Sunday, 5 March 2017

KILIMO BORA CHA MIEMBE



Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini
MIEMBE hulimwa karibu katika nchi zote zilizoko kwenye ukanda wa joto, na hasa tropiki. Nchini Tanzania miembe hulimwa zaidi kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya (wilayani Kyela), Morogoro, Mtwara, Mwanza, Pwani, Tabora na Tanga, MaendeleoVijijini inakuletea ripoti kamili ya kilimo hicho.

Taarifa za Wizara ya Kilimo, Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi zinaonyesha kwamba, uzalishaji wa maembe nchini ni wastani wa tani 159,472 kwa mwaka na kwa kawaida maembe ni miongoni mwa matunda ya bustani yanayochangia Pato la Taifa (GDP).

Waswahili huwa wanasema; “Usidharau dafu, embe tunda la msimu!”Wako sahihi kwa sababu dafu linapatikana wakati wote, lakini embe hupatikana kwa msimu.
Lakini japokuwa ni tunda la msimu, lakini embe linafahamika kama mfalme wa matunda kutokana na ladha na harufu yake. Msimu wa embe unajulikana kwa harufu ambayo hutamalaki.

Rangi ya nyama ya embe iliyo ya njano huvutia walaji na asilimia 60 mpaka 70 ya tunda lililoiva huliwa. Linaweza kuliwa kama tunda, lakini pia hukamuliwa kupata maji ya matunda, hutengenezwa jamu, saladi, siki na achali.
Embe mbivu ina sukari, vitamin A, B na C kwa wingi, hivyo ni tunda muhimu kwa lishe na afya ya binadamu.


Mazingira mazuri
Miembe hupendelea kipindi kirefu cha jua, joto la wastani ambalo ni nyuzi joto 25 za Sentigredi na mwinuko wa kuanzia meta 0 hadi 600 kutoka usawa wa bahari.
Miembe hustawi zaidi katika maeneo yanayopata wastani wa mvua kati ya milimeta 650 hadi 1,800 kwa mwaka na udongo wenye kina kirefu, unaopitisha maji kwa urahisi na wenye uwezo wa kushika unyevu kwa muda mrefu.
Kwa kawaida, miembe hupendelea uchachu wa udongo (soil pH) kati ya 5.5 na 7. Udongo wenye uchachu zaidi ya 7 huwa na upungufu wa madini aina ya zinki na chuma.


Aina za miembe
Zipo aina nyingi za miembe, hata hivyo, zinaweza kugawanywa katika makundi matatu kulingana na sifa zifuatazo:
a) Umbile la Mti, Maua na Majani
Katika kundi hili kuna aina fupi na ndefu. Aina fupi ni kama vile miembe Chotara, Sabre, Kent, Keith, Tommy Atkins na Alphonso. Aina ndefu ni kama vile Sindano na Boribo.
b) Umbo, Ukubwa, Uzito, Ladha na Ubora wa Tunda
Aina za miembe yenye matunda makubwa ni Dodo na Sabre. Aina zenye matunda madogo ni Sindano na Mawazo.
c) Mazingira yanayofaa kwa kilimo chake
Mazingira hayo ni kama vile; hali ya hewa, ubebaji wa matunda, msimu wa kuvuna na ustahimilivu wa magonjwa na mashambulizi ya wadudu. Aina zinazopendelea mwinuko wa juu ni kama vile Sabre na zinazopendelea mwinuko wa chini ni Boribo, Sindano na Dodo.


