Saturday, 1 October 2011

Waijua Yubilei ya Dhahabu?




Na Gustav Chahe, Tanga
YUBILEI YA DHAHABU inatarajiwa kuadhimishwa katika Paroki ya Mt. Theresia Barabara ya 20 katika Jimbo Katoliki la Tanga.
Adhimisho hilo linakuja baada ya kukamilika kwa mchakato wa maandalizi na mafanikio ya utaratibu wa kukusanya maoni ya waamini na kuyaweka mazingira katika hali nzuri.
Katibu wa Parokia hiyo Bw. Costantino Mwanga ameeleza kuwa adhimisho hilo litakuwa ni la pekee tofauti na maadhimisho mengine ukilinganisha na menginre yaliyokwisha kupita hata kutokana na mazingira yenyewe yalivyo.
Akifafanua maana ya Yubilei ya Dhahabu, Bw. Mwanga ameeleza kuwa wameamua kuita hivyo kutokana na tendo hilo kuadhimishwa kwa mara ya kwanza katika Parokia hiyo na pili kutokana na kuadhimishwa katika mwaka wa maadhimisho ya yubilei ya miaka 50 ya uhuru wa Taifa.
“Tumeiita YUBILEI YA DHAHABU kwa sababu ya: kwanza, hatujawahi kuadhimisha Yubilei ya miaka 25 ya Parokia hii kama wanavyofanya wengine; hii ni mara ya kwanza kufanya hivyo na pili tumeangalia suala zima na maadhimisho haya kwa kuwa yanakwenda sambamba na maadhimisho ya Yubilei ya miaka 50 ya Uhuru wan chi yetu. Hii ni fahari kubwa ambayo imetufanya tiite kwa jina hilo” anaeleza Bw. Mwanga.
Ili kufanikisha maadhimisho kama hayo, suala la ushirikiano na mshikamano ni la muhimu. Imeelezwa kuwa bila kujali umri na uwezo wa wadau, michango mbalimbali ya hali na mali imekuwa ikipokelewa ikiwa ni pamoja na mawazo na ushauri mbalimbali uliokuwa ukitolewa kwa mijadala ya pamoja.
“Tunachojivunia ndugu mwandishi ni kuwa na ushirikiano. Suala hii si rahisi akafanya mtu mmoja kwani ni gumu wala mawazo ya mtu mmoja hayawezi kufanikisha tukio hili bali mawazo ya watu na michango yao ndiyo mhimili wa mafanikio vinginevyo ni sawa na kutwanga pilipili mshahara kukohoa” anaeleza na kuongeza kuwa “ushirikiano baina ya sisi viongozi na waamini, viongozi na mapadre pamoja na waamini na mapadre ni mzuri ndiyo maana imekuwa ni rahisi kwetu sisi kupata mafanikio haya”.
Parokia inapoendelea kuadhimisha Yubilei hiyo imeonekana kukabiliana na changamoto mbalimbali pamoja na kuwa na mafanikio mengi ambayo yanatokana na ubunifu wa vyanzo vya mapato na matunda ya uvumilivu katika kumtegemea Mungu.
Akizungumza na mwandishi wa makala haya mweka hazina wa Parokia hiyo Bw. Marucus Msekefu amevitaya vyanzo vya mapatoika Parokia hiyo kuwa ni Misaada mbalimbali wanayojitoa waamini, Sadaka na mavuno, kupitia mchango wa kulitegemeza jimbo, michango ya hiari kulingana na mtu anavyojisikia kutoa”. Anaeleza.
Pamoja na vyanzo hivyo, Parokia inatarajia kutumia zaidi ya shilingi 100 milioni katika ujenzi wa ukumbi na hosteli ambavyo ni vyanzo vya mapato.
“Tupo katika ujenzi wa hosteli na ukumbi kwa ajili ya mapato ya Parokia yetu ambapo tunatarajia kutumia zaidi ya shilingi milioni 100” anaeleza Bw. Msekefu na kuongeza kuwa “hii ni matokeo ya jitihada za waamini kwa kutoa michango yao ya hali na mali kwa ajili ya ujenzi huu”.
Hosteli hiyo ina vumba 9 ambapo itakapokamilika inatarajia kubeba watu 6 hadi 8 kwa kila chumba na ukumbi unatarajia kubeba watu wasiopungua 200, shule ya chekechea pamoja na kiwanja kikubwa ambacho kinatarajiwa kujengwa hosteli kubwa itakayobeaba watu wengi zaidi.
Yubilei hiyo ambayo kilele chake ni Oktoba 2, mwaka huu itatanguliwa na  matukio mbalimbali ambapo Mhashamu Baba Askofu Anthony Banzi wa Jimbo hilo anatarajiwa kufungua shule ya awali Marungu, kufungua Golota la B. Maria Marungu, ufunguzi wa Kanisa la Marungu ambako huko atatoa Sakramenti ya Kipaimara na Ndoa ambayo hayo yatafanyika Septemba 30 mwaka huu.
Oktoba 1, Mhashamu Baba Askofu Banzi anatarajiwa kuweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa katika kigango cha Duga kilichop ndani ya Parokia hiyo pamoja na kufanya ufunguzi wa ukumbi na hosteli parokiani hapo.
