Wednesday, 9 November 2016

HOSPITALI MKOA WA IRINGA KUENDESHA KLINIKI YA KUPIMA KISUKARI NA SHINIKIZO LA DAMU




Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa itaendesha Kliniki ya kupima ugonjwa wa Kisukari na Shinikizo la Damu kwa wananchi wa Manispaa ya Iringa na maeneo yanayozunguka Manispaa hiyo. 

Kliniki hiyo itazinduliwa tarehe 10/11/2016 na itaendelea kwa siku tano mfululizo hadi tarehe 14/11/2016 siku mbayo ni kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kisukari Duniani.

Akizungumza na SIMBAYABLOG leo (Jumatano) Afisa wa Habari Mkoa wa Iringa Dennis Gondwe, alisema huduma za upimaji zitafanyika katika Bustani ya Manispaa ya Iringa kuanzia saa 2:00 Asubuhi hadi saa 10.30 Jioni kila siku, na kuongeza kuwa huduma zote zitatolewa bure.

Siku ya Kisukari Duniani ilianzishwa mwaka 1991 na Mashirika mawili ya kimataifa yaani World Health Organization (WHO) na International Diabetes Federation (IDF) baada ya kuona ugonjwa wa Kisukari unaongezeka sana Duniani na Siku hiyo huadhimishwa Duniani kote kila mwaka ifikao tarehe 14 Novemba. 

Alisema kuwa Mkoa wa Iringa kama maeneo mengine Duniani unaadhimisha siku hii, kwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kupima wananchi wake ili waweze kufahamu hali zao na pia kutoa elimu ya umuhimu wa kuzuia na kujikinga na madhara yatokanayo na ugonjwa wa kisukari.

Ugonjwa wa Kisukari ni hali ambayo hutokea wakati sukari katika damu inapokuwa nyingi kupita kiwango cha kawaida kwa muda mrefu. 

Sukari hutumiwa na mwili ili kupata nishati lishe. Ili mwili uweze kutumia sukari inayotokana na vyakula, unahitaji kichocheo cha insulin. 

Insulin husaidia sukari kuingia kwenye chembechembe hai ili kutengeneza nishati lishe. Ugonjwa wa kisukari unasababishwa na kichocheo hiki kupungua au kutofanya kazi kama inavyotakiwa.

Hivyo kiwango cha kisukari kinabaki kikubwa kwenye damu kwa sababu sukari haikuwezeshwa kuingia kwenye chembechembe hai za mwili.


“Mara nyingi, watu wengi hawajitambui kuwa wana ugonjwa huu. Wengine wanakuwa na dalili lakini hawachukui hatua mapema,” alisema Gondwe. 

Alisema kuwa dalili za kisukari ni rahisi kuzitambua. Dalili hizo ni: kiu isiyoisha, kukojoa mara kwa mara, kupungua uzito, kusikia njaa kila wakati na mwili kukosa nguvu. Mwananchi yeyote akiwa na dalili hizi aende hospitali au katika kituo cha Afya ukapime sukari. 

Hata hivyo, afisa habari huyo ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Iringa kuzingatia ulaji unaofaa wa vyakula. 

Aliseam kuwa ulaji unaofaa ni kula chakula mchanganyiko cha kukutosha kukua na kuwa na uzito wa kawaida na chenye virutubisho vyote vinavyohitajika mwilini. 

Kwa mfano vyakula vya wanga vinasaidia kuupa mwili nguvu na joto, protini husaidia kujenga mwili na kutengeneza vichocheo mbalimbali, vitamin na madini hulinda mwili dhidi ya magonjwa.

“Wananchi wetu lazima kujiepusha na kula vyakula bila kuzingatia aina na kiasi kulingana na mahitaji ya mwili. Ulaji huu huweza kusababisha kupungua au kuzidi kwa virutubishi mwilini,” aliseam afisa habari huyo.

Ulaji usiofaa ni pamoja na kula vyakula vyenye mafuta mengi hasa yale yatokanayo na wanyama, kula vyakula vyenye chumvi nyingi, sukari nyingi, kula chakula kupita kiasi, kukoboa nafaka na kutokula mbogamboga na matunda kiasi cha kutosha.

Mambo yanayoongeza uwezekano wa kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza ni pamoja na ulaji usiofaa hasa matumizi ya chumvi kwa wingi, mafuta na sukari, uzito uliozidi, unene uliokithiri, kutofanya mazoezi, uvutaji wa sigara na bidhaa zitokanazo na tumbaku, unywaji pombe kupita kiasi na msongo wa mawazo.

Ili kuzuia ugonjwa wa kisukari na maradhi mengine yasiyo ya kuambukiza ni muhimu kufuata kanuni za afya ambazo ni ulaji bora, na mtindo bora wa maisha ambao ukifuatwa vyema huweza kwa kiasi kikubwa kuzuia mtu kupata kisukari au kwa mtu ambaye tayari ana ugonjwa wa kisukari hupunguza uwezekano wa kupata madhara makubwa ya kiafya.


No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...