KUPANDA kiholela kwa bei za bidhaa mbalimbali
wilayani Ludewa kunatokana na idara kadhaa ndani ya Halmashauri ya wilaya hiyo
kutofanyakazi kwa ufanisi sanjari na ushirikiano hafifu uliopo kati ya idara na
idara.
Hayo yamethibitika kufuatia wafanyabiashara
ya nyama ya ng’ombe na nguruwe mjini hapa kupandisha bei ya bidhaa hiyo
kiholela huku mamlaka zinazohusika zikifumbia macho suala hilo kwa madai kuwa
hazina taarifa na wakati mwingine kutupiana mpira juu ya nani awajibike.
Kwa mujibu wa wananchi na watumiaji wa bidhaa
hiyo muhimu waliokutwa katika mabucha yaliyoko mjini hapa jana, walisema kilo
moja ya nyama ya ng’ombe mchanganyiko imefikia shilingi 5,000 badala ya 4,000
ambapo steki ni shilingi 6,000 badala ya shilingi 5,000 na kwamba bei hizo
zimeanza August 3 mwaka huu.
Kwa upande wake Afisa Biashara wilayani
Ludewa Bi Martha Mfugale alipotakiwa kueleza ni kwanini bei imepande ghafla na
kwa kiwango kikubwa alisema yeye mara ya mwisho alinunua nyama siku ya Sikukuu
ya Eid el Fitr kwa bei ya shilingi elfu
nne.
Hata hivyo alisema kama ni kweli, kiwango
kilichopandishwa ni kikubwa mno na kwamba hajui wachinjaji hao wametumia vigezo
gani kufikia bei hiyo, lakini aliahidi kufuatilia suala hilo. Wafanyabiashara
za chakula wamelalamikia bei hizo na kusema kuwa inawezekana hakuna serikali
ndiyo maana watu wanaweza kuamuka asubuhi na kujipangia bei huku wananchi wenye
kipato kidogo wasio na jukwaa la kusemea wakiendelea kuumia.
Afisa Mifugo Wilaya ya Ludewa Bw Marco
Mhagama yeye amekilaani kitendo kilichofanywa na wafanyabiashara hao wa nyama
na kusema kuna haja ya idara ya biashara na idara ya mifugo kufanya kazi kama
timu kwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara. Akifafanua kuhusu tozo na ushuru kwa
wachinja nyama hao Bw Mhagama alisema kwa sasa ushuru wa Halmashauri ni
shilingi elfu nne na mia tano kwa mchanganuo kuwa ushuru wa machinjio ni
2,000,ada ya mkaguzi yaani mtaalam ni shilingi 2,500 na serikali kuu shilingi
1,000.
Kwa upande wa nyama ya nguruwe Bw Mhagama
alisema wao hawapaswi kupandisha bei kwa sababu ushuru huo hauwagusi wao kwa
kuwa hawana machinjio maalum na kwamba hawarusiwi kutoa nguruwe nje ya kijiji
kwa hiyo hakuna gharama.
Wakitoa mapendekezo yao wananchi wameitaka
serikali kutoa bei elekezi kwa wachinjaji hao lakini wakawalaumu maafisa
biashara na wale wa mifugo kuacha kung’ang’ania kukaa maofisini na kusubiri
mishahara badala yake wafanye ukaguzi wa mara kwa mara siyo kwa wachinjaji tu
bali na katika bidhaa zingine.
Wafanyabiashara hao wa mjini Ludewa
wamejipandishia bei kiholela huku wakilaumiwa na wateja wao kwa kuchakachua
mizani inayotumika katika mabucha, huku wakitumia mikokoteni kusafirishia nyama
toka machinjoni.
No comments:
Post a Comment