ZAIDI YA VIONGOZI 53 wa dini mbalimbali wanawake
kwa wanaume kutoka katika maeneo mbalimbali wilayani Ludewa, Mkoa Iringa wamehudhuria
mafunzo ya siku tatu kuhusu Afya ya uzazi na mtoto.
Shirika lisilokuwa la kiserikali la IMA WORLD
HEATH la jijini Dar es Salaam limetoa mafunzo hayo maalum kupitia mradi wa
Maisha Program uliofadhiliwa na shirika la maendeleo la kimataifa la watu wa
marekani USAID.
Awali akitoa taarifa kwa mgeni rasmi Mratibu wa
mradi huo Bw Joel Lubebe alieleza kuwa
sababu ya kuwapa elimu hii viongozi wa dini mbalimbali ni kutokana na viongozi
hao kuaminiwa na jamii, pia jamii kuwa tayari kupokea maagizo na mafundisho yao
sanjari na ushawishi na vipawa walivyopewa na Mungu mwenyewe.
Bw Lubebe alisema mradi wa Maisha Program unalenga
kupunguza vifo vya uzazi vinavyotokana na sababu za moja kwa moja kama kutokwa
damu kupita kiasi kwa wajawazito baada ya kujifungua pia kupunguza vifo vya
watoto wachanga na kupunguza kiwango cha watoto waliozaliwa na uzito pungufu
kwa kuhakikisha akina mama wanatibiwa Malaria mapema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya
Ludewa Bi Hilda Lauo katika hotuba yake kwa washiriki wa mafunzo hayo alisema
Tanzania imeandaa mpango mkakati wa kitaifa wa kuongeza kasi ya kupunguza vifo
vya uzazi na mtoto kufikia robo tatu ¾ na 2/3 kwa vifo vya watoto ifikapo 2015.
Bi Lauo aliongeza kuwa mkakati huu unatoa fursa
kwa wadau wote katika miradi yote kusisitiza katika maeneo mawili, utoaji wa
huduma katika vituo, na huduma ya Afya ya jamii ili kufikia malengo ya mpango
wa Taifa wa kupunguza umaskini na kuongeza uchumi Tanzania (MKUKUTA) na mpango
wa Maendeleo wa Afya ya Msingi( MAAM).
Kwa upande wake Bi Velonica Mkusa mwezeshaji
kutoka Ima World Heath alisema mradi umelenga kuwafundisha viongozi wa dini ili
watumie miongozo yao kuhusu afya ya uzazi na mtoto katika kushirikiana na
Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii.
Mkusa alisema tatizo la vifo vitokanavyo na uzazi kwa
akina mama na watoto ni kubwa kwani kati ya akina mama 100,000 watakaojifungua
watoto hai 454 wanafariki dunia sababu ya uzazi na kuongeza kuwa kuna umuhimu
kwa akina mama kuwahi cliniki mapema anapohisi ujauzito kwani husaidia kupata msaada
mapema.
Naye Mratibu wa hudum za Afya ya uzazi na mtoto
wilayani Ludewa Bi Imelda Mtemi (Mama Mnyagala) akitoa takwimu ya Wilaya yake
alisema mwaka 2008 akina mama 139 walifariki dunia kutokana na vizazi hai
100,000 ambapo mwaka 2009 akina mama 85 walifariki na 2010 akina mama 108 walifariki dunia kutokana
na vizazi hai 100,000.
Bi Mnyagala Mtemi aliongeza kuwa vifo vya watoto
chini ya mwaka mmoja (IMR) mwaka 2008 vifo 26 vilitokea ambapo mwaka 2009
ilikuwa 25/1000 na mwaka 2010 vifo 25 kwa 1000 vilitokea.
Aliongeza kuwa akina mama waliojifungua katika
vituo vya kutolea huduma za afya kwa mwaka 2008 ilikuwa asilimia 67 ambapo 2009
ilifikia asilimia 68 na mwaka 2010 ilifikia asilimia 69 na akina mama
wanaojiunga na cliniki kabla ya miezi minne ya ujuzito mwaka 2008 ilifikia
asilimia 68 ambapo mwaka 2009 ilishuka na kufikia asilimia 58 na mwaka jana
ilifikia asilimia 59.
Hata hivyo, Mtemi alisema anakabiliwa na
changamoto kadhaa ikiwemo uelewa mdogo wa jamii katika kufanya maamuzi ya
haraka juu ya kuwawahisha hospitali akina mama wenye matatizo ya uzazi, uelewa mdogo
juu ya akujiunga na cliniki kabla ya miezi minne, juu ya lishe kwa wajawazito
na muda wa kupumzika sanjari na kutumia dawa za Malaria kwa mjamzito
Akifunga mafunzo hayo Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ludewa
Dr. Happenes Ndosi aliwashukuru wawezeshaji kutoka shirika la Ima World Heath
kwa mafunzo hayo na kuwataka washiriki hao viongozi wa dini mbalimbali kufikisha
elimu waliyoipata kwa waumini wao ili kupunguza vifo vya uzazi na mtoto
wilayani mwake.
No comments:
Post a Comment