Soko Kuu la Manispaa ya Iringa, mkoani Iringa linakabiliwa na
uhaba wa samaki kutokana na uvuvi haramu unaoendelea katika Bwawa la Mtera.
Baadhi ya wafanyabiasha wa samaki walioongea na gazeti la Nipashe
leo walisema uhaba wa samaki katika soko hilo unatokana na sababu nyingi na
kubwa zaidi ni uvuvi haramu uliyokidhiri katika Bwawa la Mtera.
Walisema kuwa kuna uvuvi haramu unaondelea katika bwawa hilo
unaofanywa na wafanyabiashara wakubwa kwa kushirikiana na viongozi na wanasiasa
wanaofanya biashara ya kuvua samaki wadogo wanaofahamika kwa jina maarufu kama dungu.
Walisema kuna wafanyabiashara wakubwa, viongozi wa serikali
na wanasiasa wanachochea kukuwa kwa biashara ya uvuvi haramu kwa kutumia nyavu
zenye nchi moja kuvua samaki katika bwawa pamoja na kufungua maduka mengi ya
nyavu zenye macho madogo (small mesh fish nets) kila kona.
Walisema kuwa siasa imekuwa ikitumika kuchochea biashara
haramu ya uvuvi na kuingilia kazi za wataalamu ambapo wafanyabiashara hao walishauri
kuwa kazi ya wataalamu iaachwe ifanywe na wataalumu wenyewe na masuala ya siasa
yawekwe pembeni ili kunusuru kizazi cha samaki bwawa la Mtera kisipotee.
Francis Haule, ni wafanyabiashara ya samaki maarufu ambaye
alianza biashara ya samaki tangu mwaka 1984, alisema kuwa kuna sababu nyingi
zinazopelekea kupungua kwa samaki sokoni hapa.
Alisema kuwa sababu ya kwanza kabisa vyanzo vya samaki
vimekuwa ni vilevile havioongezeki wakati walaji wa samaki wanaongezeka kila siku lakini vyanzo vya
samaki vinabakia vile vile.
Alisema kuwa kimekuwa na chanzo kimoja cha samaki cha Bwawa
la Mtera ambapo samaki wanaotoka katika bwawa hilo wanapelekwa katika mikoa
mbalimbali kama vile Mbeya, Ruvuma, Njombe, Dodoma, Morogoro, Dar es Salaam,
Lindi na Mtwara.
Aidha, alisema samaki wanaopatikana katika bwawa la Mtera ni
pamoja na Perege, Kambale, Galala, Sulusulu, Mchema na Katoga.
Alisema kuwa sababu nyingine inayosababisha kuwa na uhaba wa
samaki ni bwawa hilo kukauka maji kutokana na kilimo cha umwagiliaji cha mpunga
katika Mto Ruaha.
“Kumekuwa na matumizi mabaya ya maji yasiotumika kulingana na
mahitaji, maji mengi yanaenda porini bure. Watu wanatakiwa kiwa na kilimo cha
umwagiliaji endelevu kwa kutumia maji kulingana na mahitaji na baada yakutumika
maji yarudishwe kwenye mkondo wake wa mto yakatumike kuzalisha umeme katika
bwawa la Mtera,” alisema Haule.
Alisema kuwa kuwepo na matumizi ya maji yasiotumika kulingana
na mahitaji kunapelekea kupungua kwa maji bwawa la Mtera na kusababisha tatizo
la umeme la mara kwa mara.
Alisema pia kwamba kumekuwepo na mahitaji makubwa ya samaki
katika jamii na baada ya watu wengi kuacha kula nyama nyekundu (red meat) na kukimbilia
kwenye nyama nyeupe (white meat) baada yakushauriwa na madaktari kuwa nyama
nyekundu ina madhara kiafya.
Alisema kuwa watu wengi wamekuwa wakikimbila kula nyama
nyeupe kama vile samaki, kuku na kitimoto, ambayo wanadai kwamba haina madhara
ukilinganisha na nyama nyekundu ambayo ina kemikali kwenye nyama kutokana na
madawa yanayotumika kufugia.
