Friday, 13 January 2017

HALMASHAURI YAIFUNGIA KWA MUDA USIOJULIKANA SHULE YA MSINGI HAZINA MISION ...





Na Woinde Shizza,Arusha



HALMASHAURI ya jiji la Arusha imeifungia kwa muda usiojulikana shule ya msingi Hazina Mision iliyopo kata ya Baraa mara baada ya uongozi wa shule hiyo kushutumiwa kwa makosa mbali mbali ikiwemo kuwatelekeza watumishi wake pamoja na mindombinu kuwa chini ya viwango vinavyohitajika katika uandikishaji wa shule.

Hatua hiyo ya kufungiwa kwa shule hiyo imekuja mara baada siku chache zilizopita wamiliki wa shule hiyo kulalamikiwa kuwanyanyasa na kushindwa kuwalipa mishahara watumishi na walimu wa shule hiyo na hivyo kutakiwa kufanya marekebisho na kuwalipa stahiki watumishi lakini wakakaidi kufanya maagizo hayo kwa muda waliopewa.

Akitoa agizo hilo katika viwanja vya shule hiyo kaimu afisa elimu shule za msingi katika jiji la arusha Eunice Elibariki alisema kuwa wameamua kusimamisha huduma ya utoaji elimu kutokana na shule hiyo kushindwa kufanya marekebisho waliyotakiwa kuyafanya shuleni hapo.

Alisema kuwa awali kabla hatua hiyo haijafikiwa walipata taarifa kuwa uongozi wa shule hiyo inawanyanyasa walimu kwa kuwanyima mishahara yao, kutokuwa na mindombinu kuachilia viwango pamoja na kuwepo uchafuzi wa mazingira na ndipo uongozi ukapewa muda wa kufanya marekebisho hayo pamoja na kimaliza migogoro ya kimaslahi lakini walikaidi kutoa ushirikiano hali iliyopelekea halmashauri hiyo kuchukua hatua ya kusimamisha utoaji huduma.

"Kwa kuwa uongozi wa shule hii mlishindwa kufanya marekebisho mlioagizwa ikiwa ni pamoja na kishindwa kumaliza migogoro ya walimu kuanzia sasa nasimamisha huduma za masomo hadi hapo mtakapoweza kuiweka shule yenu katika mazingira yanayohitajika kwani lazima shule iwe na viwango na sifa zinavyohitajika sio tu kuendesha kiholela "alisema Eunice

Wananchi wa eneo hilo akiwemo Diwani wa kata ya baraa Elifasi Ndetika akizungumzia uamuzi wa kufungiwa kwa shule hiyo alisema kuwa ni halali kabisa kwani walikuwa na malundano ya muda mrefu baina ya uongozi na walimu lakini walishindwa kumaliza wenyewe huku akidai kuwa mazingira yalikuwa hayadhirishi na hivyo kupitia usimamishaji huo unaweza kupelekea marekebisho yakawepo.

WANAFUNZI 17,549 KUJIUNGA NA ELIMU YA SEKONDARI MKOANI IRINGA

Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu (kushoto) ambaye pia ni Katibu wa Kikao cha Kamati ya Ushauri cha Mkoa (RCC) akisoma taarifa katika kikao hicho huku Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza ambaye pia mwenyekiti wa kikao hicho akifuatilia kwa makini leo. 







Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Iringa, Suzana Mgonukulima (CHADEMA) na Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kusini, Menrad Kigola (CCM) wakibadilishana mawazo nje ya Ukumbi wa Siasa ni Kilimo wakati wa Kikao cha Kamati ya Ushauri cha Mkoa wa Iringa (RCC kilichofanyika leo  (PICHA NA FRIDAY SIMBAYA)





IRINGA: Jumla la wanafunzi 17,549 mkoani Iringa (wavulana 7,988 na wasichana 9,561) sawa na mkiondo 439 watajiunga kidato cha kwanza mwaka 2017, imeelezwa.

Hayo yalisemwa na Kaimu Afisa Elimu wa Mkoa wa Iringa Richard Mfugale (pichani) wakati wa Kikao cha Kamati ya Ushauri cha Mkoa (RCC) kilichofanyika leo mjini Iringa.

Kaimu afisa elimu huyo alisema kuwa wanafunzi wote waliofauli wamechaguliwa kujiunga elimu ya sekondari mkoani iringa, ambapo aliongeza kuwa halmashauri zote zinaendelea na maandalizi ya kupokea wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza.

