Wananchi wa kijiji cha Ludilo wilayani Mufindi, mkoani Iringa wamepitisha sheria ndogo ya usimamizi wa maliasili (misitu na wanyamapori) ilikukabiliana na kasi ya uharibifu wa rasilimali hizo.
Hatua hiyo ilifikiwa tarehe 4 Augusti, 2016 katika mkutano wa hadhara ambapo Diwani wa kata ya Mdabulo Mheshimiwa Henry Nyeho pamoja na Mwanasheria wa Wilaya ya Mufindi Leonard Jaka walihudhuria mkutano huo.
Sheria zilizopitishwa na wananchi hao ndio itakayotumika katika usimamizi wa maliasili.
Mchakato wa uboreshaji sheria ulianza mwezi Juni, 2016 ambapo Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) kwa kushirikiana na Mwanasheria wa Wilaya ya Mufindi pamoja na wananchi hao, kupitia mkutano wa hadhara waliangalia upya sheria zilizokuwa zikitumika kijijini hapo na kugundua kuwa zilikuwa na mapungufu.
Wananchi wakiongozwa na Wanasheria kutoka LEAT na Mwanasheria wa Wilaya Mufindi walitoa mapendekezo ya maboresho na kuiruhusu timu ya LEAT kuchapisha sheria hizo mpya ambazo ziliwasilishwa tarehe 4 August 2016.
Mtendaji wa kijiji cha Ludilo Martin Mwanule alisoma kipengele kimoja baada ya kingine kupitishwa na wananchi.
Sheria hizo zinaelekeza haki na wajibu wa wananchi, serikali ya kijiji, kamati ya maliasili pamoja na timu ya Ufuatiliaji Uwajibikaji Jamii. Pia sheria zimefafanua adhabu zitakazotolewa kwa watu watakao kiuka sheria na kuharibu maliasili.
Hii ni awamu ya kwanza ya kuzijengea uwezo serikali za vijiji wa kuunda sheria ndogo za kusimamia maliasili.
Katika awamu hii vijiji vya Ludilo, Ikangamwani na Kibada kwa wilaya ya Mufindi. Kwa wilaya ya Iringa ni vijiji vya Mbweleli, Kinyika na Kinyali.
Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) inatekeleza mradi wa Ushiriki wa Wananchi katika Usimamizi wa Maliasili katika vijiji 32 vya wilaya za Iringa na Mufindi mkoani Iringa.
Mradi huu umefadhiliwa na Watu wa MArekani kupitia Shirika la Kimataifa la Maendeleo la MArekani (USAID).
Lengo la mradi ni kuzijengea uwezo jamii zinazoishi karibu na rasilimali misitu na wanyamapori, iliwaweze kuzisimamia na kunufaika nazo.
Mradi unatoa mafunzo ya sheria, sera, miongozo, kanuni na Ufuatiliaji uwajibikaji jamii kwa kamati za vijiji za maliasili na mazingira, uchumi, maji na matumizi ya ardhi.
Pia mradi umetoa mafunzo kwa wananchi, madiwani na asasi za kiraia. Takriban wananchi 6500 watafikiwa na mafunzo hayo.
Katika kutimiza azma ya kutoa elimu ya usimimizi wa maliasili kwa wananchi wengi, LEAT inatoa mafunzo kwa njia ya redio, sambamba na kutoa elimu kwa njia ya sanaa kupitia kikundi cha Sanaa Mashujaa kwa wilaya ya Iringa na kikundi cha Sanaa Mapogoro kwa wilaya ya Mufindi.
No comments:
Post a Comment