Ndugu Wananchi wa Mkoa wa Iringa
Ninayo heshima kubwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha tuwe na afya njema tokea tulipoanza mwaka 2014. Ni matumaini yangu kuwa Mungu atatuwezesha pia kuumaliza salama mwaka 2014 na hatimae kuuanza mwaka 2015.
Aidha, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru wananchi wote wa Mkoa wa Iringa kwa ushiriki wenu katika shughuli mbalimbali za kujiletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Ndugu Wananchi,
Katika kipindi chote cha mwaka 2014 wananchi wa Mkoa wa Iringa mmekuwa mkifanya kazi kwa kujituma na kwa ushirikiano mkubwa. Ni matumaini yangu kwamba tabia hii ya kufanya kazi kwa kujituma na mshikamano itaendelea Mwaka 2015. Kufanya kazi kwa kujituma na mshikamano kutaleta tija na maendelo ya mwananchi mmoja mmoja na Mkoa wa Iringa kwa ujumla.
Ndugu wananchi;
Msimu wa kilimo tayari umeanza. Nitoe wito kwenu kuzitumia vizuri mvua zinazo endelea kunyesha. Muda huu ni muda muafaka wa kupanda mazao ili kujihakikishia uhakika wa chakula.
Katika maeneo yenye uzoefu wa kupata mvua chache hususani Mahenge, Isimani, pandeni mazao yanayovumilia ukame. Aidha, tukumbuke kupanda miti katika Msimu huu wa mvua kwa kuwa Mkoa wetu unahali ya hewa nzuri inayostawisha miti.
Ndugu wananchi;
Tunapopanda mazao mbalimbali tumieni mbegu bora, mbolea ya kupandia na kukuzia hasa kwa kilimo cha Mahindi na Mpunga ili kupata mazao bora. Wahenga walinena kuwa “Mvua ya kwanza ni mvua ya kupandia”
Ndugu Wananchi; Ulinzi na Usalama
Nawaomba sana ndugu zangu wananchi wa Mkoa wa Iringa, kwa umoja wetu tuhakikishe tunasimamia na kudumisha Ulinzi na Usalama ili Mkoa wetu uendelee kuwa na amani na utulivu. Ni wajibu wetu sote kuhakikisha tunatokomeza kabisa vitendo vyote vinavyopelekea uvunjifu wa amani katika Mkoa wetu wa Iringa na nchi yetu kwa ujumla. Sote tujikite kwenye shughuli za maendeleo na kudumisha umoja. Hali ya usalama ya Mkoa ni shwari na Vyombo vyote vya Dola vitaendelea kuwa makini katika kusimamia amani na utulivu katika Mkoa wa Iringa ili wananchi waweze kushiriki katika shughuli zao za kujiletea maendeleo.
Salamu za Noeli na Mwaka Mpya 2015
Ndugu Wananchi;
Napenda kuwatakia sikukuu njema ya Noeli na Mwaka Mpya 2015 wenye mafanikio tele. Ninawasihi kuhakikisha mnasherehekea sikukuu hizi kwa amani, usalama na utulivu.
Serikali itahakikisha ulinzi na usalama vinakuwepo kipindi chote cha sikukuu kwa sababu uzoefu unaonesha kuwa katika majira ya sikukuu watu wasiopenda kuona amani na utulivu wa Mkoa hutumia majira haya kufanya uhalifu. Ulinzi uanzie ngazi ya kaya, kila mwanafamilia awe makini na kutoa taarifa anapokuwa na wasiwasi na jambo linaloweza kuhatarisha amani na usalama wake na wa Mkoa kwa ujumla.
Wazazi, kipindi hiki cha Sikukuu ni kipindi muafaka cha kukaa na familia kutafakari tulikotoka, tulipo na tunapokwenda. Ni wakati muafaka wa kupanga malengo ya familia na namna ya kuyafikia.
Mwisho,
Mvua zinaendelea kunyesha zimeanza kusababisha maafa, hivyo nawasihi wananchi wote kuchukua tahadhari, hususani wanaoishi mabondeni naomba wahame maeneo hayo.
Ndugu wananchi,
Baada ya kusema haya asanteni kwa kunisikiliza na nawatakia Sikukuu njema ya Chrismas na Mwaka Mpya (2015).
No comments:
Post a Comment