Njia za kuzalisha miembe
MaendeleoVijijini inaelewa kwamba, njia kuu zinazotumika kuzalisha miembe ni kupanda mbegu halisi moja kwa moja shambani au kupandikiza miche iliyobebeshwa (Graft Method).
a) Kupanda mbegu moja kwa moja shambani
- Shamba ni lazima litayarishwe mwezi mmoja hadi miwli kabla ya kupanda mbegu. Tayarisha shamba kwa kuchimba mashimo yenye ukubwa wa sentimeta 90 upana na urefu. Kina kiwe na sentimeta 60.
- Mashimo yenye ukubwa huo yatumike sehemu zenye ukame. Sehemu zinazopata mvua nyingi tumia mashimo yenye ukubwa wa sentimeta 60 upana, urefu na kina.
- Nafasi kutoka shimo hadi shimo ni meta 10 mpaka 15 na kati ya mstari na mstari ni meta 10 hadi 15. Hata hivyo, nafasi ya kupanda hutegemea aina ya miembe.
- Mashimo yakishakuwa tayari, jaza mbolea za asili kama vile samadi au mbolea vunde zilizooza vizuri kiasi cha debe mbili hadi tatu kwa kila shimo.
- Changanya mbolea na udongo wa juu pamoja na gramu 250 za mbole ya chokaa (Triple Super Phosphate – TSP).
- Wakati mzuri wa kupanda ni mwanzoni mwa msimu wa mvua.
- Panda mbegu zilizokomaa vizuri mara baada ya kuzitoa kwenye kokwa. Mbegu zipandwe katika kina cha sentimeta tano. Mwagilia baada ya kupanda na endelea kumwagilia hadi mbegu zitakapoota. Mbegu huota baada ya siku 20.
b) Njia ya Kubebesha (Graft Method)
Miche kwa ajili ya kubebesha hukuzwa kwanza kitaluni na baadaye huhamishiwa shambani baada ya kubebeshwa.
Katika kitalu, mbegu hupandwa kwenye mistari yenye nafasi ya sentimeta 30 mstari hadi mstari. Nafasi kati ya shimo na shimo ni sentimeta 15. Mbegu pia zinaweza kupandwa kwenye vifaa kama vile mifuko ya plastiki, vikapu vya majani au viriba vya majani ya migomba vyenye urefu wa sentimeta 30. Vifaa hivyo hujazwa udongo uliochanganywa na mbolea za asili zilizooza vizuri.

Jinsi ya kubebesha

- Miche hubebeshwa inapofikia umri wa miezi sita hadi 18. Kata kikonyo kutoka kwenye miti inayozaa matunda bora na ambayo haina magonjwa wala wadudu waharibifu.
- Chagua kikonyo chenye unene ulio sawa na ule wa mchemama na urefu wa sentimeta 20.
- Kikonyo kiwe na vichomozo viwili hadi vitatu.
- Chonga pande mbili za kikonyo kwa urefu kiasi cha sentimeta mbili hadi tano. Wakati wa kuchonga hakikisha mamcho yanaangalia juu.
- Kata sehemu ya juu ya mchemama sentimeta 25 kutoka usawa wa ardhi.
- Pasua mchemama katikati sentimeta mbili hadi tatu kuanzia juu kwenda chini.
- Chomeka kikonyo kwenye mkato huo.
- Funga kwa kutumia uutepe wenye urefu wa sentimeta 25 na upana wa sentimeta moja.
- Baada ya siku 30 hadi 45, fungua utepe kuangalia kama kikonyo kimeunga. Kama kimeunga, legeza utepe na acha mpaka mche utoe majani.
- Miche huwa tayari kupandikizwa shambani ifikiapo umri wa miezi 12 kuanzia ilipobebeshwa.


Kupandikiza michezo shambani
Mashimo yatayarishwe mwezi mmoja kabla ya kupandikiza. Tayarisha kwa kuweka mbolea za asili kama vile samadi kiasi cha madebe mawili hadi matatu kwa kila shimo. Pandikiza miche mwanzoni mwa msimu wa mvua au wakati wowote kama unatumia kilimo cha umwagiliaji.
Miti iliyobebeshwa huwa na umbile dogo hivyo huhitaji nafasi ndogo ambayo ni meta nane hadi 10 kati ya mstari na mstari na kati ya shimo na shimo.


