Tuesday, 28 January 2014

HALMASHAURI YA WILAYA YA SONGEA INA JUMLA YA WANAFUNZI 3770 WASIOJUA KUSOMA, KUANDIKA NA KUHESABU



Na Friday Simbaya, Songea

Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Mkoa wa Ruvuma katika Idara ya Elimu ya Msingi  ina jumla ya wanafunzi 3770 wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu (K.K.K.), imefahamika.

Hayo yalibainika wakati  wa mkutano wa kutathmini elimu na matokeo ya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi na daras la nne mwaka 2013 uliofanyika hapa Peramiho hivi karibuni .
Akisoma taarifa yake ya utekelezaji kwa wadau wa elimu mbalimbali waliohudhuria kikao hicho cha siku moja, Afisa Elimu Taaluma, Wilaya ya Songea, Vincent Chimoto alisema kuwa wapo wanafunzi wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu katika shule za msingi mwaka 2013 wapatao 3770 darasa la I-VII.

Afisa huyo wa elimu taaluma pia aliwaagiza walimu kuchukuwa jitihada za makusudi kwa kutenga muda wa ziada na kuwa na ratiba ya kuwafundisha wanafunzi hao ili wajue stadi za K.K.K.
Aidha, alisema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Songea inazo jumla ya shule za msingi 96, kati ya hizo shule zenye darasa la saba ni 89.
“ Wilaya ina jumla ya wanafunzi wapatao 32,592 kati ya hao wavulana ni 16,010 na wasichana 16,582,” alifafanua.
Alisema wilaya ina jumla ya walimu 721, mahitaji ni 911 hivyo upungufu ni walimu 190.
“Katika mgao wa walimu wapya mwaka 2013 tulipata walimu 96, lakini walioripoti ni 87 na ambao walisafirishwa hadi katika vituo vyao vya kazi,” aliongeza.

Awali akifungua kikao hicho cha wadau wa elimu, Mkuu wa Wilaya ya Songea, Joseph Mkilikiti aliwataka wadau  kuchukua hatua za makusudi  kwa kuweka nguvu ya pamoja kuinua sekta ya elimu wilayani hususani elimu ya msingi.
Alisema kuwa elimu ya msingi ndio kila kitu ni kama msingi wa nyumba. Msingi wa nyumba unapokosewa hakika nyumba hiyo haiwezi kuwa imara tena.

MATOKEO YA MTIHANI

Mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi ulifanyika nchini kote kuanzia tarehe 10-11/9/2013. Wilaya ilikuwa na jumla ya shule za msingi zipatazo 89 zenye wahitimu wapatao 3738 kati yao wavulana ni 1680 na wasichana ni 2058 waliosajiliwa kufanya mtihani.
Matokeo ya mtihani yanaonesha kuwa wilaya ina wastani wa ufaulu wa asilimia 42.5 ukilinganisha na ule wa mwaka 2012 ambao ni asilimia 30. Katika matokeo ya kimkoa, wilaya ni ya pili kwa kupata wastani wa ufaulu asiliamia 42.5.

CHANGAMOTO ZINAZOKABILI UTOAJI TAALUMA

Upungufu wa walimu unaotokana na walimu wengi kustaafu na wengine kufariki dunia, mfano wastaafu 2010/2011 walimu 28, 2011/2012 walimu 26, 2013/2014 walimu 37. Jumla yao ni 91 na waliofariki dunia ni walimu 13.
Utoaji chakula kwa wanafunzi bado ni tatizo, msisitizo unahitajika wa pamoja ili kufikia malengo ya shule zote kutoa chakula. Mwaka 2013 shule 48 kati ya 96 zinatoa chakula.

Utoro wa rejareja wa walimu na wanafunzi huchangia kushusha taaluma. Kwa upande wa walimu mada katika masomo hazimaliziki na kwa upande wa wanafuzi kukosa baadhi ya mada.
Baadhi ya walimu kutokuwa na moyo wa kujituma kuwafundisha wanafunzi hususani wanafunzi wasiojua K.K.K. na wanajiandaa kufanya mitihani ya taifa darasa la nne na la saba.

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...