Tuesday, 17 May 2011

RAIS KIKWETE MGENI RASMI KATIKA KUMSIMIKA ASKOFU NDIMBO

ASKOFU MTEULE WA JIMBO LA MBINGA
MHASHAMU JOHN C. NDIMBO





RAIS Jakaya Mrisho Kikwete anatarajia kuwa mgeni rasmi katika sherehe za kumsimika Askofu Mpya wa Pili wa Jimbo Katoliki la Mbinga mkoani Ruvuma hapo tarehe 05.06.2011. Aidha, Ibada ya kuwekwa wakfu Askofu huyo itaongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Da es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Akiongea na Blog ya http://www.fridaysimbaya.blogspot.com/ leo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Jimbo la Mbinga Pd. Jospeh Mwingira amesema kuwa Rais Kikwete ndiye atakuwa mgeni rasmi katika sherehe za kumsimika rasmi na kuweka wakfu Askofu Mteule wa Jimbo la Mbinga, Mhashamu John Chrisostom Ndimbo.

Jimbo Katoliki la Mbinga limepata Askofu Mpya aliyeteuliwa na Baba Mtakatifu Benedikto XVI kuwa Askofu wa Pili wa Jimbo hilo. Mwashamu Askofu John Ndimbo aliteuliwa na Baba Mtakatifu Benedikto XVI kuwa Askofu wa pili wa Jimbo Katoliki la Mbinga hapo tarehe 12 Machi, 2011.
Uteuzi huo umefuatia kustaafu kisheria kwa Mhashamu Askofu Emmanuel Mapunda aliyeliongoza jimbo hilo kwa miaka 21 mpaka sasa. Mhashamu Askofu Emmanuel Mapunda amefikisha umri wa miaka 75 ambayo kwa taratibu na sheria za Kanisa Katoliki, maaskofu wake wafikapo umri huo wanapaswa kustaafu majukumu ya kuliongoza jimbo.

Askofu Mapunda alifikisha umri huo tarehe 10. 12. 2010. Baada ya kupeleka maombi ya kustaafu kwa mkubwa wake Papa Benedikto XVI, Askofu huyo alikubaliwa na kuomba aendelee kusimamia Jimbo la Mbinga hadi hapo Askofu mpya atakapoteuliwa.
Askofu Jonh C. Ndimbo alizaliwa tarehe 12. 10. 1960 huko Kipololo katika Parokia ya Lundamato Jimbo la Mbinga. Wazazi wake walikuwa Chrisostom Ndimbo na Fransiska Ndunguru. Ubatizo alipata tarehe 13.11 1960 na kipaimara tarhe 29.10. 1972.

Shule ya msingi alisomo huko Kipololo katika Porakia ya Lundamato la Jimbo la Mbinga, kwa darasa la kwanza hadi nne mwaka 1969 hadi 1972. Masomo ya darasa la tano hadi saba alisoma huko Hanga Seminari katika Jimbo Kuu la Songea kuanzia mwaka 1973 hadi 1975.

Masomo ya sekondari alisoma katika Seminari za Likonde katika Jimbo la Mbinga (wakati huo lilikuwa Jimbo la Songea) na Nyegezi katika Jimbo la Mwanza. Kidato cha kwanza hadi cha nne mwaka 1976 hadi 1979 huko Likonde. Kidato cha tano hadi cha sita mwaka 1980 hadi 1981 huko Nyegezi.

Pia alipata mafunzo ya kijeshi huko Urujoro-Arusha maka 1982. Kisha aliendelea na malezi na kozi ya upadre katika Seminari Kuu Peramiho. Falsafa alisoma mwaka 1983 hadi 1985 na teolojia mwaka 1986 mpaka 1989. Alipewa Daraja Takatifu la Ushemasi Juni 1988 na upadre 21.06. 1989 huko Mbinga na Mhashamu Askofu Emmanuel A. Mapunda wa Jimbo la Mbinga. Yeye ni miongoni mwa mapadre sita (6) waliopadrishwa mwaka huo jimboni Mbinga.

