Sunday, 9 November 2014

Wakulima wa miti waaswa kutokuvuna miti kabla ya kukomaa






Mwakilishi wa Balozi wa Finland nchini Tanzania, Mikko Leppanen na Naibu wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Mahmoud Mgimwa (MB) wakizindua rasmi kwa pamoja programu ya panda miti kiabiashara mjini Njombe. (Picha na Friday Simbaya)

Na Friday Simbaya, NJOMBE

Mwakilishi wa Balozi wa Finland nchini Tanzania, Mikko Leppanen aliwatoa wasiwasi wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya kupanda miti katika nyanda za juu kusini kutoogopa kuhusu kupoteza ardhi yao ya kilimo kwa kupanda miti.


Alisema kuwa kuna haja ya kuwaelimisha wananchi juu ya faida za misitu ili waweze kuondokana na hofu juu ya  kupoteza ardhi yao ya kilimo kwa kupanda miti katika Nyanda za juu kusini.

Leppanen alitoa kauli hiyo Alhamisi wiki iliyopita wakati wa uzinduzi rasmi wa program ya panda miti kibiashara (PFP) uliyofanyika mkoani Njombe.

Alisema kuwa Tanzania ina maeneo mengi yanayofaa kwa kuanzisha mashamba makubwa ya misitu ikilinganishwa na Finland lakini kinachohitajika ni kuhamasisha watu kuanzisha mashamba ya misitu zaidi.

Alisema kuwa Tanzania ina sera nzuri ya misitu ya taifa ya mwaka 1998, lakini kinachohitaji ni kuboresha matumizi ya bora ya ardhi vijijini kama msingi wakusaidia kupunguza migogoro ya ardhi nchini.

Alisema Tanzania ina idadi nzuri ya wakulima wa miti ikilinganishwa na Finland lakini changamoto kubwa ni mpango hafifu wa matumizi bora ya ardhi.

 "Kama mashamba ya misitu yatatumika vizuri yatasaidia kupunguza umaskini na kuboresha maisha yao, alisema."

Programu ya panda miti kibiashara inatekelezwa kwa pamoja na serikali ya Finland kupitia wizara ya mambo ya nje na serikali ya Tanzania kupitia wizara ya maliasili na utalii ambao inatekelezwa katika mikoa ya Iringa, Njombe na Morogoro.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mahmoud Mgimwa (MB) ambaye alikuwa mgeni rasmi wakati wa uzinduzi rasmi program ya PFP, alisema kuwa serikali ya Finland inatoa mchango mkubwa katika kuendeleza misitu ya asili iliyoko katika milima ya Usambara Mashariki.
Alisema kuwa serikali ya Finland ilifadhili uundaji upya wa sera ya taifa ya misitu ya mwaka 1998, sheria ya misitu na program ya taifa ya misitu na nyuki.

“Kweli, tangu wakati huo hadi sasa serikali ya Finland inashirikiana na serikali ya Tanzania katika kutekeleza kwa dhati programu ya taifa ya misitu,” alisema.

Alisema kuwa Finland imekuwa mstari wa mbele kusaidia Tanzania katika programu mbalimbali lakini hasa katika misitu.

Alisema kuwa serikali ya Tanzania na ile ya Finland kwa pamoja wanatekeleza program ya upandaji wa miti  kibiashara katika Nyanda za Juu Kusini hasa katika mikoa ya Njombe, Iringa na wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro kwa sababu watu katika maeneo hayo wana moyo wa kupanda miti tayari.

Hata hivyo, alisema kuwa pamoja kuwepo mafanikio katika upandaji miti katika maeneo ya nyanda za juu kusini, changamoto kubwa ni baadhi ya wananchi kuvuna miti yao kabla ya kufikia umri sahihi wa kuvunwa.

“Huo sio upandaji kibiashara. Nawaasa wananchi kuacha kabisa kufanya hivyo maana ni hasara kwao na hasara kwa mtumiaji wa mbao husika,” alisema naibu waziri maliasili na utalii.

Mkurugenzi wa Programu ya Panda Miti kibiashara (PFP) Dkt. Maria Tham alisema kuna haja ya kuboresha utendaji wa kuchunga, kuvuna na kupanda misitu katika nchi ili kufanya hivyo kwa faida vizazi vijavyo.

 Alisema kuwa uzalishaji misitu ni biashara ya kimataifa na Tanzania  itanufaika na biashara kutokana na utulivu wa kisiasa pamoja na kuwa maeneo mazuri kupanda miti.

Alisema kuwa program ya PFP inalenga katika kuongeza kipato vijijini katika maeneo ya nyanda za juu Kusini baadaye kusababisha kupungua kwa umaskini na kukosekana kwa usawa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Sara Dumba ambaye alikuwa kaimu Mkuu wa Mkoa, alisema Njombe amepanda miche milioni 43 mwaka jana na kushukuru program ya PFP mpango kwa kusaidia kuongeza kasi ya upandaji katika wilaya yake na mkoa kwa ujumla.

Alisema kuwa kabla ya kuja kwa mpango huu katika wilaya yake ilikuwa inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa utaalamu, lakini kwa vileprogramu ya PFP umefika na tatizo litatatuliwa.

Alisema changamoto nyingine ni tatizo la moto na miti kuvuna  mapema kabla ya kukomaa lakini PFP itawawezesha wananchi kuweza kufanya shughuli zingine za kiuchumi wakati wakisubiri miti kukomaa.

"Wakulima mti lazima wa hakikisha kwamba wanatengeneza njia kuzunguka mashamba yao ya miti dhidi ya moto kama njia mojawapo ya kupambana dhidi ya moto katika misitu," alisema.

Alitoa wito kwa wakulima wa miti na wadau wengine katika Mkoa wa Njombe na maeneo mengine kujiunga na vyama vya wakulima wa miti (TGAs) ili serikali iwawezesha

Pia, alitoa wito kwa wananchi kupanda miti kwa wengi iwezekanavyo na kwa ufanisi hivyo kupunguza umaskini wa kipato.

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...