Moja za kadi za chama zilizochanwa na wapambe wa mbunge Prof. Rapheal Mwalyosi huko Ludewa hivi karibuni.
WANA Chama cha Mapinduzi (CCM) wilayani Ludewa wamesikitishwa na kitendo kilichofanywa na wapambe wa mbunge wa zamani wa Jimbo la Ludewa (CCM) Prof. Raphael Mwalyosi kuchukua kadi zao na kuzichana .
Wapambe hao wanaodaiwa kuchukua kadi za wana CCM na kuzichana ni Boscow Thobias Lingala Lingala,Obote Msemakweli, Aulerian Mhagama (Amca) na Florian Mtweve (Mvanginye) huku kadi za wana CCM hao zilizochanwa ni zile za kata za Ludewa Mjini, Manda na Nkomang’ombe ambao walikuwa wakimpinga Mwalyosi na kumuunga mkono Filikunjombe.
Siku mbili kabla ya kura za maoni wapambe wa Prof. Mwalyosi walikuwa wakienda kwenye zile Kata asizokubalika Profesa wakinunua kadi moja ya CCM kwa shilingi 10,000/= mpaka 20,000/= toka kwa wana CCM na kuzichana ili kuwafanya wanachama hao wasipige kura wakihofia kuwa wakifanya hivyo watawapigia wagombea wengine.
Wakati kadi zilizochanwa Manda zilitupwa chooni kadi zilizochanwa Ludewa Mjini zilitupwa kwenye jalala la kilabu cha Pombe za Kienyeji cha Henry kilichopo Ludewa Mjini.
Blog hii imeviona vipande vipande vya kadi za CCM viingine vikiwa vimeunguzwa na moto jalalani hapo na vingine vikiwa vimetapakaa pembeni ya jalala hilo.
Wagombea wengine walioshiriki kwenye mchakato wa kura za maoni Jimboni Ludewa ni Injinia Zebadiah Chaula, Deo Filikunjombe – Kamanda wa Vijana UVCCM (W) na James Mgaya.
Allen Ngingo, Katibu Kata wa Kata ya Ludewa Mjini ambako kadi za CCM pia zilichanwa amelaani kitendo kilichofanywa na Mbunge huyo wa zamani (Prof. Mwaloysi).
“Hatukutegemea kama Profesa anaweza kuchana kadi za Chama kilichomweka madarakani kwa miaka mitano,” alilalamika Katibu Kata huyo akiongeza kuwa “Sisi tumekitafsiri kitendo hicho kama ni mbinu mahsusi za kutaka kukihujumu Chama Cha Mapinduzi, kwa maslahi binafsi.”
Lakini pia sisi tumesikitishwa zaidi kuona kuwa baadhi ya walioshiriki kuzichana kadi hizo za CCM ni watumishi wa serikali,” alisema kwa uchungu mwana CCM mwingine mkongwe, Andrew Nyilawila, 75. “Sielewi kabisa; mtumishi wa serikali anawezaje kuchana kadi ya chama tawala?” alihoji Bw. Nyilawila.
Katibu wa CCM wa Wilaya ya Ludewa, Mama Magreth Chusi, amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kusema kuwa swala hilo linashughulikiwa kiChama ndani ya CCM na kwamba hatua stahiki zitachukuliwa kwa waliofanya hivyo. “Tumelifikisha swala hilo kwenye vyombo husika,” alisema mama Chusi.
Katibu wa Mkoa wa Iringa, Mary Tesha naye amekiri kuzipokea taarifa za kuchanwa chanwa kwa kadi za CCM jimboni Ludewa.
“Taarifa ambazo nimezipata zimenistua na zimenisonesha sana,” alisema Mary Tesha huku akiongeza kuwa uchunguzi makini unaendelea ili kuwabaini wale waliohusika na vitendo hivyo na kwamba hatua kali zitachukuliwa kwa watakao bainika kuihujumu CCM.
Hata hivyo Prof.Mwalyosi mwenyewe hakuweza kupatikana katika simu yake ili kujibia madai hayo dhidi yake .
Prof. Raphael Mwalyosi alikuwa Mbunge wa Jimbo la Ludewa (CCM) toka mwaka 2005 hadi 2010 amedondoshwa kwenye kura za maoni na mwandishi wa habari, Bw. Deo Filikunjombe aliyepata ushindi wa kura 7175 huku Prof. Mwalyosi Raphael (6,652),James Mgaya (588) na Chaula Daniel (461).
No comments:
Post a Comment