Thursday, 7 May 2015

VIGOGO WANNE WANAODAIWA KUFUKUZWA KAZI WA TALGWU KILOLO YAWATETEA

Mwenyekiti wa TALGWU Kilolo, Andrea Mwandimbile

CHAMA cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU), wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa kimepinga uamuzi wa halmashauri ya wilaya hiyo, wa kuwafuta kazi vigogo wake wanne.

Taarifa iliyotolewa juzi na Mwenyekiti wa TALGWU wa wilaya hiyo, Andrea Mwandimbile kwenye mkutano mkuu wa chama hicho, inaonesha vigogo hao wamefukuzwa kazi hivikaribuni baada ya kusimamishwa kazi Oktoba mwaka jana.

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo, Rukia Muwango hakuweza kupatikana kuzungumzia sababu za watumishi hao “vigogo” kufutwa kazi kama ilivyodaiwa na chama hicho.

Vigogo hao wametajwa katika kikao hicho kuwa ni pamoja na mweka hazina wa halmashauri hiyo Eriekel Mbise, mwanasheria wa halmashauri Alto Lixolelo, afisa misitu wa halmashauri Godfrey Mwita na afisa ununuzi wa halmashauri Alex Mkuba.

Novemba mwaka jana, mkurugenzi wa halmashauri hiyo, alitoa kwa wanahabari taarifa iliyohusu kusimamishwa kazi kwa vigogo hao kwa kile alichosema ni kwa ajili ya kupisha uchunguzi wa tuhuma zilizoelekezwa dhidi yao.

Wakati akitoa taarifa hiyo, Muwango alisema watumishi hao wanahusishwa katika mikataba tata iliyoisababishia halmashauri hiyo hasara na akakataa kutoa ufafanuzi wa hasara hiyo akidai kwamba ingekuwa ni “sawa na kuingilia suala linaloendelea kufanyiwa kazi.”

Aliitaja mikataba hiyo kuwa ni ile inayohusiana na uvunaji wa miti katika msitu wa halmashauri hiyo na wa kampuni ya New Forest inayozalisha nguzo katika eneo la Viwengi wilayani humo.

“Siwezi kufafanua nini kipo katika mikataba hiyo na hawa watumishi wanatuhumiwaje katika mikataba hiyo. Kwa kuwa wanatakiwa kujieleza au kujitetea, tunasubiri wafanye hivyo ili haki iweze kutendeka” alisema.

Katika mkutano huo, mwenyekiti wa Talgwu alisema; “kuna kila dalili kwamba watumishi wenzetu hao wamefukuzwa kazi katika mazingira yanayoashiria kutofuatwa kwa kanuni, taratibu na maadili ya utumishi wa umma.” alisema.

Aliwauliza wajumbe zaidi ya 80 waliohudhuria mkutano huo kama wanakubaliana na maamuzi ya halmashauri hiyo ya kuwafukuza kazi watumishi hao na kwa pamoja walijibu “hatukubaliani” huku wakipiga meza.

Mkanda mzima wa kilichojiri katika mkutano huo kukujia kupitia mtandao huu hivi punde... 

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...