Changanya na mazao mengine
Miembe inaweza kuchanganywa na mazao mengine kwa miaka mitano hadi sita ya mwanzo.
Mazao ambayo yanaweza kuchanganywa ni kama vile mananasi, migomba na aina mbalimbali za mboga.


Utunzaji wa shamba
MaendeleoVijijini inasisitiza kwamba, jambo la muhimu kabisa ni palizi. Katika shamba la miembe, palizi hufanyika kwa kufyeka majani yote na kutengeneza kisahani kuzunguka shina.
Weka madebe mawili hadi matatu ya mbolea za asili kama vile samadi kwa mti kila mwaka.
Mbole ya N.P.K. pia inaweza kuwekwa ambapo kiasi kinachotakiwa ni kilo moja kwa mti kila mwaka.
Mbolea inapaswa kuwekwa mwanzoni mwa msimu wa mvua.


Magonjwa yanayoshambulia miembe
Miembe, kama mimea mingine, hushambuliwa na magonjwa mbalimbali, lakini yaliyo makubwa ni haya yafuatayo:


Chule (Anthracnose)
Huu ni ugonjwa wa ukungu unaoshambulia majani na matunda.



Dalili zake
- Majani huwa na madoadoa meusi ambayo baadaye huwa makubwa na makavu.
- Maua pia huwa na madoa madogo meusi yaliyosambaa.
- Maua hupukutika.
- Matunda huwa na mabaka madogo meusi ambayo baadaye huwa makubwa na yenye rangi ya kikahawia iliyochanganyika na nyeusi.
- Kukiwa na unyevu mwingi, ukungu wa rangi ya pinki huonekana katikati ya baka. Hali hiyo husababisha maembe mamchanga kudondoka.


Kuzuia

- Nyunyizia dawa za ukungu kama vile Dithane M-45. - Ondoa matawi yote yaliyozeeka kabla ya maua kutoka.


Ubwirijivu (Powdery Mildew)
Huu pia ni ugonjwa unaosababishwa na kuvu au ukungu. Hushambulia zaidi maua, majani na matunda.


Dalili
- Maembe machanga huanguka kabla ya kukomaa.
- Matunda yaliyokomaa huwa na ranggi ya kahawia.


Kuzuia
Nyunyizia dawa za ukungu aina ya Sulphur Dust au Baylaton.




Wadudu Waharibifu
MaendeleoVijijini inatambua kwamba, miembe hushambuliwa na wadudu wengi. Baadhi ya wadudu hao ni vijasidi, vidugamba, vidung’ata na nzi wa tunda aliyezoeleka na nzi wa tunda mgeni (Bactrocera evadens).


Nzi wa Tunda Mgeni (Bactrocera evadens)
Nzi huyu ni hatari zaidi katika uzalishaji wa maembe. Nadhani unafahamu ule wimbo wa “Mdudu kaingiaje ndani ya kokwa la embe”! Basi huyu nzi ndiye kisababishi kikubwa.


Dalili
- Kuanguka kwa maembe kiasi cha asilimia 50 hadi 80.
- Maembe yakikatwa huwa yameoza na mara nyingi yanakuwa na funza wengi.


Kuzuia
- Fukia maembe yaliyoanguka katika kina cha futi tatu.
- Palilia mara kwa mara eneo lililo chini ya miembe ili kuwaacha wazi funza na buu waweze kushambuliwa na wadudu walawangi au kuathiriwa na hali mbaya ya hewa katika ukuaji wake.
- Ondoa au fyeka miti ya matunda ya porini ambayo iko karibu na shamba la miembe ili kupunguza mazalio ya nzi nje ya msimu wa embe.
- Vuna maembe ambayo hayajashambuliwa yakiwa bado juu ya mti. Hali hiyo inapunguza ongezeko la idadi ya nzi katika shamba.
- Tumia vivutio vilivyochanganywa na dawa aina ya Decis au dawa yoyote ya wadudu ili kuua majike ya nzi huyo.
- Tumia dawa ya kuvutia dume (Pheromone) aina ya Methly eugenoliliyochanganywa na dawa ya Dichlorovos ili kuua nzi dume.
- Nyunyiza dawa aina ya Dimethoate.
- Tumia mbinu husishi.


