Na Friday Simbaya, Songea
Asumpta Magunga mwenye miaka kumi na saba (17) wa Kijiji cha
Peramiho, Wilaya ya Songea (V) mkoani Ruvuma amezaa mtoto
asiyekuwa na ngozi tumboni, yaani amezaliwa na viungo vyote vya ndani vinaonekana
wazi kwa kitaalamu wanaita (congenital
malfunction) katika Hospitali ya Mtakatifu Joseph Peramiho.
Magunga ambaye alikuwa ni
mwanafunzi wa Kidato cha Pili Shule ya Sekondari Namihoro, willayani Songea Vijijini
mkoani Ruvuma ni mkazi wa mtaa wa Lihangano katika kijiji cha Peramiho alijifungua
mtoto bila ngozi ya tumboni, lakini bahati mbaya mtoto huyo hakuishi muda mrefu
alifariki dunia Jumapili tarehe 24 Novemba mwaka huu.
Nilipopata taarifa
kuhusu kuzaliwa kwa mtoto wa ajabu mwenye kuzaliwa na viungo vya ndani vikiwa
nje nilichukuwa kamera ya ofisini na kukimbia mara moja hospitalini kupata
picha na maelezo kidogo kuhusiana na tukio lenyewe.
Nilipofika pale
hospitali nilikwenda moja kwa moja kwenye ofisi ya Muuguzi Mkuu, Romanus Mgimba
ambaye naye akanielekeza niende wodi ya kinamama Chumba Namba Tatu (3), ambapo alilazwa
mama huyo ndipo nikakutana na Muuguzi Mkunga, Odila Kapinga na aliyenionesha mtoto
wa ajabu wa jinsia ya kike aliyezaliwa
na utumbo nje.
Nilitaka kupata maelezo
ya kitaalam kuhusiana na tatizo hilo, lakini juhudi za kumuona daktari ili kuelezea
tukio lenyewe ziligonga mwamba baada ya kuambiwa nisubiri mpaka hapo watakapokuwa
na taarifa kamili.
Hata hivyo tatizo la
mimba za utotoni hapa Peramiho linaendelea kukua siku hadi siku kama ambavyo
wadau mbalimbali wanaelezea kwamba kila
kona upitapo utaona mabinti wenye umri chini ya miaka 19 wakiwa wamebeba
watoto migongoni, ambapo chanzo chake kikielezwa kuwa ni umasikini pamoja na mmomonyoko
wa maadili katika familia nyingi.
Katekista George
Millinga ni katekista wa Parokia ya Peramiho ambaye pia ni mwalimu wa dini anayefundisha
soma la dini katika shule za sekondari na taasisi mbalimbali za hapa Parokia ya
Peramiho, Jimbo Kuu la Songea.
Amesema kuwa tatizo la
mimba za utotoni Peramiho linaongezeka siku hadi siku, ambapo alielezea chanzo
kikubwa ni umasikini na mmomonyoko wa maadili kwa familia nyingi za hapa
Peramiho.
Amesema watu wengi hapa Peramiho hawapendi kujishughulisha na
kazi kwa kutegemea misaada mbalimbali kutoka mahali fulani na matokeo yake watu
wanatumia kutatua umasikini kwa njia isio halali.
Vijana wengi wamekuwa
mbali na Mungu kwa kutoshika maadili ya kidini na kupenda kuanza mapenzi katika
umri mdogo badala ya kusubiri hadi hapo watakapofunga ndoa wakishakomaa, na zinaa
au uasherati kidini ni dhambi.
“Tatizo kubwa ninavyojua mimi watu wengi wanatumia
uasherati kwa kutatua matatizo yao ya umasikini, hawapendi kujituma kazi wanapenda
zaidi kupata fedha kwa njia isio halali kwa kutegemea misaada kutoka sehemu na
mapato yake ni hizo mimba za utotoni…”
amesema Kat. Millinga.
Amesema kitu kingine
kinachochangia tatizo la mimba za utotoni ni wazazi wenyewe kwa sababu
hawawafundishi watoto wao maadili mema na kuwa watoto wakirandaranda mitaani
bila msaada wowote.
Kat. Miliinga ameshauri Serikali
itoe adhabu kali kwa mtu yeyote anayempa
mimba mtoto mdogo na mwanafunzi kwa sababu huko ni kuharibu taifa la baadaye na mtu
kama huyo anastahili apewe adhabu sawa
na mauaji.
“Mtu anayempa mimba msichana
mwenye umri mdogo afananishwe na mtu mwenye kosa la mauaji kwa sababu anaharibu taifa la baadaye, anaharibu
afya ya mtoto vile viungo vya uzazi havijakomaa sawa sawa,” amesema Kat.
Millinga.
Ameshauri walimu na wazazi wasichoke kukemea maovu kwa wanafunzi
na kuwapa maadili mema na wazazi ili kupunguza tatizo la mimba za utotoni.
Ongezeko kubwa la mimba za utotoni Tanzania
Shirika
la Umoja wa Mataifa linalohusika na idadi ya watu UNFPA limezindua ripoti yake
na kuitaja Tanzania kama moja ya nchi ambazo zinakabiliwa na ongezeko kubwa la
mimba za utotoni na hivyo kuwafanya wasichana wengi kukatiza masomo yao.
Ripoti hiyo iliyozinduliwa hivi karibuni
imeangazia hali ya idadi ya watu na kusema kuwa kati ya mimba milioni moja
zinazotungwa nchini Tanzania, asilimia 23 ya mimba hizo zinawahusu wasichana
walio chini ya umri wa miaka 19.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, idadi ya watoto wa
kike wanaopata mimba bado ni kubwa na kwamba takwimu za sasa zinaonyesha kuwa
kila kwenye wasichana 10, 4 kati yao wamepata mimba.
Baadhi ya mambo yaliyotajwa kusababisha hali
hiyo ni pamoja na kuwepo kwa mila potofu ambazo zinawakandamiza na kuwabagua
watoto wa kike. Jambo jingine lililoelezwa na ripoti hiyo ni kuendelea
kuongezeka kwa ndoa za utotoni ambazo hutumika kama kigezo cha kujipatia mali
kwa baadhi ya wazazi.
Alanna Armitage Mkurugenzi wa UNFPA mjini
Geneva amesema mimba za utotoni huathiri afya, elimu na haki za mtoto wa kike.
Ameongeza kuwa mtoto wa kike asiye na elimu atakuwa na ugumu kupata ajira na
kujijengea maisha bora na familia yake.
Caption
Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Namihoro
wilayani Songea vijijini, mkoani Ruvuma, Asumpta Magungu (17) mkazi wa Kijiji
cha Peramiho akimuangulia mtoto wake huruma katika wodi ya kinamam Chumba Namba
Tatu (3) Hospitali ya Mtakatifu Joseph Peramiho hivi karibuni. Picha ndogo ni
sehemu ya mtoto huyu aliezaliwa bila ngozi ya tumboni. (Picha na Friday
Simbaya)
No comments:
Post a Comment