Na Friday Simbaya, Kilolo
Mwenyekiti wa Kijiji cha Idete, Bimas Mkemwa katika Kata ya Idete amesema kuwa elimu na utafiti iliyotolewa na mashirika yasio kuwa ya kiserikali ya Mazombe Mahenge Development Association (MMADEA) na Iringa Civil Society Organization (ICISO) wilayani Kilolo, mkoani Iringa vimewafungua kwa kiasi kikubwa wananchi kuhusu upatikanaji wa huduma za afya.
Mkemwa aliyasema hayo katika mkutano wa kutoa mrejesho wa utafiti uliofanywa na shirika la CISO uliofanyika wilayani Kilolo juzi.
Kiongozi huyo wa kijiji aliiomba serikali kuwajengea kituo cha afya ili kuboresha afya ya mama na mtoto katika Kijiji cha Idete na kata ya Idete kwa ujumla.
Alisema kuwa wananchi wa Kijiji cha Idete na kata Idete, wilayani Kilolo mkoani Iringa wameitaka serikali kwa kusaidiana na wadau mbalimbali kuwajengea kituo cha afya ili waweze kuondokana na adha ya wajawazito kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya.
Alisema kuwa ubovu wa miundombinu ya barabara ya Idete hasa katika kipindi hiki cha mvua kunasababisha kina mama wengi kujifungulia njiani, huku wakishindwa kumudu gharama ya kukodi gari la wagonjwa (ambulance) kutoka zahanati ya misheni ya Madege.
Alisema kuwa wananchi wamekuwa wakikodi gari hilo kati ya shilingi laki mbili na nusu (250,000/-) na laki tatu (300,000/-) kutoka Idete hadi Iringa mjini kwa ajili ya kufuata huduma ya afya hususani kina mama wanapoenda kujifungua.
Mwenyekiti wa kijiji cha idete Bimas Mkemwa alisema miundombinu mibaya imepelekea hata kuvunjika kwa baadhi ya ndoa pamoja na mimba za utotoni kwa vile wakina mama na wasichana wanalazimika kulala kwenye mabasi ili kuwahi kwenda mjini.
“Barabara hii ni barabara ya mkoa inayoishia katika kijiji cha Idete lakini basi likitoka mjini linaishia Kidabaga ambapo wanalazimika kukodi bodaboda kwa shilingi 18,000/- hadi kidabaga kupanda basi kesho yake. Gaharama hiyo ya usafiri ni kubwa ukilinganisha na nauli ya basi yenyewe kutoka Idete hadi mjini Iringa ni elfu nne…,” alisema Mkemwa.
Aliongeza kuwa wananchi wanalazimika kulala kwenye mabasi kutokana na kutokuwa na hela ya kulala gesti na kupelekea kina mama na mabinti kufanyiwa vitendo visivyofaa wanapolala kwenye mabasi.
Aliiomba serikali kuboresha miundombinu ya barabara ili kurahisisha usafiri pamoja na kuwajengea kituo cha afya ili kuboresha afya ya mama na mtoto katika maeneo yao.
Hata hivyo, halmashauri ya wilaya ya Kilolo imeahidi kuutumia utafiti uliofanywa na Mwamvuli wa Mashirika Yasio ya Kiserikali Mkoani Iringa (ICISO Umbrella) kushughulikia changamoto mbalimbali zinazokwamisha utoaji wa huduma bora ya afya ya uzazi na mtoto.
Afisa Maendeleo ya Jamii wa halmashauri ya wilaya hiyo, Phillemon Naminga alisema changamoto nyingi zilizobainishwa kupitia taarifa ya utafiti huo zinasababishwa na pengo la mawasiliano na elimu ya utawala bora.
“Mtiririko wa kupeana taarifa kutoka chini hadi ngazi ya halmashauri ya wilaya sio mzuri, kuna pengo la namna ya kupena taarifa kati ya wananchi na viongozi na wakati mwingine viongozi wenyewe,” alisema.
Naminga alisema watautumia utafuti huo kutoa elimu ya utawala bora katika ngazi zote za halmashauri, ili taarifa za changamoto zinazohusu upatikanaji wa huduma hizo na nyingine zifikishwe na kufanyiwa kazi kwa kuzingatia taratibu.
Katibu Mtendaji wa ICISO, Raphael Mtitu alisema utafiti huo uliofanywa kwa miezi sita (Oktoba 2016 hadi Machi 2017) katika vijiji 40 vya kata ya Ibumu, Image, Idete, Irole, Ilula, Nyalumbu, Ruaha Mbuyuni, Uhambingeto na Nyanzwa.
Alisema kuwa utafiti huo uliofadhiliwa na The Foundation for Civil Society ulilenga kuziwezesha asasi za kiraia na wananchi kutathimini na kupima matumizi ya fedha za umma katika serikali za mitaa juu ya ubora na uridhishwaji wa huduma zitolewazo, hususani kwenye afya ya uzazi na mtoto.
Mtitu alisema matokeo ya utafiti huo yanaonesha watu 319 sawa na asilimia 65 ya wahojiwa wote wameeleza uwepo wa huduma ya afya ya uzazi na mtoto katika maeneo yao na watu 172 walisema hakuna huduma hizo katika maeneo yao.
“Hiyo ni kwasababu ya kutokuwepo kwa vituo vya kutolea huduma katika vijiji vyao au wananchi na baadhi ya vijiji kuwa mbali na vituo vya kutolea huduma za afya,” alisema.
Akizungumzia umbali wa upatikanaji wa huduma, Mtitu alisema utafiti unaonesha zinapatikana kwa umbali wa kati ya kilimota moja na nne na zaidi ya kilomita tano huku miundombinu ya kufika katika baadhi ya vituo hivyo ikiwa mibovu.
Alisema utafiti huo unaonesha pia kwamba wananchi wanatumia wastani wa saa moja hadi saa mbili kupata huduma hizo katika vituo vya kutolea huduma ingawa kuna baadhi wanatumia zaidi ya saa nne.
“Kuna haja ya kuwa na watoa huduma wa kutosha na vifaa tiba vya kutosha ili wananchi waweze kupata huduma kwa muda mfupi na kuwaepusha kwenda kwa waganga wa kienyeji au kujaribu kujitibu wao wenyewe,” alisema.
Alizitaja changamoto zingine zilizobainika kupitia utafiti huo kuwa ni pamoja na upungufu wa dawa, baadhi ya wananchi kutokuwa na elimu ya uzazi bora, ukosefu wa magari ya kubeba wagonjwa na tatizo la mawasiliano hasa kwa wajawazito na watoto wanaohitaji huduma za haraka.
Wakitoa maoni yao baada ya taarifa ya utafiti huo kuwasilishwa, wadau wa sekta hiyo waliiomba serikali iboreshe huduma hiyo huku vipaumbele vyao vikiwa ni huduma ya kliniki, usafiri kwa wajawazito, vifaa tiba, na huduma ya wakunga kabla na baada ya kujifungua.
MWISHO
No comments:
Post a Comment