Friday, 30 September 2011

WAHASIBU KORTINI KWA WIZI WA MILIONI 79.8 MAKETE


Makete
WATUMISHI wanne wa Halmashauri ya wilaya ya Makete kitengo cha fedha wamefikishwa mahakamani kwa makosa 233 yakiwemo wizi wa fedha zaidi ya 79.8m/- mali ya umma.
Watumishi hao ni pamoja na Bw. Golden Asheri Sanga Mkuu wa Kitengo cha Uhasibu katika Halmashauri hiyo na mke wake aitwaye Bi. Naheri Paten Chengula ambaye ni mwalimu katika Shule ya Msingi Makete.
Wengine waliofikishwa mahakamani hapo ni pamoja na Sued Abdul Milanzi na Ernest Mwangomela wote wahasibu wasaidizi katika halmashauri hiyo ya Makete.
Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo mheshimiwa Chanjalika mwendesha mashtaka mrakibu msaidizi wa polisi ambaye ni mkuu wa upelelezi wilaya ya Makete ASP Komba aliiambia mahakama kuwa washtakiwa wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 233 ikiwemo wizi.
Bw Komba aliyataja makosa mengine kuwa ni pamoja na wizi wakiwa watumishi, kula njama za kuiibia serikali na kuingiza hesabu za uongo katika vitabu vya serikali huku wakijua kuwa kufanya hivyo ni kosa la janai na kwamba wamekuwa wakitenda makosa hayo kwa kipindi cha miaka minne hadi walipogundulika na Benki ya NMB Tawi la Makete mwezi Juni mwaka huu.
Hata hivyo washtakiwa wote walikana kuhusika na makosa hayo na kumwomba kuwapa dhamana ambapo upande wa mashtaka haukuwa na pingamizi kwa sababu dhamana ni haki yao ingawa mwendesha mashtaka alimtaka Hakimu kuzingatia kifungu 148 (4) cha mwenendo wa mashtaka sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2000.
Akisoma kifungu hicho Bw Komba alisema kuwa wizi wowote unaozidi kiwango cha shilingi 10m/- mdhamini anatakiwa kutoa fedha taslimu inayolingana au nusu yake, lakini wadhamini na washtakiwa walishindwa kutimiza masharti hayo.
Akifafanua na kutafsiri kifungu hicho Hakimu Chanjalika alikubaliana na mwendesha mashtaka lakini akasema dhmana ni haki ya mshtakiwa hata hivyo mahakama imepewa uwezo na mamlaka ya kuamua na kuona inavyofaa kama wadhamini na washtakiwa watakosa kutimiza sharti hilo.
Kutokana na uwezo huo kisheria, mahakama katika wilaya ya Makete, iliamuru kila mshtakiwa kuleta wadhamini wawili wenye hati ya mali isiyohamishika lakini yenye thamani ya shilingi 20m/- kila mmoja.
                         



No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...