Baada ya upadrisho Pd. John Ndimbo alitumwa seminari ya Likonde kuwa mwalimu na mlezi wa waseminari. Mwaka 1990 alipelekwa Ufilipino kwa masomo ya juu ambako alipata shahada ya kwanza na ya pili katika masomo ya sayansi na utawala wa elimu. Vyuo alivyosoma ni Rigina Carm Katikaeli kilichopo katika jiji la Manila na cha DE LA SALLE hapa hapo Manila. Alihitimu masomo hayo mwaka 1994 na kurudi jimboni Mbinga.

Tarehe 8 Septemba 1994 aliteuliwa na Mhashamu Askofu Emmanuel Mapunda kuwa Gombera wa seminari Likonde wadhifa aliodumu nao mpaka tarehe 28. 09.2010 alipoacha kufuatia kuteuliwa kwake kuwa Katibu Mtendaji wa Idara ya Elimu ya Baraza la Maaskofu Tanzania tarehe 3 Agosti 2010.

Mhashamu Askofu John Ndimbo ni Askofu pacha wa Mhashamu Askofu Bernadine Mfumbusa wa Jimbo Katoliki la Kondoa katika Mkoa wa Dodoma. Kwani, siku alipoteuliwa na kutangazwa Askofu John Ndimbo wa Jimbo la Mbinga, tarehe 12 Machi, 2010, Baba Mtakatifu Benedikto XVI alianzisha Jimbo la jipya la Kondoa lililozaliwa kutoka Jimbo la Katoliki la Dodoma. Kisha akamteua Pd. Bernadine Mfumbusa, ambaye alikuwa makamu  mkuu wa taaluma katika chuo kikuu cha Kanisa Katoliki cha Mt. Augustino (SAUTI) Mwanza .

“Jimbo jipya la Kondoa lina eneo la kilometa za mraba 13, 210, watu 541,345, wakatoliki 46,067, mapadre 17, watawa 87. kumbe, Jimbo Katoliki la Mbinga ambalo lina milikiwa na Mhashamu Askofu John Ndimbo lina eneo la kilometa za mraba 11, 400, watu 532,019, wakatoliki 418,000, mapadre 69 na watawa 270,” sehemu ya taarifa inaelezea.

Uteuzi wa maaskofu hawa umepokelewa na wakristo na Watanzaia kwa ujumla kwa hisia za pekee na tofauti. Kundi kubwa la watu linasifu na kupongeza uteuzi wao, lakini wengine wanaonja kwa karibu sana pengo waliloacha katika nafasi zao walizoziacaha. Wote hao wamekuwa katika nafasi za juu na nyeti za kitaaluma katika Kanisa letu.

Mhashamu John Ndimbo alikuwa Katibu Mtendaji wa Idara ya Elimu TEC baada ya kushughulika na taaluma kwa miaka 22 katika seminari Likonde, hivyo kwa uhakika ana mang’amuzi na uzoefu wakutosha.

Mhashamu Askofu Mfumbusa amekuwa makamu wa mkuu wa taaluma katika chuo cha SAUTI-Mwanza na mhadhiri nguri wanafunzi wa kozi ya uandshi wa habari. Hapo alikuwa mhimili mkubwa wa taaluma ya mwasiliano.

Wahashamu maaskofu Benedine Mfumbusa na John Ndimbo walikula kiapo cha utii na kukiri kanuni ya Imani kwa kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki Papa Benedikto XVI huko Roma katika Kikanisa cha mweyeheri Kardinali Henry Newman hapo tarehe 4 Aprili, 2011. Katika nafasi hiyo walikabidhiwa vitendea kazi vya kiaskofu.

"Tunawatakia maaskofu wetu hawa amani, baraka na nguvu katika wajibu huo mpya. Mungu aandamane nao daima."



No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...