Sunday, 21 June 2015

GRL yakabidhi jengo kwa kijiji cha Mabaoni


Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mabaoni, Sailas Ndenga (kushoto) akipekea hati ya jengo kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa Green Resources Ltd, Anthony Kisondella wakati wa hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika katika Kijiji cha Mabaoni, wilayani Mufindi, mkoani Iringa jana. (PICHA NA FRIDAY SIMBAYA)

Wananchi wa Kijiji cha Mabao, viongozi wa Green Resources Ltd pamoja na viongoizi wa serikali wakiwa nje jengo jipya lililojengwa na Kampuni ya GRL na kukabibidhiwa kwa serikali ya kijiji hicho baada ya hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika katika Kijiji cha Mabaoni, wilayani Mufindi, mkoani Iringa jana. (PICHA NA FRIDAY SIMBAYA)



Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mufindi (DED) akihutubia wananchi wa Mabaoni.

Rai hiyo imetolewa jana na Kaimu Mkurugenzi wa GRL, Anthony Kisondella kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Roselyne Mariki, wakati akikabidhi jengo la ukumbi na ofisi kwa Kijiji cha Mabaoni katika Kata ya Makungu, wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa.

Kaimu mkurugenzi huyo aliwataka  wananchi kutoa ushirikiano unaostahili na michango iliyo ndani ya uwezo wao kama nguvukazi na vifaa kama mawe, matofali na mchanga.


Alisema kuwa mradi wa ujenzi wa jengo la ukumbi na ofisi kwa ajili ya serikali ya Kijiji cha Mabaoni ulianza rasmi Oktoba mwaka jana, ambapo ujenzi wake uligharimu jumla ya shilingi 66,439,456/-.

Aidha, alisema jamii ilishiriki kwa kiasi kikubwa kutoa nguvukazi wakati wa utekelezaji wa mradi huu.

“Jengo hili lina ukumbi wenye uwezo wa kuchukua watu 200 kwa ajili ya kufanyia mikutano, sherehe na semina na vilevile jengo hilo lina vyumba vinne vya ofisi na vyumba viwili vya kuifadhia wahalifu, ” alisema.

Alisema kuwa ujenzi wa jengo hilo ulisimamiwa kwa niaba ya GRL na shirika linaloitwa ‘Southern Highlands Participatory Organization (SHIPO)’ lenye makao yake makuu mkoani Njombe.

Kampuni ya GRL imekabidhi rasmi Halmashauri ya Serikali ya Kijiji cha Mabaoni jengo la ukumbi na ofisi mbele ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, ili kama wamiliki waweze kulitumia kulingana na malengo yaliokusudiwa.

“Moja ya mikakati ambayo Kampuni ya GRL imejiwekea ni kushirikiana na jamii kwenye maeneo iliyowekeza kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya jamii katika sekta ya afya, elimu na kadhalika inaotokana na mahitaji na vipaumbele vya jamii husika,” alisema kaimu mkurugenzi mtendaji.

Hata hivyo, mradi wa ujenzi wa ukumbi na ofisi hiyo ni moja ya miradi itakayozinduliwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru unaotarajia kuwasili wilayani Mufindi tarehe 25 Juni mwaka huu.

Mwenge wa Uhuru katika Mkoa wa Iringa  utaweka mawe ya msingi, utakagua, utazindua na kufungua jumla ya miradi ya maendeleo 35 yote ikiwa na thamani ya 4,985,562,793/=. 

Green Resources Ltd (GRL) ni kampuni tanzu ya Green Resources AS ya Norway. GRL imewekeza katika sekta ya misitu ikiwa na mashamba makubwa ambapo hekta 17,000 tayari zimepandwa miti katika wilaya za Mufindi na Kilombero.
Zaidi ya miche milioni tano (5,000,000) imegawiwa kwa  wananchi wa vijiji na kutokana na mafunzo waliopatiwa ya namna ya utunzaji na upandaji wa misitu, hekta zinazokadiriwa kufikia 20,000 zimepandwa miti katika mashamba binafsi ya wanavijiji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mufindi (DED), Saada Malunde ambaye pia alikuwa mgeni rasmi katika makabidhiano ya  jengo la ukumbi na ofisi kwa Kijiji cha Mabaoni, aliishukuru kampuni ya GRL kwa msaada huo.

Aidha, DED huyo aliwaasa wananchi wa Kijiji cha Mabaoni kwa kuhakikisha wanatunza vizuri jengo na endapo kutatokea uharibifu wowote, basi watafanya matengenezo yanayotakiwa.

 Alisema kuwa serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Dkt. Jakaya Kikwete imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji nchini.

“ Na faida ya uwekezaji ni kama haya matunda tunayoyaona leo kwa kijiji cha Mabaoni,” aliongezea.

Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mabaoni, Sailas Ndenga aliishukuru Kampuni ya GRL kwa msaada huo kwa niaba ya wananchi wake na kuahidi kushirikiana na kampuni hiyo kwa lengo la koboresha maisha ya wananchi.

Alisema kuwa wakati anatoa ardhi hiyo kwa kampuni ya GRL, wapo wananchi waliothubutu kumnyoshea vidole kwamba ameuza ardhi ya kijiji kwa mwekezaji, lakini leo wanaona matunda yake.

Aidha, kampuni hiyo ya Green Resources Ltd ina bustani kubwa ya kuzalisha miche iliyopo Kijiji cha Mabaoni.

Mashamba mengine ya miti yapo kwenye vijiji vya Mapanda, Chogo, Ukami, Incomet na Idete kwa Wilaya ya Mufindi na vijiji vya Uchindile, Masagati na Kitete kwa Wilaya ya Kilombero.


No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...