Siku ya kilele chenyewe, Mhashamu Baba Askofu Banzi atatoa Sakramenti ya Kipaimara, Sakramenti ya Ndoa kwa watu mbalimbali wakiwemo walioishi katika umba sugu pamoja na kuwaombea waliotimiza Yubilei ya miaka 50 ya ndoa.
Licha ya kuwepo kwa mafanikio katika Parokia hiyo, imeelezwa kuwa kuna changamoto mbalimbali zinazoikabili katika kaziya uinjilishaji ambazo zinatoa fursa kwa waamini hao na uongozi kukabiliana nazo kwa nguvu zote bila kuchoka.
Akizungumza na mwandishi wa makala haya parokiani hapo, mwenyekiti wa Parokia hiyo Bw. Karol Makungu anaeleza kuwa zipo changamoto mbalimbali zinazoweza kukwamisha uinjilisha katika parokia hususani katika jimbo zima.
“Tusiseme tuna mafanikio pekee yake bali tunakabiliana na changamoto mbalimbali ambazo bila ya kupambana nazo kwa uvumilivu, uinjilshaji unaweza ukayumba” anasema na Bw. Makungu na kuongeza kuwa “changamoto kubwa ni kujitokeza kwa wale wasiomjua Kristo na kutaka kutuvuruga lakini kwa pamoja tunasimama na kumtukuza Kristo kwa nguvu zote ili hata wale ambao bado kwao ni msamiati, wapate kumjua na baadaye waweze kumkiri ya kuwa Kristo ni Bwana na mwokozi wa maisha yao”.
Hata hivyo, akizungumzia suala la Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo Bw. Mwanga anaeleza kuwa kunamafanikio ingawa zipo changamoto ambazo kama zingezingatiwa lisinkuwa ni tatizo sana.
“Kwa upandea wa Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo, kuna changamoto lakini kubwa zaidi inatokana na akina Baba kutohudhuria kwa sababu za kusema kuwa wamebanwa na majukumu ya utafutaji lakini kama hili lingezingatiwa na wakaweza kujitoa kwa wingi basi, tunaweza tukalimaliza lakini akina Baba ndio ambao kwenye Jumuiya hawaonekani”. Anaeleza.
Kwa upande wa uhai wa vyama vya kitume pia nako hakusita kuzungumza kwa kile alichosema uhai upo wa kuridhisha na kuwataka waamini kuimarisha mshikamano, upendo na uadilifu katika kumtumikia Mungu,
“Ndugu mwandishi, kwa upande wa vyama vya kitume kwa ujumla kuna uhai unaoridhisha na labda ambacho ningeweza kusema, ni kwamba wasikate tamaa bali waendelee kudumisha upendo, mshikamano bila kusahau matendo ya huruma kwa kila mtu bila kujali itikadi mbalimbali na madhehebu au dini” anaeleza.
Wakati huo huo Makamu mwenyekiti wa Parokia hiyo Bw. Feddy Rocky amewakumbusha waamini kuwa katika mapambano dhiti ya wokovu hakuna kulala wala hakuna kujisahau kwani shetani anaweza akawateka.
“Mimi ninachoweza kusema ni kwamba, katika mapambano ya wokovu tusijisahau kwani mwovu shetani anaweza akatuteka ila wakumbuke kuwa kanisa litajengwa na sisi wenyewe wala katika miaka ya leo tusitegemee watu kutoka nje kuwa watalijenga Kanisa letu; kazi kubwa imebaki mikoni mwetu hawawezi kurudi tena kuja kutujengea, tujitoe kwa moyo wetu wote kwa hali na mali ili tuweze kujenga Kanisa letu” anaeleza Bw. Rocky
Mbali na adhimisho la yubilei hiyo, siku hiyo kutakuwa na uzinduzi wa albam ya Kwaya ya Mt. Alois Gonzaga yenye jina la “TUISHI KAMA NDUGU” yenye jumla ya nyimbo 10.
Parokia ya Mt. Teresia ina jumla ya vigango 10 ambavyo ni Kigango Mama, Kigombe Bago, Marungu, Mapojoni, Mbuyukenda, Kirare Korosini na vingine ni Kirare Bango, Mgwisha, Neema pamoja na kigango cha Duga ambapo kila kigango kina makatekista wakutosha.
Parokia imefanikiwa kuto Padre mmoja mwaka 2007 ambaye ni Pd. Augustino Temu pamoja na masista 2 ambao ni Sr. Aristidia Mchunguzi na Sr. Sara Mpera
Parokia ya Mt. Teresia Ngamiani Tanga ilianzishwa mwaka 1961 chini ya mapadre wa misionari Warosmini ambapo awali kilikuwa kigango mojawapo cha Parokia ya Mt. Anthony Chumbageni.
                     



No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...