Dar es salaam. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema uandikishaji wa wananchi kwenye Daftari la Wapigakura nchini utamalizika mwishoni wa mwezi ujao baada ya mashine 1,600 zaidi za kielektroniki kwa ajili ya kazi hiyo kuwasili juzi.
Ofisa ugavi mwandamizi wa NEC, Datus Matuma alisema mashine hizo zinazotumia teknolojia ya utambuzi wa alama za mpigakura (Biometric Voter’s Registration), zitaanza kupelekwa mikoa ya Mara, Arusha, Manyara na Kilimanjaro.
“Ule uvumi ambao ulikuwa ukienea nchini kwamba Tume ya Taifa haiwezi kumaliza uandikishaji, sasa umefikia mwisho kwani hizi mashine ni za kisasa na zitaanza kazi moja kwa moja kwenye mikoa hiyo niliyoitaja na mwishoni mwa mwezi Juni au mwanzoni mwa mwezi wa Julai watu wote watakuwa wameshaandikishwa,” alisema Matuma.
Alisema wananchi wajitokeze kwa wingi kujiandikisha ili wasikose haki yao ya msingi ya kupiga kura kwani kila aliyefikisha umri wa kupiga kura anatakiwa kujiorodhesha kwenye daftari hilo.
Alisema Serikali ni sikivu ndio maana imekata kiu ya Watanzania kwa kuleta mashine hizo ambazo sasa zimefikia 8,000 na zinakidhi kabisa mahitaji ya Watanzania wote kwani zinafika kila mkoa na zitagawiwa kwenye halmashauri kwa ajili ya kuzisambaza kwenye vituo vya uandikishaji .
BVR 250 ndizo za kwanza kuwasili na kutumika kwa majaribio katika majimbo ya Kawe, Kilombero na Mlele na baadaye kutumika kwenye uandikishaji mkoani Njombe.
Baadhi ya changamoto zilizojitokeza katika uandikishaji huo ni mashine kushindwa kutambua vidole sugu na kuchukua muda mrefu kuandikisha mtu mmoja. Hata hivyo changamoto hizo zilipatiwa ufumbuzi
Wadau wa uchaguzi walipokutana na NEC Februari 12, mwaka huu waliilalamikia tume hiyo kushindwa kuweka wazi ratiba, makadirio ya wapiga kura watakaoandikishwa, mzabuni wa vifaa hivyo, nchi vinakotoka, kiasi cha fedha kilichotolewa na serikali na kampuni inayohusika kuweka mfumo wa ndani wa mashine hizo.
Aprili 2, NEC ilitangaza rasmi kushindikana kwa kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa iliyokuwa imepangwa kufanyika Aprili 30 baada ya kushindwa kumaliza kuandikisha wapigakura kama inavyopanga.
NEC ilisema uandikishaji utaendelea na kwamba hadi kufikia Julai, mwaka huu watakuwa wamemaliza nchi nzima na kwa kushauriana na Tume ya Uchaguzi Zanzibar watatangaza tarehe ya Kura ya Maoni.
Uhaba wa BVR uliwapa wasiwasi wadau wengi hususani vyama vya siasa kwamba uandikishaji hautakamilika kufikia Julai na kwamba hali hiyo inaweza kusababisha kuahirishwa kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Hata hivyo, mwezi uliopita NEC ilitangaza kwamba hakuna mpango wowote wa kuahirisha Uchaguzi Mkuu na kusisitiza kuwa utafanyika kama ilivyopangwa.
No comments:
Post a Comment