Naye, Henry Shabani ambaye pia ni mfanyabiashara wa samaki
katika Soko Kuu la Manispaa alisema kuwa uhaba ya samaki sokoni ni kutokana na uvuvi
haramu unaendelea katika bwawa la mtera bila kudhibitiwa.
Alisema kuwa uvuvi haramu unaofanywa aidha na wafanyabiashara
wakubwa kwa kushirikiana na viongozi mbalimbali wa serikali na wanasiasa kwa
maslahi binafsi ndio chanzo cha uhaba wa samaki.
Alisema kuwa wafanyabiashara hao wakubwa kwa kushirikiana ama
na viongozi wa serikali na wanasiasa wamekuwa wakifanya uvuvi haramu kwa
kutumia nyavu zenye nchi moja badala yakutumia nyavu za nchi tatu ( 3 ply fish nets) zinazoruhusiwa.
Alisema kuwa nyavu zenye nchi moja kimsingi ni makokolo kwa
sababu zinakusanya kila aina ya samaki wakubwa kwa wadogo pamoja na samaki
wenye mayai.
Alisema kuwa na kuwepo kwa kuzembea kwa waatalamu hasa
mabwana samaki ambao muda wote wapo maofisini na kuruhusu watu wafanye uvuvi
haramu tatizo lingine linalosababisha kukosekana kwa samaki sokoni.
“Na kumbuka enzi za Magufuli wakati akiwa Waziri wa Uvuvi
kulikuwa na udhibiti mkubwa wa uvuvi haramu tulishuhudia makokolo yakikamatwa
na kuchomwa moto lakini leo hii uvuvi haramu ni jambo la kawaida…!,” alisema
Shabani.
Alisema wafanyabiashara wakubwa wana maduka ya kuuza nyavu
kila kona lakini cha kushangaza hakuna bwana samaki au kiongozi yeyote wa
serikali anayekagua maduka hayo kuhakikisha yanauza nyavu zilizoruhusiwa kuvua
samaki.
Aliongeza kuwa wamekuwa wakishuhudia pia magari makubwa
kutoka nchini Congo ya kibeba samaki wadogo
(dungu)pale Mtera kwa kuwa kuna soko kubwa la samaki wadogo wanaovuliwa
kinyume cha kisheria.
“Ndugu mwandishi wa habari hebu jaribu kutembelea kila meza
ya samaki hapa sokoni utaona samaki wadogo kwa jina maarufu (dungu), zamani
ukikutwa unauza samaki kama hawa unakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria
pamoja na mtu aliyekuuzia samaki hao kutoka bwawani.
Laiti mabwana samaki
wangekuwa wakifanyakazi ipasavyo na kufuatilia kwa makini kuhakikisha nyavu
zenye macho madogo na samaki wadogo
kudhibitiwa wasingefika hapa sokoni,” alisema Shabani.
Alisema kuwa samaki hao wadogo kwa mfano, wanauzwa shilingi
30/- mmoja wakati samaki mkubwa mmoja anauzwa kati ya 2,000/- na 5,000/-, kwa
maana hiyo utalazimika kuuza samaki wadogo kwa wingi ili upate shilingi elfu
mbili au elfu tano.
Aliongeza kwa mtazamo wake yeye kuwa baada ya miaka mitano
ijayo bwawa la Mtera litakauka na samaki watapotea kutokana na baadhi ya watu
kulima karibu na bwawa kunako sababisha bwawa kujaa udongo kutokana na shughuli
za kilimo kandokando la bwawa.
Alisema biashara ya samaki imemfanya ajenge nyumba na
kupeleka watoto shule lakini anapoona uvuvi haramu unaendelea kunamfanya akate
tamaa.
“Nimekuwa katika biashara ya kuuza samaki tangu 2002 na
takribani miaka 13 sasa nipo bado kwenye biashara hii nimejenga nyumba yangu na
kupeleka shule watoto kwa biashara hii, lakini ninapoona uvuvi haramu huu…
isee,” alimalizia shabani.
No comments:
Post a Comment