Friday, 3 October 2014

Tahliso:TCU simamieni majukumu yenu vizuri



Ofisa Habari wa Taasisi ya Vyuo vya Elimu ya Juu Tanzania (Tahliso), , Andrew Mwakalobo.PICHA: OMAR FUNGO

Jumuiya ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu (Tahliso) wameitaka Tume  ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kusimamia majukumu yake vizuri kwa vyuo ambavyo vinaongeza ada kinyume cha utaratibu.


Wamevitaja baadhi ya vyuo hvyo kuwa ni KCMC, CUHAS-Bugando na St. Francis Ifakara. Pia, Tahliso wameitaka TCU kuacha kuwatoza wanafunzi wa elimu ya juu Sh. 20,000 ikiwa ni mchango wa ‘Quality Assurance fee’ kwa madai ya kuendesha shughuli za TCU.

Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa Tahliso, Musa Mdede, alipozungumza kuhusu maazimio ya mkutano mkuu uliofanyika Septemba 25 hadi 27, mwaka huu mkoani Iringa. Alisema kumekuwa na malalamiko ya ongezeko la ada hadi kufikia Sh. milioni tano kutoka Sh. milioni tatu.

“TCU imekuwa haizungumzii au kuchukua hatua juu ya suala hili, kuna wanafunzi ambao wameshindwa kuendelea na masomo, tunatengeneza Taifa la wasio na elimu na kisha umasikini,” alisema Mdede.

Aliongeza kuwa mikopo inayotolewa na serikali ni asilimia 40 badala ya 100 kwa wanafunzi wa vyuo vikuu binafsi hususan fani ya afya na kusema vyuo vingi kwa upande wa ada na michango wanahitajika kulipa ada ya Sh. milioni tano hadi sita.

Hata hivyo Mdede alizungumzia utoaji wa mikopo kuzingatiwa pia na kwa wanafunzi wa elimu ya kati yaani Stashahada kutokana na wanaosoma katika fani ya uuguzi, udaktari, ufamasia, ugavi ndiyo wanaofanya kazi  pembezoni mwa nchi.

Tahliso imeitaka serikali kutoa kipaumbele kwa mikopo ya wanafunzi wa fani zote wa elimu ya juu kutokana na nchi kuhitaji wataalam wa nyanja zote. Kwa mujibu wa TCU, jumla ya waombaji mkopo ni 58,037 na bajeti ya serikali ilikuwa ni kutoa mkopo kwa wanafunzi 30,000 tu.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...