Wednesday, 6 May 2015

MIPANGO NA SERA ZITEKELEZWE KUMUOKOA MAMA NA MTOTO MCHANGA



Mratibu wa Mawasiliano na uhamisishaji wa mradi wa Mama Ye unaoendeshwa na asasi ya Evidence for Action linalofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID), Chiku Lweno akielezea jitihada zinazofanywa na mradi wa Mama Ye katika kukabiliana na vifo vya Mama na mtoto ambapo aliwataka waandishi wa habari kutumia kalamu zao kuelemisha jamii ili iweze kuepukana na vifo vya mama na mtoto ambalo nalo ni janga la taifa.(Picha zote na Zainul Mzige wa modewjiblog).

Na Mwandishi wetu, Musoma

SERIKALI imeshauriwa kuhakikisha sera na mipango mizuri iliyopo kwa afya ya mama na mtoto mchanga inasimamiwa na kutekelezwa ili kuliondoa taifa katika janga la kupoteza mama na watoto wakati wa uzazi.

Kauli hiyo imetolewa na Mratibu wa Mawasiliano na uhamisishaji wa mradi wa Mama ye unaoendeshwa na asasi ya Evidence for Action linalofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID), Chiku Lweno katika mafunzo kwa waandishi wa habari mjini Musoma.

Alisema bila kutekeleza mipango mizuri ambayo Rais Jakaya Kikwete amekuwa championi wa masuala ya wanawake na watoto kitaifa na mataifa, tatizo la vifo kwa wanawake wenye pingamizi za uzazi na watoto wachanga.

Alisema kutokana na haja ya kutoa msukumo katika masuala ya uzazi wameamua kuwapatia elimu waandishi wa habari ili wawe chachu ya kutambua umuhimu wa ukunga na uzazi salama.

"Tunafunza waandishi wa habari ili waweze kusukuma mbele shahuri hili ili kila mtu katika nafasi yake atetee nafasi yake" alisema Lweno.

Alisema suala la mama na mtoto mchanga ni masuala mtambuka ambapo mambo mengi lazima yaunganishwe yafikiriwe na kutambuliwa ili kudhibiti vifo vya wanawake na watoto wachanga.

Alitaja masuala hayo kama upangaji wa bajeti ya kueleweka kwa ajili ya kusaidia kupatikana kwa wakunga wataalamu na vifaa vyao vya kazi na maeneo ya kufanyia kazi. Aidha kuwapo kwa ukubali wa wakunga na elimu ya uzazi.

Alisema ni vyema waandishi wa habari kama watia chachu kuelimishwa mambo mengi yanayohusiana na uzazi salama ambapo ndani yake kuna masuala ya bajeti na ufuaji wa wataalamu na ufuatuiliaji wa sera na sheria zilizopo katika kuhakikisha usalama wa mama na mtoto.

Alisema anaamini waandishi wa habari wakielewa mambo hayo watasaidia kukomaa nalo na kuwezesha kila mtu kuwajibika.


Kaimu Muuguzi Mkuu wa Serikali kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Ama Kasangala akifafanua jambo kwa washiriki wa mafunzo ya siku moja yaliyofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu (UNFPA) kuelekea kwenye kilele cha sherehe za maadhimisho ya siku ya wakunga duniani ambapo kitaifa imefanyika mkoani Mara.

Naye Afisa Muuguzi mwandamizi kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii, Saturini Manangwa akiwasilisha mada kwa waandishi wa habari alisisitiza haja za waandishi kutambua dhana ya afya ya mama na mtoto kuwa ni kitu mtambuka kutokana na suala la lenyewe kutegemeana.

Alisema serikali inapohimizwa kuwekeza kwa mkunga kunatokana na ukweli kuwa huduma ya mama na mtoto mchanga itakujwa bora kwa kuwa na mkunga bora mwenye vifaa na anayefahamu wajibu wake kuanzia ujauzito wa mama hadi kujifungua kwake.

Alisema uwekezaji huo unagusia changamoto nyingi zilizopo sasa kama upungufu wa wakunga, vituo vya kutolea huduma, dawa, miundombinu na masuala anuai ambayo yameegemezwa na utambuzi wa bajeti na umuhimu wake kama kipaumbele.

