Na Basil Makungu,
Ludewa
IKIWA imetimia zaidi ya wiki moja tangu kuuawa kwa Rais wa zamani wa Libya Muamar Gadaffi, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea Norbert Mtega amewataka viongozi wa Afrika kujali na kuheshimu haki za raia wao kwani mwenye kuua kwa upanga hufa kwa upanga.
Askofu Mkuu Mtega aliyasema hayo jana katika Misa ya shukrani na sherehe yake ya kutimiza miaka 25 ya uaskofu iliyofanyika katika Parokia ya Yesu Kristo Mkombozi, lililoko mjini Ludewa mkoani Iringa.
Askofu Mtega alisema yeye anachukia sana viongozi wenye dhuruma kwa raia wake na kuwataka viongozi wa Afrika kuacha ubabe, kuacha unafiki na kwamba tukio la Libya liwe changamoto kwao na kuwataka waache kuendesha nchi kama asasi binafsi kwani wananchi wanapochoka kwao kila kitu ni silaha.
“Tazameni na oneni enyi viongozi wa Afrika jinsi kiongozi mwafrika ambaye amepewa nafasi na dhamana ya kuongoza wananchi anavyoweza kukosea na kupitiwa kwa ulevi wa madaraka huku anasema yeye anawapenda watu wake huku akiendelea kuwaua,”alihuzunika Baba Askofu.
Askofu Mtega aliwaambia viongozi wa Afrika kuwa kuongoza nchi ni dhamana wanayopewa na mwenyezi Mungu kupitia watu wao, ili uongoze watu lazima kwanza uwapende, uwaheshimu, utambue na kuthamini utu na haki za Binadamu na kuthamini kwa kugawana kwa usawa kile kilichopo bila upendeleo.
Alisema fursa sawa kwa wote ndiyo silaha kwa kiongozi, lakini anapoanza kupotoka na kujitazama yeye binafsi au familia yake na marafiki huku watu wa kawaida hasa masikini hawana kitu na ndiyo maana wanapokuwa wamechoka na kugundua haki zao hutumia umoja wao kama silaha.
Mtega aliwataka viongozi wa Afrika kuwajibika katika kuongoza nchi zao kwa kuzikabili mapema kero za wananchi na mambo yote yanayochukiza na kuchokoza raia, wasingoje mpaka waje kujaa hasira na jazba kwani hatua hiyo hupelekea kutenda vitendo vya mauaji watambue wajibu zao zinatoka kwa Mungu.
Akizungumzia kifo cha Rais wa Libya aliyeondolewa madarakani kwa kuuawa na majeshi ya NATO Muamar Gadaffi, Askofu Mkuu Mtega alisema kuuawa kwake ni tukio litakalobadilisha historia ya wana Libya.
Alisema tunasikitika kuuawa kinyama, lakini alikwisha pewa nafasi na fursa nyingi za kujisalimisha ili asiuawe, lakini alikaidi na kuendelea kung’ang’ania.
Ameua watu wengi sana wa Taifa lake bila ya hatia wala sababu yoyote ya msingi.
Aidha, amewataka wanaLibya wakae chini kwanza wapoe, watulize hasira, jazba na chuki yao na kwamba kama walimchukia Gadaffi kwa mambo na vitendo vyake viovu, basi mambo hayo wasiyatende wala kuyaendeleza kwa kuua, kugombanisha, na kuchukia watu.
Alisema kama Wana Libya watakaa pamoja na kuunda Serikali ambayo itatazama suala la upatanishi, upendo, ushirikiano, na umoja wa kitaifa itakuwa na mwanzo mzuri kuliko kuanza kulipa visasi kwa wale wote waliokuwa wafuasi wa Gadaffi.
Aliongeza kuwa Libya inakabiliwa na changamoto nyingi sana kwa sababu Gadaffi tunafahamu kwa ujanja wake alikuwa na wafuasi wengi na hata marafiki wa nje na ndani ya nchi yake kwa hiyo ni matumaini yetu kuwa Serikali mpya itatambua umuhimu wa upatanisho hakuna njia nyingine zaidi ya kusahau ugomvi na chuki na sasa waanze kulijenga Taifa lao ambalo limebomolewa sana.
Tuesday, 25 October 2011
Subscribe to:
Posts (Atom)
WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...
Na Friday Simbaya, Mufindi Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...
-
KIKUNDI cha Upendo ni kikundi cha kina mama 20 walioamua kujiunga kwa pamoja na kuanz...
-
Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini MIEMBE hulimwa karibu katika nchi zote zilizoko kwenye ukanda wa joto, na hasa tropiki. Nchini ...
-
Habari ndugu msomaji wetu wa blog, Natumaini unaendelea vyema. Leo tutaanza kujifunza kilimo cha bora cha nyanya, na tutaanza kufahamu vit...