Tahadhari
- Wakulima ambao mashamba yao yanapakana wanashauriwa kufanya zoezi la kudhibiti kwa pamoja ili kuzuia uwezekano wa wadudu hao kuhamia shamba linguine ambalo hatua za kmdhibiti hazijachukuliwa.
- Wadudu wengine wanaweza kuzuiwa kwa kunyunyizia dawa aina ya Selectron au Sevin. Dawa zinyunyiziwe wakati miembe imetoa maua. Kwa ushauri zaidi muone mtaalam wa kilimo.


Uvunaji wa maembe
MaendeleoVijijini inafahamu kwamba, miembe ambayo haikubebeshwa huanza kuzaa inapofikia umri wa miaka sita hadi saba tangu kupanda mbegu. Lakini ile iliyobebeshwa huzaa inapofikia umri wa miaka miwili mpaka mitatu tangu kupandikiza miche.
Uvunaji wa maembe hutegemea matumizi yaliyokusudiwa. Mfano, maembe kwa ajili ya matumizi ya nyumbani huvunwa baada ya kkuanza kubadilika rangi kutoka kijani kibichi na kuwa njano. Maembe kwa ajili ya kusafirisha huvunwa yangali bado na rangi ya kijani kibichi lakini yamekomaa.
Njia bora ya kuvuna maembe ni kuchuma kwa mikono ambapo matunda huchumwa pamoja na vikonyo vyake. Acha kikonyo chenye urefu wa sentimeta tatu hadi nne ili kuzuia utomvu. Utomvu huchafua matunda na hushusha ubora wake. Embe lililovunwa bila kikonyo huingiliwa na vimelea vya magonjwa kwa urahisi.
Vuna maembe wakati wa asubuhi au jioni ili kuepuka jua kali linaloweza kuharibu matunda. Wakati wa kuvuna hakikisha maembe hayadondoshwi chini ili kuepuka uharibifu.
Mavuno hutegemea aina na umri wa mti. Mti wenye umri mdogo unaweza kuzaa wastani wa matunda 4000 hadi 600 kwa msimu. Mti mkubwa unaweza kuzaa matunda 10,000 na zaidi. Wastani wa mavuno ni tan inane kwa hekta moja.


AFRICAN PRESIDENTS AND THEIR AGES


Saturday, 4 March 2017

WATANZANIA WAHIMIZWA KUCHANGAMKIA HISA ZA KAMPUNI YA TCCIA INVESTMENT



Rais wa Chama cha Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo TCCIA, Ndibalema John Mayanja (katikati), akizungumza hii leo Jijini Mwanza kwenye mkutano na wadau mbalimbali wa biashara. Kulia ni Makamu Mwenyekiti TCCIA mkoani Mwanza, Leopord Lema, na kushoto ni Mshauri TCCIA mkoani Mwanza, Lazaro Kiheya.




BMGHabari

Rais wa Chemba ya Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo nchini TCCIA, Ndibalema Mayanja, amewahimiza watanzania kuchangamkia fursa ya ununuaji wa hisa za kampuni ya TCCI Investment.




Mayanja ameyasema hayo Jijini Mwanza hii leo na kubainisha kwamba hisa hizo zilianza kuuzwa tangu Februari Mosi mwaka huu kwa bei ya shilingi Mia Nne na kwamba mwisho wa uuzwaji wa hisa hizo ni Machi 14 mwaka huu.