Mfugale alisema kuwa ufaulu wa mtihani wa kidato cha nne kimkoa umepanda kutoka asilimia 65.25 mwaka 2013 hadi asilimia 72.34 mwaka 2015, hali kadhalika kwa halmashauri ya manispaa ya iringa na halmashauri ya wilaya ya iringa ufaulu umekuwq ukiongezeka. 

Kwa upande wa mtihani wa kidato cha sita, Mfugale alifafanua kuwa kati ya wanafunzi 4,142 waliohitmu kidato hicho, wanafunzi 4,055 sawa na asilimia 97.88 ya walifauli kwa kiwango cha daraja la kwanza hadi la nne.

Alifafanua kuwa kati yao hao waliofauli asilimia 95.6 waliofaulu kwa daraja la kwanza hadi la tatu wamechaguliwa kujiunga na vyuo vikuu na vyuo vingine nchini.

Wakati huohuo, mjumbe wa kikao hicho, Mendrad Kigola ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kusini alisema kuwa ili kuwepo boreshaji elimu, halmashauri za wilaya hazinabudi ya kutenga kiasa cha pesa kutoka katika kwenye bajeti zao kwa ajili ya maendeleo ya elimu.

Alisema kuwa ili kuunga juhudi za serikali katika sera yake ya elimu bure ni lazima halmashauri zitoe mchango wake.

Aidha, mjumbe huyo alishauri pia kuwa kuwepo na jitihadi za makusudi mazima za kutoa elimu kwa wazazi na walezi kuhusu elime bure ili kupunguza malalamiko na mkanganyiko uliopo wa suala la sera ya elimu bure.





SIASA ZA CHUKI NA CHAFU HAZIWEZI KULETA MAENDELEO KATIKA TAIFA LETU




Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi Taifa wa Chama cha Wananchi (CUF), Mhandisi Shaban Kaswaka (kushoto), akimtambulisha kwa wananchi Mgombea Udiwani kupitia chama hicho Kata ya Kijichi, Abdallah Shamas katika mkutano wa kampeni uliofanyika eneo la Mwanamtoti Temeke jijini Dar es Salaam jana.





Wafuasi wa CUF wakimkaribisha mgombea udiwani wa Kata ya Kijichi wakati alipokuwa amewasili kwenye mkutano wake wa kampeni.



Meza kuu katika mkutano huo.






Mkutano ukiendelea.



Wafuasi wa chama cha CUF wakiinua mikono kukubali kumpigia kura mgombea wa chama hicho.






Na Dotto Mwaibale


MGOMBEA Udiwani Kata ya Kijichi kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Abdallah Khalid Shamas amewataka wananchi na wagombea wenzake kuacha siasa za chuki na chafu ili kuiletea maendeleo kata hiyo na taifa kwa ujumla.


Shamas alitoa ombi hilo wakati wa mkutano wake wa kampeni uliofanyika eneo la Mwanamtoti Kijichi Dar es Salaam jana wakati akijinadi kwa wapiga kura.


"Siasa chafu za chuki na zinazowatenganisha wananchi kutokana na itikadi za vyama vyao hazifai na haziwezi kuleta maendeleo katika kata hiyo na taifa kwa ujumla" alisema Shamas.


Alisema siasa chafu zilizokuwepo katika eneo hilo la Mwanamtoti zilifikia hatua ya kugawana makaburi jambo ambalo lilikuwa ni hatari katika kushirikiana.


Akizungumzia baadhi ya vipaumbele vyake iwapo atachaguliwa kuwa diwani wa kata hiyo alisema cha kwanza ni kuhakikisha eneo la Mwanamtoti wanapata shule ya msingi ambayo itawasaidia watoto wa eneo hilo kutotembea umbali mrefu wa kwenda shuleni.


Alitaja kipaumbele chake cha pili ni kuhakikisha eneo hilo linapata zahanati pamoja na kukaa na wataalamu wa taasisi za fedha kuona namna ya kuanzisha Saccos au chombo cha fedha ili kuweza kutoa fursa kwa wananchi wa kata hiyo kukopa na kufanikisha maendeleo yao.



Mgombea huyo amewaomba wananchi wa eneo hilo Januari 22, mwaka huu wamchague ili awatumikie baada ya kata hiyo kukosa maendeleo kwa zaidi ya miaka 20.



Uchaguzi huo mdogo wa ngazi ya udiwani unafanyika katika kata hiyo kufuatia aliyekuwa diwani kufariki dunia mapema mwaka jana na nafasi hiyo kuwa wazi.



WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...