Saturday, 6 August 2016

N/WAZIRI JAFO: WATANZANIA WANAPASWA KUTHAMINI BIDHAA ZINAZOZALISHWA NCHINI


Naibu waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na serikali za mitaa TAMISEMI Jafo Suleiman Said akiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama mara baada ya kutembelea banda la Halmashauri hiyo.




Mgeni na Mwenyeji wakifurahi kufuatia maandalizi mazuri ya Maonesho ya Nane nane kanda ya kati.




Naibu waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na serikali za mitaa TAMISEMI Jafo Suleiman Said akisikiliza maelezo ya namna ya kulima kilimo na ufugaji wa kisasa




Na Mathias Canal, Dodoma

Watanzania wametakiwa kuthamini na kununua bidhaa zinazozalishwa nchini Tanzania hususani katika sekta ya Kilimo, Ufugaji na uvuvi kwani hakuna sababu ya kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi ilihali bidhaa hizo wanazoagiza zinazalishwa na watanzania wenzao.

Naibu waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na serikali za mitaa TAMISEMI Jafo Suleiman Said ameyasema hayo mara baada ya kutembelea baadhi ya mabanda katika maonyesho ya wakulima Nane nane Kanda ya kati Dodoma yanayofanyika katika uwanja wa Nzuguni huku kauli mbiu ya mwaka huu ikiwa ni "Kilimo, Mifugo na Uvuvi ni nguzo ya maendeleo, Kijana shiriki kikamilifu (Hapa Kazi Tu).

Jaffo amesema kuwa asilimia kubwa ya watanzania wamekuwa watumwa wa mambo ya kigeni, kuiga tamaduni mbalimbali ikiwemo matumizi ya bidhaa zinazotoka nje ya nchi wakati pia bidhaa hizo zinazalishwa nchini, huku akitolea mfano wa manunuzi ya viatu kutoka nchi mbalimbali wakati hapa nchini Jeshi la Magereza linatengeneza viatu bora vya ngozi tena kwa bei nafuu.

Sambamba na hayo pia Naibu Waziri huyo ameiagiza Mamlaka ya Ustawishaji Makao makuu Dodoma kusimamia vyema na kwenda na kasi kubwa katika utengenezaji wa stendi kubwa na ya kisasa ili kufanana na mji wa Dodoma ambapo pia hivi karibuni makao makuu ya serikali yatahamia mjini hapo.

Aidha ameongeza kuwa Maonesho hayo yanapaswa kuboreshwa ili maonyesho yajayo yawe ya kitaifa ambapo nchi mbalimbali zitapata fursa ya kutembelea na kuifanya Tanzania kujikomboa katika wimbi la umasikini.

Maonesho hayo yanahusisha Shughuli za wakulima, wafugaji wa mifugo, wafugaji wa nyuki, wavuvi, wana mazingira, wasindikaji wa bidhaa za mazao ya kilimo na mifugo, wizara taasisi/Makampuni ya umma, makampuni Binafsi, mabenki, taasisi za umma na za binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali.

Akitoa salamu za shukrani kwa niaba ya waandaaji wa Maonesho hayo Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida Miraji Jumanne Mtaturu amesema kuwa maandalizi ya maonyesho hayo yametumia muda mfupi lakini kwa kiasi kikubwa yamekuwa bora na kuahidi kuwa na Maonesho yajayo kuwa bora zaidi katika kipindi kinachokuja.

Mtaturu amesema kuwa lengo mahususi la maonesho hayo ni utoaji wa elimu ya matumizi ya teknolojia mbalimbali kwa wadau wengi kwa muda mfupi ambapo watajifunza kwa njia ya kuona, kujadiliana na kuulizana maswali.

Ameongeza kuwa maeneo makuu ya mafunzo ni teknolojia za uzalishaji wenye tija wa mazao, mifugo na usindikaji wa bidhaa ili kuongeza thamani.

Dc Mtaturu amesema kuwa pia wadau watajionea na kujifunza huduma zitolewazo na serikali, Mashirika ya umma na binafsi, ambapo wafanya biashara wanayatumia maonesho hayo kwa kuuza bidhaa, kufahamiana na kuingia makubaliano.

Kwa upande wake Katibu wa maandalizi ya Maonesho hayo Aziza Rajabu Mumba amesema kuwa Wanatarajia kila mwananchi atakayetembelea maonesho hayo kwenda kutekeleza kwa vitendo anayojifunza katika eneo lake na kuwafundisha wengine ambao hawakupata fursa ya kuhudhuria kwenye Maonesho hayo.

Aidha amesema Malengo ya muda mrefu ni kuendeleza uwanja wa Nzuguni ufikie ubora na hadhi ya viwanja vya maonesho ya Kilimo Kimataifa na kuendelea kushawishi wadau mbalimbali kuwekeza ili kuufanya uwanja wa Nzuguni uwe kituo cha huduma cha Maonesho ya Kilimo nchini kama ilivyo kwa uwanja wa Mwalimu Nyerere Dar es salaam kwa maonesho ya Biashara.


No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...