Sunday, 16 March 2014

MAMIA YA WAKAZI WA PERAMIHO WAMZIKA BABA MZAZI WA RAIS WA VICOBA TANZANIA



Na Friday Simbaya, Songea
Paroko Msaidizi wa Parokia ya Peramiho katika Jimbo Kuu la Songea, Padre Benedict OSB ametoa rai kwa wazazi wa Peramiho na kwingineko kuwaelekeza watoto katika masomo kwa sababu elimu ni mwanga wa maisha.
Alisema kuwa wazazi na walezi wanapaswa kuwasomesha watoto wao ili kuwaandalia maisha mazuri kwa baadaye yenye faraja.
Paroko huyu aliyasema haya jana wakati wa Ibada ya Misa Takatifu ya mazishi ya marehemu Barnabas Jacob Mkuwa (91), ambaye alikuwa baba mzazi wa Mbunge wa Viti Maalum, Rais wa Vicoba Tanzania na Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Devote Mkuwa Likokola.
Misa hiyo iliyofanyika nyumbani kwa marehemu Mtaa wa Madukani, Peramiho wilayani Songea, mkoani Ruvuma iliongozwa na mapadre saba, akiwemo Padre Lucius OSB aliyeongoza madhehebu yote ya Misa.
Alisema kuwa kuna baadhi ya wazazi wanakwepa majukumu ya kuwalea watoto wao katika maadili mema ikiwa pamoja na kuwapatia elimu, afya, mavazi na malezi. “Watoto ni zawadi kwenu, simameni imara katika malezi ili baadaye wawe faraja kwenu,”aliongeza paroko huyo.
‘Wazazi na walezi popote duniani wanatambua kuwa hakuna jukumu zito kama la kulea watoto. Ni kazi ngumu ambayo haina likizo. Wazazi makini huwalea watoto wao kwa kuwapatia elimu, afya, mavazi na malezi,’alisema paroko huyo.
Alitoa mfano wa marehemu Barnabas Jacobo Mkuwa walifanya kazi  vizuri ya malezi kwa kuwasomesha watoto wake wote, ndiyo maana aliishi maisha marefu yenye faraja kwa sababu ya kuwapatia elimu watoto wake.
Aliongeza kuwa wazazi wa jana, leo na kesho wakumbuke kuwa kazi ya malezi ni jukumu la uhai wote, hivyo basi wazazi wakumbuke kuwa samaki mkunje angali mbichi, kwa sababu jinsi watakavyo walea watoto wangali wadogo ndivyo watakavyofarijika zaidi baadaye na kuyaona matunda mema ya watoto wao.
Kwa upande wake Fr. Lucius OSB ambaye pia Priori Mstaafu wa Abasia ya Peramiho kwa niaba ya jamii ya Abasia ya Peramiho alitoa shukurani  kwa ukoo wa familia ya Mkuwa kwa kutoa mchango mkubwa kwa  kuendeleza umissionari  hapa Peramiho tangu kuanzishwa kwake miaka 114.
Alisema kuwa ukoo wa Mkuwa ulikuwa bega kwa bega kwa kuhakikisha maendeleo ya Abasia ya Peramiho kwa hakikisha kuwa umisionari hapa Peramiho unakuwa na kusimama imara.
Wakati huohuo, wabunge wa Mkoa wa Ruvuma kwa kupitia mwenyekiti wa wabunge wa Mkoa wa Ruvuma, Jenister Mhagama wametoa rambirambi ya shilingi laki tisa (900,000/-) kwa mbunge mwenzao, Devote Likokola kwa kufiwa na baba yake mzazi.
Marehemu Barnabas Mkuwa alizaliwa tarehe 23.04.1923 hapa Peramiho, ameacha watoto saba wote wakike, wajukuu 36 na vitukuu 31. Alifariki dunia tarehe 13.03. 2014 katika Hospitali ya Mtakatifu Joseph Peramiho kwa ugonjwa shinikizo la damu na kuzikwa katika makaburi ya Namihoro Peramiho.
Marehemu Barnabas alibatizwa tarehe 27.04.1923, alipata Kumunio ya Kwanza tarehe 25.06.1931. Kipaimara tarehe 28.05.1934 na alifunga ndoa na Isabella Mukaranga ambaye pia ni marehemu mnamo tarehe 10.06.1943 katika Kanisa la Peramiho.
Alianza kazi ya ualimu mwaka 1942 na kustaafu  mwaka 1978 ambapo wakati wa uhai wake alifundisha shule mbalimabli za msingi zikiwemo Likuyufusi, Ndilima, Namabengo, Lilambo, Parangu, Mtyangimbole, Tukuyu, Liganga, Lipaya na Peramiho zote za Mkoa wa Ruvuma.
Mwisho











No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...