"Njia pekee ya kijiendeleza kiuchumi hivi sasa ni kupitia hisa hivyo nunueni hisa hizi za kampuni ya uhakika ambayo kila mwaka huwapatia wanahisa wake gawiwo lao". Amesisitiza Mayanja na kuongeza kwamba hisa hizo zinauzwa katika benki ya CRDB na kwa mawakala mbalimbali walioidhinishwa na Mamlaka ya Masoko na Dhamana (CMSA).




Mwenyekiti wa TCCIA mkoani Mwanza, Joseph Kahungwa, amebainisha kwamba walionunua hisa za TCCIA Investment mwaka 2005 kwa shilingi 250, hisa zao zimepanda bei hadi shilingi 5,000 hivyo pesa hiyo iligawanywa na kupatikana bei ya shilingi 400 ya kuuza hisa mwaka huu ambapo kwenye mauzo hayo kila mwanahisa atapata gawio la hisa 12.5 kwa kila hisa moja.




Makamu Mwenyekiti TCCIA mkoani Mwanza, Leopord Lema, mesema jumla ya hisa Milioni 112 zinatarajiwa kuuzwa lengo ikiwa ni kampuni ya TCCIA Investment kupanua mtaji wake na kufikia Bilioni 45 kutoka Bilioni Nane za mwaka huu 2017 ambazo zimeongezeka kutoka hisa Bilioni Moja mwaka 2005 wakati kampuni hiyo inaanzishwa.




Amedokeza kwamba hatua hiyo itasaidia TCCIA kuongeza uwekezaji wake ikiwemo ujenzi wa majengo ya kisasa na maghara ya kuhifadhia mazao katika mikoa ya Dar es salaam, Dodoma, Mtwara na Tanga pamoja na kuanzisha taasisi ya mikopo.


Makamu Mwenyekiti TCCIA mkoani Mwanza, Leopord Lema, akisisitiza juu ya umuhimu wa watanzanua kununua hisa za Kampuni ya TCCIA Investment. Pia amesema TCCIA itaendelea kushirikiana na serikali katika kuondoa changamoto za kiuwekezaji zilizopo ikiwemo upimaji wa maeneo ya ujenzi wa viwanda pamoja na uwanja wa maonesho ikiwemo Maonesho ya Biashara ya Afrika Mashariki


Mshauri TCCIA mkoani Mwanza, Lazaro Kiheya akitoa neno la shukurani kabla ya mkutano huo kuahilishwa. Kulia ni Rais wa TCCIA, Ndibalema Mayanja.


Meneja Elimu kwa Mlipa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA mkoani Mwanza, Lutufyo Mtafywa (kulia), akizungumza kwa niaba ya meneja wa TRA mkoani Mwanza katika mkutano huo. 




Ameelezea umuhimu wa kila mfanyabiashara kuwa namba ya utambulisho wa biashara (TIN Number) na kuwasihi kutoa ushirikiano kwenye zoezi la uhakiki wa namba hizo ambapo amesema baada ya kufanyika Jijini Dar es salaam, litaendeleo Jijini Mwanza na maeneo mengine pia.


Mmoja wa wafanyabiashara waliohudhuria mkutano huo akiwasilisha maoni na ushauri wake


Baadhi ya wafanyabiashara na wadau wa biashara na uwekezaji wakifuatilia mkutano huo


Baadhi ya wafanyabiashara na wadau wa biashara na uwekezaji wakifuatilia mkutano huo

BARAZA LA MADIWANI MANISPAA YA UBUNGO LAPITISHA BAJETI YA ZAIDI YA BILIONI MIA MOJA



Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo Jijini Dar es salaam wakiwa katika kikao cha kupitisha makisio ya mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 (Picha zote na Nassir Bakari)



Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo akisisitiza jambo wakati wa kikao cha kupitisha makisio ya mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 kulia kwake ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo Mhe Boniface Jacob


