Songea/Dar. Wananchi wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma jana walikumbwa na taharuki baada ya askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuvamia mitaa, ofisi za Serikali na binafsi, benki, nyumba za ibada na katika maeneo ya biashara wakiwa na silaha huku magari yao yakiranda kila kona na kuanza kuwapekea watu wote waliyekutana naye huku wakidai kuonyeshwa vitambulisho.
Hata hivyo, hiyo ni mara ya kwanza kwa wanajeshi hao kuchukua hatua hiyo ambayo ilielezwa kuwa ni sehemu ya mazoezi na mafunzo kwa vitendo.
Wananchi waliohojiwa na gazeti hili kwa nyakati tofuti kufuatia kizaazaa hicho akiwamo Anastazia Mhale alisema alikutana na wanajeshi hao alipokuwa akielekea benki, walimsimamisha na kumuuliza maswali kisha wakamfanyia upekuzi.
“Nilishangaa kusimamishwa na wanajeshi na kutuhoji maswali huku wakitutaka tuwaonyeshe vitambulisho, hali hii iliwakuta hata watu waliokwenda wanakwenda sokoni,” alisema Mhale.
Alisema mbali ya kuwakagua raia, pia walisimamisha kila gari barabarani na kulifanyia upekuzi sambamba na abiria waliokuwa ndani ya magari hayo.
Erasto Haule alisema: “Hata kama hakuna madhara yoyote wangetutangazia kama wanafanya mazoezi, wametutia hofu kubwa,” alisema.
Alisema baadhi ya watu jana walishindwa kutoka kwenda kuendelea na shughuli zao wakihofi kukamatwa na wanajeshi hao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela alipoulizwa alisema zoezi hilo ni la kawaida na aliwataka wakazi mjini humo kuwa na amani na waendelee kufanya shughuli zao kama kawaida.
Gazeti hili pia liliwashuhudia askari hao wa jeshi wakiwa wametanda eneo lote la ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, lilipotaka kwenda kuonana na mkuu wa mkoa ili atolee maelezo zoezi hilo.
Alipoulizwa Brigedia Jenerali wa Kamandi ya Kusini, John Chacha alisema hiyo ni sehemu ya mafunzo kwa wanajeshi hao.
Alisema JWTZ hufanya mafunzo mbalimbali ya kujiimarisha ikiwamo ya kulinda miji, maporini na mengineyo.
“Mazoezi haya yameanza leo (jana) na tutamaliza usiku. Mafunzo hayo ni muhimu kwetu, yanatoa mbinu za kujihami na uvamizi wa adui yeyote anayeweza kuingia ndani ya mipaka yetu na kuteka viwanja vya ndege, ofisi nyeti za Serikali, benki au hospitali kubwa, ndiyo maana tunayafanya mahali popote,” alisema.
Hata hivyo, Brigedia Chacha alisema kabla ya kuanza kwa zoezi hilo, walitoa taarifa katika ofisi zote kuanzia ngazi ya kata hadi wilaya kwa lengo la kuondoa hofu ambayo ingeweza kutoa kwa wananchi. (CHANZO: MWANANCHI)
No comments:
Post a Comment