Tuesday, 25 January 2011

UGONJWA WA KUANGUKA KIFAFA

Naam! Mpendwa msomaji wa blog yangu hii habari za saa hizi, nimatumaini yangu u mzima wa afya njema. Napenda kutumia nafasi hii kukupatia japo kidogo habari ya ugonjwa wa kuanguka kifafa.

Inakadiliwa kuwa kwenye nchi zinazoendelea asilimia moja ya watu wake wana ugonjwa wa kuanguka kifafa. Kati ya watu hao nusu yao ni watoto na hali hiyo inaweza kudumu maisha kama haikutibiwa.

Kwenye nchi hizi wagonjwa wa kuanguka kifafa hudhalilishwa na hivyo kutengwa na jamii kwani ugonjwa huu hudhaniwa kuwa ni wa kuambukizwa.

Kwa hiyo wagojwa hawa hula na kucheza peke yao na hivyo hawaruhusiwi kujiunga na wenzao katika kazi na shughuli nyingine za kijamii ingawa akili zao mara nyingi zipo sawa kabisa.

Hivyo baada ya kusoma makala haya utaweza kuelewa baadhi ya mambo muhimu kuhusu ugonjwa wa kuanguka kifafa na kwamba ugonjwa huu HAUAMBUKIZI.

UGONJWA WA KUANGUKA KIFAFA NI NINI?

Ugonjwa wa kuanguka kifafa ni ugonjwa unaoathiri ubongo. Ugonjwa huu huwakumba watu wa aina na mataifa yote hapa ulimwenguni bila kujali dini, rangi, kabila au kiwango cha elimu yao.

Hali ya kuanguka kifafa inaweza ikaanza wakati wowote, lakini mara nyingi hujitokeza wakati wa utotoni. Mtu aliyepatwa na ugonjwa huu huanguka na kujitupatupa kiwiliwili chake, kujiuma ulimi, na hatimaye kupoteza fahamu. Akiwa amepoteza fahamu anaweza kujikojolea pia.

Ni vyema kuelewa pia kuwa mtu mwenye kuanguka kifafa hawezi kuambukiza mtu mwingine ugonjwa huu kwa njia ya:

a. Kutoa ushuzi

b. Pumzi

c. Mkojo

d. Haja kubwa

e. Kugusana

f. Jasho

g. Kutumia vyombo vya chakula pamoja.

KUANGUKA KIFAFA KUNASABAIBISHWA NA NINI?

Sababu kuu za kupatwa na ugonjwa wa kuanguka kifafa ni kupata;

: athari kwenye ubongo wakati mama anapokuwa na uzazi wa matatizo au uzazi wa muda mrefu,

: magonjwa yanayaoathiri ubongo kama vile malaria na ugonjwa wa uti wa mgongo,

: majeraha kichwani yanayotokana na ajali ya gari, kupigwa, matumizi ya Pombe kali kwa muda mrefu au uvimbe kwenye ubongo.

MATIBABU YA UGONJWA WA KUANGUKA KIFAFA

Ugonjwa wa kuanguka kifafa unatibika ili mradi tu mgonjwa anafuata maagizo ya matumizi ya dawa kama anavyoelekezwa na mganga wake. Kuna dawa nyingi zinazotumika kutibu ugonjwa huu, kati ya hizo ni ‘Phenobarbitone’na ‘Phenytoin’ Iwapo mgonjwa ataandikiwa mojawapo ya dawa hizi ni lazima zimezwe kufuatana na maagizo ya Mganga na kwa kufanya hivyo tu ndipo vipindi vya kuanguka vitapungua.

KUMBUKA: MTU MWENYE KUANGUKA KIFAFA SIYO MGONJWA WA AKILI, MHALIFU, KWAMBA ANA MASHETANI AU MWAMBUKIZAJI.

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...