Alisema kwamba katika upangaji bajeti kila kitu kinategemea huwezi kusema unazidisha hiki na unakiacha hiki.

Alisema mathalani katika hali bora ya ukunga na uwezo wa kumsaidia mhusika ,viwango vya dunia vilivyoweka na Shirika la Afya Duniani (WHO) kila mkunga mmoja ahudumie angalau watu sita, lakini sehemu kubwa ya dunia haifikii hivyo.

Aidha alisema kwa Tanzania kiwango ni mkunga mmoja ahudumie watu 20-25 lakini kwa sasa Tanzania mkunga mmoja anahudumia zaidi ya watu 50.

Kimsingi alisema Tanzania ina tatizo la wakunga na pamoja na serikali kuanzisha vyuo vya kufunza wakunga na kukubali mashirika ya dini nayo kufanya hivyo hali bado ni tete.

Hata hivyo alisema ni kupitia wakunga waliowataalamu upo uwezekano wa kuzuia vifo visivyo vya lazima.


Mratibu wa Chama cha Wakunga nchini (TAMA), Martha Rimoy akizungumzia nia ya chama hicho ni kuhakikisha kwamba kila mwanamke mwenye uwezo wa kuzaa anapata huduma za mkunga mtaalamu.

Muuguzi huyo mwandamizi pia alisema katika juhudi za serikali kunaanzishwa mafunzo ya mwaka mmoja ambapo yatatoa maofisa afya ambao kazi yao kubwa itakuwa kujua idadi ya wanawake wajawazito na wagonjwa katika maeneo yao na kutoa taarifa kwa zahanati iliyo karibu.

Alisema ofisa huyo kazi yake haitakuwa hospitalini au kwenye zahanati bali kwenye jamii akitambua idadi ya wagonjwa wake na kutoa taarifa sahihi ya hali ya afya ya kitongoji chake kwenye zahanati.

Mmoja wa washiriki Belina Nyakeke ambaye ni mwandishi wa habari wa magazeti alisema kwamba amefurahishwa na mafunzo hayo ambayo yamempa nafasi ya kutambua wajibu wake katika kusaidia kuondoa tatizo la vifo vya mama na mtoto mchanga.

Alisema japokuwa mafunzo ni ya muda mfupi lakini yamemfumbua macho kutambua wajibu na haki kwa wananchi na serikali.

Naye Ahmed Makongo akizungumzia mafunzo hayo alisema yamemfanya atambue wajibu wake kusaidia kusukuma mambo yaende sawa kwa upande wa waamuzi na pia wananchi husika kwa kuzingatia mafunzo hayo yaliyoletwa kwao na Mama Ye na UTTPC chini ya Ufadhili wa Shirika la Mpango wa watu Duniani (UNFPA)


Afisa muuguzi mwandamizi kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Saturini Manangwa akizungumzia changamoto za upungufu wa wakunga, vituo vya kutolea huduma, dawa, miundombinu n.k wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari wa mjini Musoma mkoani Mara.


Afisa wa Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu (UNFPA) anayeshugulikia mifumo ya Afya, Felista Bwana akitoa takwimu za nchi zinazoongoza kwa vifo vya mama na mtoto kwenye mafunzo ya waandishi wa habari mjini Musoma. 


Mwandishi wa habari wa gazeti la The Citizen, mkoani Mara, Belina Nyakeke (katikati) akishiriki kwenye mafunzo ya waandishi wa habari yaliyofanyika mjini Musoma na kufadhiliwa na Shirika la UNFPA.


Mwandishi wa habari wa gazeti la Tanzania Daima mjini Musoma, Igenga Mtatiro akiuliza swali kwa Afisa muuguzi mwandamizi kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Saturini Manangwa (hayupo pichani).


Pichani juu na chini ni baadhi ya waandishi wa habari wa mkoani Mara ambao pia wanachama wa vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) walioshiriki mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Mradi wa Mama Ye kwa kushirikiana na UTPC na kufadhiliwa na UNFPA.







Rais wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Kenneth Simbaya akisisitiza jambo kwa washiriki wa mafunzo hayo.


Rais wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Kenneth Simbaya (kushoto) akibadilishana mawazo na Mratibu wa Chama cha Wakunga nchini (TAMA), Martha Rimoy mara baada ya kuhitimisha mafunzo hayo.

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...