Saturday, 10 September 2011

KESI YA PEMBEJEO KATI YA AFISA MTENDAJI NA KATIBU WA CCM LUGARAWA YAAHIRISHWA TENA


Ludewa

KESI ya wizi wa mbolea ya pembejeo yenye thamani ya zaidi ya milioni sita inayowakabili Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Mdilidili Bw Otmari Kayombo Komnfoti, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Lugarawa Bw Yohanes Mhagama Muafaka na wenzake imeahirishwa tena.
Akiahirisha kesi hiyo mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Ludewa Emanuel Mwambeta, Mwendesha Mashtaka Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Mtikamtika alimwambia hakimu kuwa mshtakiwa namba moja ametoa taairifa ya kuumwa.
Bw. Mtikamtika alikuwa amefika na mashahidi watatu akiwemo Askari Polisi Kitengo cha Upelelezi Bw. Kelvin Kapinga, Afisa kutoka Ofisi ya TAKUKURU Bw. Lucas Swebe na mkazi mmoja wa kijiji cha Mdilidili kwa jina la  Bonifasi Mlowe.
Katika kesi hiyo yumo pia wakala wa mbolea katika kijiji hicho Bw. Anazet Mlelwa na mwenyekiti wa pembejeo wa kijiji hicho Bi. Grace Komba ambao wote walikuwepo mahakamani hapo.
Kesi hiyo imekuwa na mvuto wa pekee kuliko kesi zingine mahakamani hapo kutokana na wananchi wengi kuguswa, kuchoshwa na unyanyasaji wanaopata kutoka kwa viongozi wa vijiji na mawakala kuhusu mbolea ya ruzuku katika maeneo yao.
Katika hati ya mashtaka washtakiwa walitenda kosa hilo Januari 5 mwaka huu majira ya saa kumi za jioni na kwamba kwa udanganyifu walikula njama na kuiba jumla ya shilingi 6,966,000/- kwa njia ya kugushi kwa kuandika majina hewa wakiwemo waliokufa, wagonjwa na watoto wadogo.
Washtakiwa wanakabiliwa na makosa mia tatu kulingana na idadi ya wananchi waliokosa na kutapeliwa mbolea katika kijiji cha Mdilidili katika Kata ya Lugarawa.
Katika kesi hiyo kosa la kwanza linaloangukia katika kifungu cha 306 linawakabili washtakiwa wote wanne ambapo kosa la pili la kugushi linawakabili Bw. Komnfoti mtendaji wa kijiji na Bi Komba chini ya vifungu vya 333,335(a) na 337 sura ya 16 inayosema Januari 5 mwaka huu washtakiwa waligushi vocha 300 za mbolea ya ruzuku.
Kesi hiyo yenye jumla ya mashahidi sita wa upande wa mashtaka imeahirishwa hadi Octoba 12 mwaka huu ambapo itakuja kwa kusikilizwa na hakimu kuagiza washtakiwa wote kuhudhuria siku hiyo bila kukosa.
Mwisho

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...