Kushoto ni Muweka hazina wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo Bi Jenny Machicho, Afisa utumishi Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo Ally Juma Ally, na Mchumi wa Halmashauri ya manispaa ya Ubungo Yamo Wambura wakiwa katika kikao cha kupitisha makisio ya mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018


Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo Mhe Boniface Jacob akizungumza wakati wa kikao cha kupitisha makisio ya mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 (kushoto) ni Naibu Meya wa Manispaa hiyo Mhe Ramadhan Kwangaya na (kulia) ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo 





Mchumi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo Yamo Wambura akitoa ufafanuzi kuhusu baadhi ya matumizi ya fedha kwenye kikao cha kupitisha makisio ya mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018




Na Mathias Canal, Dar es salaam


Baraza la madiwani katika Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo Jijini Dar es salaam kwa kauli moja limepitisha makisio ya mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 kwa kuungwa mkono na madiwani wote waliozuru katika mkutano maalumu wa baraza hilo.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa waandishi wa habari na Kaimu Afisa habari na Uhusiano wa Manispaa hiyo Bi Maria Makombe imeeleza kuwa katika mpango huo Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo inakadiria kukusanya/kupokea kiasi cha Tshs 128,611,616,805.100 ambazo zimeelekezwa katika matumizi ya mishahara, utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo na matumizi mengineyo.



Fedha hizo zitatokana na makusanyo ya ndani ya Halmashauri, Ruzuku kutoka serikali kuu, Michango ya wananchi na wahisani wa Maendeleo.


Aidha Halmashauri inatarajia kupokea kiasi cha Tshs 4,233,546,143.00 kutoka TAMISEMI kwa ajili ya kutekeleza miradi ya ujenzi wa barabara (Road Fund).


Katika fedha hizo chanzo cha makusanyo ya ndani ni Tshs 24,006,600,000.00 ambayo ni Sawa na asilimia 26% ya bajeti, Michango ya wananchi ni Tshs 500,000,000 Sawa na asilimia 1% ya bajeti, Mfuko wa barabara ni Tshs 4,233,546,143.00 Sawa na asilimia 4% ya bajeti na ruzuku kutoka serikalini na wahisani wa maendeleo ni Tshs 59,892,884,406.00 Sawa na asilimia 69% ya bajeti.



Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo Mhe Boniface Jacob akisoma makisio ya bajeti ya Halmashauri ya Manispaa hiyo ameyataja maeneo yaliopata kipaumbele katika mpango huo kuwa ni pamoja na Kuboresha na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Manispaa, pamoja na Ujenzi wa ofisi za Makao makuu ya Halmashauri ya Manispaa hiyo.




Vipaumbele vingine ni kuboresha miundombinu ya afya,shule za msingi na sekondari, kuboresha miundombinu ya maji, mifereji, taa za barabarani na kilimo mjini, Kuboresha hifadhi ya mazingira na ukusanyaji wa taka, Kuimarisha ushirikishwaji wa jamii katika upangaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo sambamba na Kuboresha mazingira ya wafanyabiashara ndogondogo.




Mhe Jacob ameeleza kuwa Manispaa hiyo ya Ubungo imejipanga kusimamia vyema uimarishaji wa mahusiano mazuri kati ya serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau wengine, Kuendelea kujenga uwezo na ujuzi kwa watumishi katika utoaji wa huduma zilizo bora na zaharaka, kuimarisha utawala bora, uwajibikaji na uwazi sambamba na Kujenga uwezo kwa viongozi wakiwemo waheshimiwa madiwani na wenyeviti wa serikali za mitaa katika kusimamia shughuli za wananchi.

Katika makisio ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo kwa 2017/2018 asilimia 72% itatumika kwa matumizi ya kawaida na asilimia 28% itatumika katika kutekeleza miradi ya maendeleo.


