Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),
Jaji Damian Lubuva amesema ofisi yake ilijaribu kuazima vifaa vya
kielektroniki vya Biometric Voters Registration (BVR) katika nchi ya
Kenya na Nigeria kwa ajili ya kuandikisha wapiga kura, lakini nchi hizo
zilikataa.
Uamuzi wa NEC wa kutaka kuazima vifaa hivyo ni
kutokana na mchakato wa uandikishaji kukwama kwenda kama ulivyopangwa
kutokana na BVR 250 zilizopo kutokuwa na uwezo wa kuandikisha wapiga
kura wote nchini.
Kitendo hicho kinaweza kusababisha Kura ya Maoni
iliyopangwa kufanyika Aprili 30 mwaka huu kushindikana kwani mpaka sasa
ni mkoa wa Njombe pekee uandikishaji unaendelea kufanyika ambako
utamalizika Aprili 12, 2015.
“Tulitaka kuazima Kenya lakini wakasema
wanavitumia hata kama wamemaliza uchaguzi lakini mchakato wao wa
uandikishaji unaendelea kutokana na kwamba watu wao wanapofikisha umri
wa kuandikishwa wanawaingiza katika daftari lao,” alisema Jaji Lubuva na
kuongeza:
“Tulikwenda Nigeria nako walitueleza wanazitumia. Kuazimana siyo jambo geni kwetu na huu ndiyo ukweli wake.”
Kuhusu mchakato wa uandikishaji mkoani Njombe
alikoweka kambi alisema: “Uandikishaji huku unakwenda vizuri licha ya
kauli mbalimbali na mimi nimekuwa nikiwahamasisha kujitokeza na
tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa.”
Katika uchaguzi wa Ghana uliofanyika mwaka 2013
mfumo wa BVR ulitumika na kuonyesha mafanikio makubwa. Hata hivyo,
Malawi iliukataa mfumo huo katika uchaguzi wa mwaka 2014 baada ya
kuonyesha udhaifu mkubwa katika uchaguzi wa mwaka 2005.
Katika mahojiano maalumu na viongozi, wahariri na
waandishi wa habari wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL)
inayochapisha magazeti ya Mwananchi, Mwanaspoti na The Citizen makao
makuu ya kampuni hiyo Tabata Relini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa
CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema, NEC ilianza mchakato huo bila
vifaa ikitegemea kuazima.
“Tulipokwenda Kenya na TCD (Kituo cha Demokrasia
Tanzania) kuangalia walivyofanikisha mchakato huo wakatueleza kuwa NEC
walikuja hapa kuazima BVR za kuandikisha... tulikuwa na mawaziri pale
yaani ilikuwa aibu na walitueleza kama hadi Novemba hamjanunua hamuwezi
kuandikisha. Walisema walikuwa na BVR 15,000 Kenya na waliandikisha
wapiga kura milioni 14 kwa zaidi ya siku 45 hadi 60, sisi tuna matatizo,
matatizo.
“Wanatupa wasiwasi mkubwa, ikiwa lengo ni
kuandikisha wapiga kura wote haiwezekani tukawa na kura ya maoni Aprili
30, lakini ukiwa unahitaji lazima uandikishe kwanza halafu ufanyike
uhakiki wake, lakini muda huo hautoshi?
Kauli hiyo ya Profesa Lipumba kuhusu kusimamishwa
kwa kura ya maoni pia ilitolewa Februari 12 na viongozi wa vyama 22 vya
siasa walipokutana na NEC kujadili mchakato huo wa uandikishaji kwa
kutumia BVR.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
alisema: “Mchakato huu ni muhimu na kama hautafanyika vizuri tutaichafua
nchi yetu. Wadau washirikishwe na waridhike kwani kusipokuwa na uwazi
kutaleta shida huko mbele.” (CHANZO: MWANANCHI)
No comments:
Post a Comment