Wednesday, 3 December 2014

SIKU YA WALEMAVU DUNIANI, YAFANA KITAIFA MKOANI IRINGA, WAZIRI MKUU ATOA AHADI


Waziri William Lukuvi akitoa tuzo kwa mmoja wa wakilishi wa taasisi zilizoshirikia maadhimisho ya siku ya walemavu duniani
John Ndumbaro naye akipokea tuzo kwa niaba ya wenzake
Akifurahia tuzo

Mtoto huyu alipokea tuzo na akalambishwa elfu kumi
Amina Molel alipokuwa akizungumzia changamoto za walemavu
Makada wa CCM nao walikuwepo
Nyagawa wa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Iringa naye alipata tuzo
Wakati wakishukuru
Baadhi ya wanafunzi wenye ulemavu walioshiriki maadhimisho hayo
Wengi walikuwepo
Wanafunzi
Kukawa pia na budurani ya mpira wa miguu
Baadhi ya viongozi waliookuwepo wakifuatilia kilichokuwa kikiendelea
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amewaahidi walemavu kuwaondolea vikwazo vinavyowakabili katika suala zima la teknolojia ili waweze kushiriki ipasavyo kwenye masuala mbalimbali ya maendeleo ya uchumi na kijaamii.
Pinda aliyasema hayo kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya watu wenye ulemavu duniani ambayo kitaifa yalifanyika katika viwanja vya Kichangani, mjini Iringa, jana.
Katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera), William Lukuvi, Pinda alisema; “hapa Tanzania ustawi na maslai ya watu wenye ulemavu ndio sera ya serikali yetu kwa miaka mingi.”
Alisema kwa kupitia sheria ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2010, serikali imeweka miongozo ya namna ya kutekeleza na kutoa huduma kwa watu wenye ulemavu.
“Kwahiyo niwaahidi kwamba yapo mambo mengi ambayo serikali imefanya kwa kundi hilo na yako mengi tunayoendelea kuyafanya kwa ajili ya ustawi wao,” alisema.
Katika risala yao iliyosomwa na Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Amina Molel, jumuiya hiyo iliomba sheria ya haki za watu wenye ulemavu ya mwaka 2010 ifanyiwe marekebisho ili kuweza kulipa baraza la taifa la watu wenye ulemavu meno.
“Baraza linataka kuratibu, kusimamia na kutekeleza masuala yetu likiwa chombo huru badala ya kuwa chombo cha ushauri tu chini ya utendaji wa kamishna wa Idara ya Ustawi wa Jamii ambaye kwa nafasi yake ana majukumu mengi,” Molel alisema.
Molel alisema walemavu bado wanakabiliwa na changamoto nyingi lakini akazitaja sita alizosema zinahotaji kuchukuliwa hatua za haraka.
Kwa mujibu wa Molel, changamoto hizo ni pamoja na kutopatikana kwa taarifa muhimu katika mifumo iliyo rafiki kwa watu wenye ulemavu.
“Mfano ni kutokuwepo kwa ukalimani wa lugha ya alama kwenye vipindi vya luninga, mijadala ya vikao vya bunge na hotuba za viongozi mbalimbali,” alisema.
Alizitaja changamoto nyingine kuwa ni pamoja na vyombo vya usafiri vya umma na majengo yanayotoa huduma kwa umma kutozingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu, ruzuku ndogo kwa vyama vya watu wenye ulemavu ambayo kwa miaka mingi hajatolewa na kukosekana kwa uwakilishi katika vyombo vingi vya maamuzi na kisera.
Zingine ni kukosekana kwa ofisi ya kudumu ya shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu na kucheleweshwa utoaji ardhi huko Kibaha Pwani kwa lengo la kujenga chuo cha madereva na ufundi kwa watu wenye ulemavu.
Akiomba serikali izifanyie kazi changamoto hizo, Molel alitoa ombi kwa serikali iwapatie ofisi ya kudumu ya shirikisho lao ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea pindi wafadhili wan je watakapositisha ufadhili wa pango la ofisi.
“Pia tunaomba ofisi za mikoa kupitia TAMISEMI wazipatie ofisi kamati zote za mikoa za SHIVYAWATA ili kuwezesha uratibu wa pamoja wa masuala yetu kwenye mikoa husika,” alisema katika maadhimisho hayo yaliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, vyama vya siasa na wawakilishi wa walemavu kutoka mikoa yote nchini.
Maadhimisho ya siku ya watu wenye ulemavu duniani ni moja ya jitihada za jumuiya ya kimataifa katika kuelimisha jamii kuhusu hali waliyonayo watu wenye ulemavu. (bongoleaks)

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...