Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Celestine Mushy akizungumza machache kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema (katikati) kabla ya kuanza zoezi la usafi katika soko la Temeke Stereo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 70 ya Umoja wa Mataifa. Kushoto ni Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez.(Picha zote na Zainul Mzige wa Modewjiblog)
Na Mwandishi wetu
KATIKA kuadhimisho miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa (UN) wafanyakazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Kimataifa walijumuika na wakazi wa Temeke katika kufanya usafi kwenye soko la Temeke Stereo.
Shughuli hiyo wameifanya baada ya wiki iliyopita kufanya shughuli za upandaji miti katika miteremko ya mlima Kilimanjaro. Wakiwa katika miteremko ya milima Kilimanjaro walipanda miti 2,000.
Shughuli hizo za kufanya usafi ambazo ziliongozwa na Mratibu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Alvaro Rodriguez, zilifanyika katika juhudi za kuleta uhalisia wa utunzaji wa mazingira kama umoja huo unavyofanya.
Akizungumza katika shughuli hizo Mkuu wa wilaya ya Temeke, Sophia Mjema, ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa aliupongeza Umoja wa Mataifa kwa kusherehekea miaka 70.
“Nachukua nafasi hii kupongeza watu wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania kwa kufanya shughuli mbalimbali kuelekea maadhimisho ya miaka 70 kwa kupanda miti 2,070 kwenye miteremko ya Mlima Kilimanjaro na hili tendo la leo la usafi kama mwendelezo wa kaulimbiu inayohimiza utunzaji wa mazingira ya“ Sayari moja, watu bilioni 7: Ulinzi wa mazingira ni wajibu wetu,” alisema.
Akisisitiza umuhimu wa kutunza mazingira na usafi, Mkuu huyo wa wilaya alisema wajibu wa kutunza mazingira ni wa kila mtu.
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez akitoa salamu za Umoja wa Mataifa katika kuadhimisha miaka 70 ya Umoja wa Mataifa ikiwemo kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii kwa wananchi na wafanyabiashara wa soko la Temeke Stereo mwishoni mwa juma. Kushoto ni Kaimu Mwakilishi Mkazi wa FAO nchini, Patric Otto. Wa tatu kulia ni mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya Temeke, Sophia Mjema, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Celestine Mushy (wa pili kulia) na Mkuu wa Idara ya Usafi na Mazingira manispaa ya Temeke, Ally Hatibu.