LUDEWA
WANANCHI na watumiaji wa maji katika
Kitongoji cha Luafyo Juu Lugarawa wilayani Ludewa jana walijawa jazba na kuamua
kuyakata kwa mapanga mabomba ya maji yanayotumika pia na Kanisa Katoliki kwa
madai kuwa Paroko wao amewanyima maji bila sababu.
Awali August 23 na 24 mwaka huu Mwenyekiti wa
Kijiji cha Lugarawa Bw. Erasto Mhagama akiwa na Mwenyekiti wa Kitongoji cha
Luafyo Juu walikwenda kumpigia magoti Padri Jordan Mwajombe ili afute msimamo
wake na badala yake atoe maji kwa wananchi, lakini alikataa kabisa na kuwafokea
kama watoto wadogo viongozi hao.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Luafyo Juu Mzee Thadei
Exavery Mwinuka (70) kwa upande wake alisema anayo miaka zaidi ya thelathini
katika eneo hilo na muda wote wananchi wake wamekuwa wakitumia maji hayo
yaliyoletwa kwa ushikiano wa wenyeji na wamisionari wazungu.
Mzee Mwinuka alisema sababu za wananchi
kukata mabomba haya ni kunatokana na ukatili wa Paroko wa Parokia ya Lugarawa Padri
Jordan Mwajombe kuwakatia wananchi maji bila kuwasiliana nao huku akitumia
ukali kila anapofuatwa kutoa maji. Hata hivyo alimtaka na kumsisitizia Paroko
kufungua maji yatumike na wananchi wote kama zamani.
Baadhi ya wananchi waliokutwa katika eneo
yalipokatwa mabomba hayo Bathlomeo Mgina, John Haule (75), Benjamin Chengula,
Pangista Mtweve na Vestina Mtweve walisema wanalazimika kuchota maji
yasiyosalama mtoni kwa sababu Paroko amefunga maji na kwamba asipofungua maji
mgogoro utakua mkubwa sana.
Aidha, wananchi hao walimrushia lawama Paroko
na mafundi wake waliotajwa kwa jina mmoja mmoja kama John na Mligo ambao
amewagawia maji kwa manufaa binafsi bila mawasiliano na kwamba Paroko huyo
amekuwa mkali kila anapofuatwa na viongozi.
Awali, akizungumza kwa njia ya simu na mwandishi
kutaka kujua kiini cha tatizo Pd.
Jordani Mwajombe kwa upande wake alisema hajawahi kumwona mtu yeyote akienda
kwake kuomba maji na kwamba huo ni unafiki wa watu na hakutaka kutoa maelezo
zaidi.
Erasto Mhagama ni Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji
cha Lugarawa alisema ameenda kwa Paroko mara kadha na kuamua kumpigia magoti
mwenyewe, ili awape wananchi maji wananchi kumaliza mgogoro, lakini
ilishindikana kutokana na kauli za ukali anazotumia mchunga kondoo huyo.
Bw. Mhagama alitoa wito kwa mchungaji huyo wa
kiroho kuacha ubabe badala yake akubali kukaa na wananchi ili kumaliza mgogoro.
Akaongeza kuwa “Kama Paroko atakataa kukaa na wananchi siku ya Ijumaa August 26
na kufanya makubaliano mimi sitajihusisha na sakata hilo tena,” alisema Mhagama.
Hata hivyo, baada ya wananchi hao kumbana na
kuonesha msimamo wao Pd. Mwajombe alikubali kuhudhuria mkutano wa hadhara
uliofanyika August 26 katika Kitongoji cha Luafyo Juu alipobanwa na kuambiwa
ukweli na akasalimu amri na kuahidi kutoa maji kwa wanakijiji hao.
Chanzo cha maji hayo ni Idokonya ambako ndiko
shambani kwa mwenyekiti wa kitongoji cha Luafyo Juu na kwamba wananchi wake
walishiriki kwa kuchimba mtaro na wazungu walipokuwa wakijenga Mission ya
Lugarawa.
Mwisho
No comments:
Post a Comment