Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Sarah Dumba |
CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya Njombe kimeitaka
serikali kusitisha biashara huria ya vitabu vya kiada kwa kile walichoeleza
kwamba vinakinza na kuwapa ugumu katika ufundishaji.
Ombi hilo lilitolewa hivi karibuni wakati chama hicho
kikiadhimisha siku ya walimu iliyofanyika mjini Makambako, wilayani humo.
“Kama ikishindwa kusitisha, tunashauri kabla vitabu hivyo
havijaingizwa sokoni, serikali ifanye utaratibu wa kubihariri na kuvigonga
mihuri maalumu ili kuwahakikishia walimu kwamba vimethibitishwa,” alisema
Katibu wa CWT Njombe, Salama Lupenza.
Aidha chama hicho kimeita serikali kufanya tafiti za kutosha
katika miradi yake ukiwemo mpango wa matokeo makubwa sasa (BRN) unaolalamikiwa
kuwazidishia mzigo wa uwajibikaji bila nyongeza ya marupurupu.
Lupenza alisema pamoja na mpango huo kuanza kuongeza tija katika sekta mbalimbali za kimaendeleo, hali ya walimu imeendelea kuwa vile vile.
“Tunasikitishwa sana, pamoja na mafanikio ya BRN, hakuna
chochote kinachofanywa na serikali kuboresha maslai ya mwalimu,” alisema.
Kwasababu serikali haizifanyii kazi kwa wakati kero
mbalimbali zinazowasibu, Lupenza alisema katika maeneo mbalimbali nchini walimu
wanapoteza hali ya kuipenda kazi hiyo na kuifanya kwa nguvu zao zote jambo
linaloweza kuhatarisha zaidi maendeleo ya sekta hiyo.
“Kwa upande wa sekta yetu hii ya elimu, BRN inaonekana
kumjali zaidi mwanafunzi lakini inamsahau mwalimu mwenye wajibu mkubwa wa
kumuwezesha mwanafunzi kufikia mafanikio yake,” alisema.
Alisema tofauti na miaka ya nyuma ambapo kazi ya ualimu
ilikuwa na hadhi kubwa mbele ya jamii, hivisasa hali hiyo haipo tena kwani
ualimu imekuwa ni kazi inayodharauliwa na wengi. (bongoleaks)
No comments:
Post a Comment