KILOLO: WANANCHI wa kijiji cha Mawala, kata ya Irole katika Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa wameitaka serikali wilayani humo kuharakisha upimaji wa maeneo ya ardhi ya kijiji chao pamoja kupatiwa cheti cha ardhi ya kijiji ili kupunguza migororo mbalimbali iliyopo kwa sasa.
Wakizungumuza jana katika mdahalo walisema serikali kwa kutumia sheria ya ardhi ya vijiji itenge maeneo kwa ajili ya wakulima na wafugaji hatua itakayosaidia makundi hayo kuepukana na migogoro kwa kuwa makundi yote mawili yanategemeana.
Mdahalo huo uliozungumzia namna ya kuondoa migogoro ya ardhi ya kijiji uliandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Tanzania Grassroots
Oriented Development (TAGRODE) yenye makao yake makuu mjini Iringa kwa shirikiana na PELUM Tanzania.
Wakichangia mada, wakazi hao wa Kijiji cha Mawala walisema migogoro ya ardhi katika maeneo yao itakoma kama serikali itasimamia kwa nguvu zake zote utekelezaji wa sheria za ardhi hatua ambayo pia itaimarisha amani na utulivu na kuleta tija kwa jamii.
kijiji cha Mawala kina vitongoji viwili ambavyo Mawala ‘A’ na ‘B’ hakina cheti cha ardhi ya ardhi ya kijiji hivyo wameiomba serikali iwapatie cheti hicho ilikuweza kuondoa migogoro ya mipaka baina vijiji inavyopakana navyo.
Naye mratibu wa Shirika la TAGRODE, Dickson Mwalubandu alisema shirika hilo linaendesha midahalo hiyo katika vijiji vya Ikuka, Mbigili, Mawala, Mawambala na Masalali kwa wilaya ya kilolo na vijiji vya Usokami, Ugesa, Makungu, Magunguli na Isaula wilaya ya Mufindi kupitia mradi wake wa CEGO unaohusisha jamii ya vijijini katika uwajibikaji wa masuala ya ardhi ya kijiji.
Alisema kuwa kwa ufadhili wa shirika la Kimataifa la Maendeleo la Marekani (USAID) kupitia shirika la PELUM Tanzania wanaendesha midahalo katika wilaya mbili za Mufindi na Kilolo mkoani Iringa.
Kwa upande wake Afisa Mradi kutoka mtandao wa Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali yanayofanya kazi na wakulima na wafugaji wadogo nchini Tanzania (PELUM Tanzania) Angolile Rayson alisema, asilimia kubwa ya migogoro yote ya ardhi wilayani Kilolo mkoani Iringa, inatokana na ugomvi wa mipaka katika maeneo ya vijijini.
Rayson alisema kuwa midahalo inayofanywa katika wilaya hizo inalenga kutafuta mambo yakufanya ili kupunguza malalamiko ya migogoro ya ardhi.
Alisema kuwa Kwa ufadhili wa shirika la Kimataifa la Maendeleo la Marekani (USAID), mtandao huo ulitoa mafunzo ya haki za ardhi na utawala katika vijiji vyote vya mradi.
Alisema kuwa ili kuhakikisha wananchi wanakabiliana na changamoto hiyo shirika lake lilitoa elimu, na kuimarisha kamati za ardhi za vijiji na mabaraza ya ardhi ya vijiji ili yaweze kutatua migogoro pindi inapojitokeza kwenye maeneo yao.
Rayson alisema mafunzo hayo ya haki za ardhi na utawala yanalenga kuwaongezea wananchi wa wilaya hizo uelewa juu ya sheria za ardhi, haki za ardhi kwa wanawake na makundi maalum pamoja na utatuzi wa migogoro ya ardhi.
Afisa Mradi wa PELUM Tanzania huyo alisema shirika lake limeamua kufanya kazi hiyo kwa lengo la kusaidia kukuza uelewa wa wananchi juu ya ya haki zao kwa masuala yahusuyo ardhi na mbinu za kukabiliana nayo ili kupunguza tatizo hilo nchini.
Alisema kwa sasa mradi huo unatekelezwa katika vijiji 30 vilivyopo katika wilaya sita za mikoa mitatu ya Tanzania bara ambayo ni Morogoro, Dodoma na Iringa.
Hata hivyo, Afisa Mipango Miji na Vijiji Wilaya ya Kilolo, Bernard Kajembe alisema kuwa halmashauri ya wilaya kilolo ina vijiji 30 vilivyo na mpango wa matumizi bora ya ardhi kati ya vijiji 95 vya wilaya hiyo.
Alisema kuwa kwa shirikiana na shirika la Pelum Tanzania halmashauri hiyo wanaanda mpango wakuongoza vijiji vingine kupelekewa mpango huo wa matumizi bora ya ardhi ili kupunguza migogoro ya ardhi wilayani humo.
No comments:
Post a Comment