Friday, 15 May 2015

TTCL YATOA MSAADA WA KOMPYUTA KUMI KWA GLOBAL OUTREACH





KUMPUNI ya Simu Tanzania (TTCL) imekabidhi kompyuta kumi (10) pamoja na kifurushi cha intaneti ya bure yenye kasi ya 2Mbps kwa muda wa miezi sita vyote vikiwa na thamani ya 20,197,600/- kwa ajili ya Iringa Secondary School Internet Library (ISSIL).

Kampuni ya simu hiyo ya kizalendo ambayo inatoa huduma mbalimbali  za mawasiliano nchi imetoa misaada hiyo Global Outreach Tanzania ili kuunga mkono mradi wa maktaba mtandao (intaneti) katika kuboresha mfumo wa elimu nchini.


Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL Dr. Kamugisha Kazaura, Meneja wa Kanda Nyanda za Juu Kusini, Juvenal Utafu alisema kuwa TTCL in moja ya wadau muhimu katika kuboresha sekta ya elimu nchini kupitia teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHEMA/ELIMU MTANDAO).

Alisema jana kuwa kampuni imekuwa mstari wa mbele katika kuchangia juhudi zinazofanywa na serikali na wadau wengine katika kuboresha mfumo wa elimu kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu.

“Ili kuungana na Global Outreach Tanzania katika mradi huu mkubwa TTCL imetoa kompyuta kumi (10) pamoja na kifurushi cha intaneti ya bure kwa miezi sita,” alisema.

Alisema kuwa kituo hicho kitasaidia kuleta manufaa kwa wanafunzi wote pamoja na walimu wao na kuwaasihi wanafunzi na walimu kutumia kituo hicho ipasavyo ili kujiendeleza kielimu na kutanua wigo wa maarifa kupitia intaneti (elimu mtandao).

Hata hivyo, meneja wa kanda hiyo aliwaasa vijana wote waitumie huduma hiyo ya intaneti kwa malengo yaliyo kusudiwa na kuachana na matumizi mengine yasiyo na tija, ambayo yanapatikana kwenye intaneti kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza ambaye aliwakilishwa na Afisa Elimu Mkoa Eusedius Mtavangu alipokea msaada huo kwa niaba ya Global Outreach Tanzania katika hafla fupi iliyofanyika katika Kituo cha Kichangani Student Center mjini Iringa.

Mkuu wa mkoa huyo alitoa shukrani za dhati kwa uongozi na wafanayakazi wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) kwa juhudi za kuinua sekta ya elimu pamoja na sekta zingine.

“Jambo hili ni mfano wa kuigwa kwa makampuni mengine, sisi kama serikali tunatambua mabadiliko na ukuwaji wa tecknolojia kwa kasi ambao si budi kwa Tanzania-tukiwemo wanairinga, tujiandaa vyema ili kukabiliana na maendeleo hayo ili tusibaki nyuma,” alisema.

Pia alilipongeza shirika lisilo la kiserikali la global outreach Tanzania kwa kuanzisha mradi wa kuinua elimu kupitia teknolojia ya habri na mawasiliano.

Aidha, aliwaasa wanafunzi, walimu na wadau wengine wanaotumia kituo hicho kama chachu au njia ya kujiongezea maarifa, kutumia intaneti kutafuta vitabu au taarifa ambazo zitawasaidia katika masomo.

Pia kuelewa dunia sasa inakwendaje kiuchumi, kisiasa, na kisayansi pamoja na kutumia intaneti katika lengo la kutafuta fursa mbalimbali za masomo, kubalishana mawazo na wataalam kwa nia njema na sio kinyume chake.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Global Outreach Tanzania, Francis Mwachombe alisema shirika hilo lilianzishwa na Stan Muessle mwaka 1998 chini ya Global Outreach U.S.A na kusajiliwa mwaka 2007 kama Global Outreach Tanzania.

Lengo kuu la shirika hilo ni kuingiza elimu ya teknolojia ya kompyuta katika mihtasari ya shule za sekondari ili kuongeza ufaulu.

Shirika hilo limefanya na linafanya kazi na shule za sekondari za Pomerini, Image, Bomalang’ombe, Nyerere, Lugalo, Shule ya Sekondari ya Wasichana Iringa, Mafinga Seminary, Ifunda Shule ya Ufundi, St.     Micheal, Mawelewele, St. Joseph Ipogolo, Mtera na Cagliero.

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...