa kufuatwa Mkuu
wa Wilaya aligeuka bubu na kushindwa kueleza lolote kuhusu alichokifanya kwa
watafiti wa Kata ya Iwela, alichokumbuka ni kumfukuza mwandishi wa habari
asipige picha mkutanoni hapo kana kwamba kulikuwa na usiri wowote.
“Mimi swali
langu ni moja tu kwako Mkuu wa Wilaya naomba ujibu tujue wote kama kweli wewe
unatenda kazi zako kwa haki, taratibu na sheria kwanini umemkataze mwandishi wa
habari kufanyakazi yake katika mkutano huu wa hadhara,” aliuliza kwa jazba Bw.
Amani Chaula.
Kwa mujibu wa
kamishna wa madini maeneo mengi katika Wilaya ya Ludewa yamepewa vibali vya
utafiti, lakini hadi sasa hakuna aliyeanza kuchimba na kuongeza kuwa
kilichelewesha kuchimba makaa ya mawe ni kutokana na madini hayo kutegemeana,
ndiyo maana serikali imeamua mwekezaji anayetaka makaa lazima awekeze pia
katika chuma ili kwenda sambamba.
No comments:
Post a Comment