Thursday, 22 November 2012

ZAIDI YA WAGONJWA 80 WAMEPATIKANA NA MTOTO WA JICHO MKOANI RUVUMA

Na Friday Simbaya, Songea


Hospitali ya Peramiho ya Mt. Josefu kwa kushirikiana na daktari bingwa wa macho Dr. Grasbon toka Ujerumani waliendesha kambi ndogo ya macho, ambapo ilianza tarehe 5-12/11/2012.

Kambi hiyo ya macho ilifanikiwa kuona wagonjwa zaidi ya 120 toka sehemu mbalimbali ya Mkoa wa Ruvuma, ambapo wagonjwa 80 walipatikana na ugonjwa wa mtoto wa jicho (Cataract).

Akizungumza na Gazeti la Mwenge hivi karibuni Dr. Wade Kabuka ambaye ni daktari wa macho katika Hospitali ya Peramiho, amesema tatizo la macho katika mkoa wa Ruvuma lipo na wagonjwa ni wengi.

Amesema kuwa wakati wakiendesha kambi ya upimaji wa macho kwa ufadhili wa hospitali ya Peramiho kwa kushirikiana na Dr. Grasbon toka Ujerumani, wagonjwa waliojitokeza ni wengi sana, na wengi wao walikuwa na matatizo ya mtoto wa jicho.

Amesema kuwa zaidi ya wagonjwa 120 walipimwa na kati yao 80 waligundulika na tatizo la mtoto wa jicho (Cataract), ambapo wote walipata matibabu kwa kuwekewa kioo ndani ya jicho.

“Ugonjwa huu wa mtoto wa jicho mara nyingi unawapata watu wenye umri mkubwa kuanzia miaka 40 na kuendelea. Kama unavyojua jicho ni kiungo kama viungo vingine mwilini, linapitia ‘ageing process’ yaani na lenyewe linazeeka, lakini ugonjwa huu wa mtoto wa jicho unatibika ukiwahi hospitalini,” amesema Dr. Kabuka.

Changamoto

Dr. Kabuka amesema kuwa wakati wa kuendesha operesheni za macho zilijitokeza changamoto nyingi kama vile uwepo wa wagonjwa wengi na kuwepo kwa imani potofu katika jamii.

Wananchi wengi wanakuwa na imani potofu ya kuwa wazee wanapokuwa na matatizo ya mtoto wa jicho, jamii huwatenga watu hao kwa kudhani kuwa ni wachawi.

Changamoto nyingine kwamba wagonjwa wengi wa mtoto wa jicho ni watu wenye umri mkubwa na wengi wanaishi vijijini ambako hali zao kiuchumi ni duni. Kwa hivyo mara nyingi wazee hao wanashindwa kufika hospitali kutibiwa kutokana na hali duni ya maisha.

Kwa mfano, upasuaji wa jicho moja ni shilingi 50,000/- na kwa macho mawili ni shilingi laki moja.

“Wagonjwa wengi wenye matatizo kama hayo wenye kipato cha chini wanakosa kufika hospitali kupata matibabu kutokana na gharama. Tatizo lingine linalofanya ugonjwa huu uenee ni imani potofu katika jamii kuhusu ugonjwa wa mtoto wa jicho kwa wazee. Mara nyingi jamii huwatenga wazee kwa kudhani ni wachawi na pengine wamekula watoto wao kwa uchawi na kupelekea kutengwa,” ameelezea Dr. Kabuka.

Ni nini kifanyike?

Ili kupunguza tatizo la ugonjwa wa mtoto wa jicho na magonjwa mengine ya macho serikali hainabudi kupeleka elimu ya afya ya macho kwa jamii.

Serikali pia isomeshe wataalamu wengi zaidi wa macho na ikiwezekana wapatikane hadi ngazi za wilaya.

Hali ya Upofu Tanzania

Kulingana na takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za hivi karibuni, Tanzania inakadiriwa kuwa na watu 992,250 sawa na asilimia 3.15 wenye matatizo ya kuona ambapo kati yao wasioona ni 315,000 sawa na asilimia 0.7. Watu wenye uoni hafifu wanakadiriwa kuwa 787, 5000.

Sababu kubwa zinazosababisha upofu unaoweza kuzuilika hapa nchini na duniani kwa ujumla ni mtoto wa jicho (Cataract) na shinikizo la maji ya jicho (Glaucoma).

Nchini Tanzania huduma za macho zinapatikana katika hospitali zote za wilaya, hospitali zote za rufaa za mikoa, hospitali za rufaa, Hospitali ya Taifa Muhumbili na Hospitali Maalum ya CCBRT.

Aidha, kila wilaya na mikoa wapo waratibu wa huduma za macho kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

Katika hospitali nyingi za wilaya, pamoja na kuwa waratibu wa huduma za macho lakini upausaji wa macho hususani mtoto wa jicho haufanyiki.

Hivyo, kuna umuhimu wa kufundisha wataalamu wengi wenye uwezo wa kufanya upasuaji wa magonjwa ya macho katika ngazi ya wilaya.

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...