Maombi maalumu yamewasilishwa kupitia bajeti hii ambapo ni pamoja na maombi ya fedha kwa ajili ya ujenzi wa Makao makuu ya Halmashauri, Ujenzi wa Zahanati, Ununuzi wa magari, Malipo ya fidia kwa wananchi kwa maeneo yaliyochukuliwa na Halmashauri kwa ajili ya matumizi ya umma.


Mstahiki Meya alieleza Dira na dhima ya Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kuwa ni kuwa na jamii inayohamasika, inayokubalika ikiwa na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.



Kwa upande wake Mkurugenziwa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo akizungumza wakati wa mkutano huoamesema kuwa Bajeti hiyo ina mambo mengi ambayo ni muhimu katika ustawi wa Manispaa hiyo hivyo ushirikiano wa pamoja kati ya madiwani na watumishi wa Manispaa hiyo itaimarisha mapato na uimara wa maendeleo katika jamii kwa kuwashirikisha wananchi.



MD Kayombo amebainisha kuwa Bajeti hiyo ina vipaumbele vingi lakini vile vilivyo muhimu zaidi vitafanyiwa kazi haraka iwezekanavyo kwani ni sehemu ya kuimarisha nakukamilisha mipango ya mudamfupi katika Halmashauri.



Alisema kuwa makadirio ya mwaka 2017/2018 ya Tshs 128,611,616,805.00 yana ongezeko la kiasi cha Tshs 12,565681,576.01 ambapo Bajeti hii imepanda kwa asilimia 10 ukilinganisha na makisio ya Bajeti ya mwaka 2016/2017 ambayo yalikadiriwa kuwa ni Tshs 116,045,935,228.99.


Vipaumbele vya bajeti hii ya mwaka 2017/2018 ya Manispaa ya Ubungo vimewekwa katika sekta mbalimbali, ambapo Halmashauri imelenga kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kutumia mfumo wa kielektroniki, Kuboresha mazingira ya kufanyia kazi na kutoa huduma kwa kujenga ofisi za Halmashauri, Kuboresha utoaji huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi kwa wakazi, Kutoka mikopo kwa wajasiriamali, Kuboresha usafi wa mazingira na Kuboresha miundo mbinu ya barabara, Shule na Afya.


MISA TANZANIA YAWATUNUKU VYETI WANAHABARI KANDA YA ZIWA



Mmoja wa washiriki wa mafunzo kwa wanahabari kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa ambayo ni Mwanza, Mara, Geita na Simiyu, walionufaika na mafunzo yaliyotolewa na taasisi MISA Tanzania, akipokea cheti cha ushiriki kutoka kwa mwakilishi wa taasisi ya FES Tanzania (katikati), iliyofadhiri mafunzo hayo.



#BMGHabari

Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA) tawi la Tanzania, imewatunuku vyeti vya ushiriki wanahabari kutoka vyombo mbalimbali katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.



Wanahabari waliopatiwa vyeti hivyo ni waliopatiwa mafunzo ya kuwajengea uelewa juu ya Sheria Mpya ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 na Kanuni zake za mwaka 2017.



Mafunzo hayo ya siku mbili yalianza juzi alihamisi na kutamatika jana katika Hotel ya Adden Pallace Jijini Mwanza, yakifadhiliwa na Taasisi ya Friedrick Ebert Stiftung (FES) tawi la Tanzania.



Akizungumza mapema kabla ya kukabidhi vyeti kwa washiriki, mwakilishi wa taasisi ya FES Tanzania, Violet John, aliwahimiza wanahabari kutumia vyema hayo vyema katika kuboresha kazi zao huku pia akiwahimiza kufikisha kwa wenzao yale waliyojifunza.


Edwin Soko ambaye ni mmoja wa wanahabari waliopatiwa mafunzo hayo, aliishukuru MISA Tanzania kwa kutambua umuhimu wa wanahabari kujifunza kuhusu Sheria Mpya ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 na Kanuni zake za mwaka 2017 na kubainisha kwamba elimu hiyo wataifikisha kwa wenzao.



























WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...