Na Frank Mvungi-MAELEZO
Serikali imesema itaendelea kuboresha huduma za afya hapa nchini kuanzia ngazi ya Zahanati hadi Hosipitali za Rufaa zote nchini ili kuhakikisha wananchi wanapata matatibu bora na yanayoridhisha.
Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni jijini Dar es salaam na Makamu wa Rais Dkt. Mohamed Gharib Bilali wakati akifungua Kongamano la wadau wa Afya nchini.
Amesema kuwa Serikali inayo dhamira ya dhati katika kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapata huduma bora za afya ili apate muda mzuri wa kuchangia shughuli nyingine za maendeleo akiwa mzima.
Dkt. Bilali ameongeza kuwa Serikali itaendelea kutoa motisha kwa watumishi wa Sekta ya afya ili waendelee kutoa huduma bora za afya kwa wananchi.
Kwa upande wake Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Seif Rashid amesema Tanzania ni moja kati ya nchi nne barani Afrika zilizoweza kufikia lengo namba 4 la malengo ya millennia katika utoaji wa huduma bora za afya.
Amesema kuwa hatua imefikiwa baada ya Wizara hiyo kuamua kuanzisha idara maalum itakayohusika kuangalia ubora wa huduma zinazotolewa hapa nchini ili kuongeza tija katika Sekta ya Afya kwa kuwapa Wananchi huduma bora zinazokidhi vigezo.
Ameongeza kuwa kwa wale wanaofanya vizuri katika kutoa huduma za Afya watatambuliwa kwa mchango wao katika kutoa huduma bora.
Dkt. Rashid ametaja vigezo vinavyotumika katika kuwapata watoa huduma za afya kuwa ni kutoa huduma inavyotakiwa, kutumia utaalamu sahihi katika kutoa huduma hiyo na kuzingatia viwango vilivyowekwa katika kutoa huduma za afya.
Aidha Dkt. Rashid ametoa wito kwa wananchi kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ili waweze kunufaika na huduma zinazotolewa kupitia mfuko huo kwa lengo la kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za afya.
Kongamano la wadau wa Sekta ya Afya limehusisha wadau zaidi ya 300 kutoka katika Taasisi mbalimbali za Serikali na zisizo za Kiserikali na linafanyika kwa muda wa siku mbili ambapo baadhi ya wadau walitambuliwa kwa kutoa huduma bora za Afya ni kama vile Hosipitali ya Rufaa Mbeya,KCMC, na Bugando.
No comments:
Post a Comment