Na Friday Simbaya, Iringa
Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Mheshimiwa Jaji Shanghali amesema Kanda ya Mahakama Kuu Iringa ambayo inajumuisha mkoa wa Njombe kwa sasa wana mashauri 1,777.
Alisema kuwa Kati ya mashauri hayo, wanayo mashauri 211 tu yenye umri zaidi ya miaka miwili (2) ambayo kati yake ni mashauri 123 ya Jinai (Mauaji) na mashauri 87 ya Madai.
Jaji Shanghali alisema hayo jana wakati wa sherehe za sheria nchini zilizofanyika katika viwanja vya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa.
Alisema kuwa katika mashauri mengine yote 1,566 yana umri chini ya miaka miwili (2).
“Takwimu zinaonyesha kuwa ni asilimia nane (8%) tu ya mashauri ya muda mrefu yaliyobaki kwa nchi nzima, ” alisema Jaji Shanghali.
Aliongeza kuwa wajibu wa Mahakama ni kutekeleza jukumu lake la utoaji haki kwa wakati na Mashauri yasikilizwe na kupatiwa ufumbuzi kwa wakati bila kuchelewa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alisema kuwa haki ikitolewa kwa wakati wananchi watafanya shughuli zao za maendeleo wakiwa huru na kwa ufanisi.
“Haki ikinyimwa maendeleo hayawezi kupatikana kwa kuwa wananchi hawatakuwa huru kufanya shughuli zao kikamilifu na hivyo kudidimiza kasi ya maendeleo,” alisema Masenza.
Alisema kuwa Ibara ya 11, ya Katiba ya Jumhuri ya Muungano wa Tanzania inampa haki kila mwananchi kufanya kazi kwa bidii na kwamba kila mtu ataishi kwa jasho lake.
Masenza alisema kuwa Mahakama ni mamlaka ya utoaji haki kikatiba na ili kuharakisha ukuaji wa uchumi na kuomba ijitahidi kwa kadri iwezavyo kuharakisha kutoa haki ili kuchochea kasi ya maendeleo kwa wananchi.
“Tumeshuhudia mlundikano wa mashauri katika Mahakama, Upelelezi kuchukua muda mrefu, mlundikano wa watuhumiwa katika mahabusu, mashauri kuchukua muda mrefu bila sababu za msingi, masharti magumu ya dhamana,” alisema Masenza.
Mkuu wa Mkoa huyo aliviomba vyombo vyote vinavyohusika katika utoaji wa haki (polisi, Waheshimiwa Majaji, Mawakili wa Serikali na wa kujitegemea, Viongozi wa Serikali, Watumishi wote wa Mahakama washirikiane kwa pamoja katika kutoa haki ili kuchochea maendeleo).
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mawakili wa kujitegemea Kanda ya Mahakama Kuu Iringa Rwezaula Kaijage akisoma hotuba yake alisema kuwa wananchi wakiwemo Watuhumiwa na Mashahidi wasipoteze muda mwingi Mahakamani wakati shughuli zao za kilimo, biashara na uchumi zimesimama.
Alisema kuwa Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau wake wachukua hatua kadhaa kuhakikisha kuwa mashauri hayakai Mahakamani kwa muda mrefu.
Kaijage alisema kuwa hali hiyo, wananchi wanapokuwa Mahakamani, wanategemea na wanatamani mashauri yao yasikilizwe na kutolewa uamuzi mapema ili mashauri yakiishamalizika, waendelee na shughuli za kujenga uchumi.
Alisema kuwa Tanzania ya viwanda haitawezekana kama mashauri yatachukua miezi na hata miaka bila kumalizika yakiwafanya wahusika na mashaidi wao kufika mahakamani kila mara ili hali wakiacha shughuli zao za uchumi.
“Katika Mkoa wetu wa Iringa, tunao mfano mzuri wa Wilaya ya Kilolo ambayo ina Mahakama ya Wilaya, lakini haina gereza na ofisi ya mkuu wa polisi wa wilaya hiyo iko kilomita karibu sabini toka makao makuu ya wilaya,” alisema.
Alisema kuwa hali hii imeifanya wilaya hiyo ipange kusikiliza mashauri ya jinai kwa siku mbili katika juma na hii ni kutokana na uwezo mdogo wa mkuu wa polisi wa wilaya kusafirisha mahabusu kutoka gereza la Iringa mjini hadi Kilolo.
Kila siku ya mashauri hayo, mwendesha mashtaka analazimika kusafiri kutoka Mbigili, kuja Iringa mjini, kuwachukua mahabusu na kuwapeleka Kilolo.
“Baada ya mashauri safari hiyo inajirudia. Tumeshuhudia mara nyingine mkuu wa polisi akishindwa kupata usafiri wa kuwafikisha mahabusu mahakamani wakati mashahidi wamekwishaandaliwa,” alisema Kaijage.
Hata hivyo, alisema kuwa Mabishano ya kisheria miongoni mwa mawakili wanaowatetea wadaawa au watuhumiwa; ama miongoni mwa mawakili wa kujitegemea na waendesha mashitaka ndio sababu mojawapo inayochelewesha haki kutolewa kwa wakati.
Wakati mwingine suala hili linachelewesha haki kutolewa mapema kwa sababu ya wahusika kutokuwa makini na wakati mwingine kuwa wabishi hata wanapokuwa wameishaoneshwa ukweli.
Wakati kama huo, Mahakama hulazimika kuingia katika kusikiliza kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi jambo ambalo huchelewesha maamuzi
Pia alisema kuwa ucheleweshwaji wa kuanza kutumika sheria ya kuwaruhusu mawakili kuwatetea wateja wao kwenye Mahakama za Mwanzo ni sababu nyingine inayofanya mashauri kurundikana mahakamani pamoja na mahabusu.
Hivi sasa mahakama za mwanzo zina mahakimu waliohitimu shahada ya sheria na kuajiriwa katika kada ya Mahakimu Wakazi na baadhi yao wana shahada za uzamili na hivyo bila ya shaka wana uwezo mkubwa.
Alisema kuwa Kuendelea kuwazuia mawakili kufanya kazi katika mahakama za mwanzo kunasababisha mashauri ambayo yangemalizika katika hatua hiyo, kuendelea kwenye mahakama za juu kwa njia ya rufani au marejeo na hivyo kuwafanya wahusika waendelee kujenga vibanda mahakamani.
“Tunaomba Bunge liingilie kati mapema ili kunusuru hali hii…,” alisema Kaijage.
Mwisho
No comments:
Post a Comment