Thursday, 23 July 2015

KUMEKUCHA WATIA NIA WASHUTUMIANA KWA RUSHWA JIMBO LA IRINGA MJINI


Watia nia Jimbo la Iringa Mjini kushoto ni Peter Mwanilwa, Micheal Mlowe, Mahamudu Madenge, Dk. Yahaya Msigwa, Frank Kibiki na Frederick Mwakalebela wakati wakiongea na waandishi wa habari kuhusu ukiukwaji wa kanunu za uchaguzi wa CCM.





Madenge (katikati) akisoma kanunni hizo kwa wanahabari

WAKATI Joto la uchaguzi likishuka na kupanda mkoani Iringa kada wa chama chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa huo na mtia nia kugombea ubunge wa jimbo la Iringa Mjini kwa tiketi ya chama cha mapinduzi CCM, Jesca Msambatavangu ametuhumiwa na makada wenzake wa chama hicho kwa kutoa rushwa kinyume na matakwa ya maadili na kanuni ya chama hicho.

Msambatavangu ametuhumiwa na makada wenzake 11 kati ya 13 ambao wameomba ridhaa ya kuwania kugombea ubunge jimbo la Iringa Mjini kwa tiketi ya CCM .

Shutuma hizo zimakuja mara baada ya kila mgombea kwa maana ya makada hao kuanza kutembelea kata hadi kata za wanachama wa jimbo hilo kwa lengo la kujinadi kwa wanachama na kuwaomba wawasikilize kila mmoja sera zake na baadaye wananchama waweze kufanya maamuzi ya kumchagua kiongozi wanayemtaka.

Wakizungumza leo kwenye ofisi ya CCM Manispaa ya Iringa baadhi ya watia nia walitoa malalamiko hayo mbele ya wanahabari na kusema kuwa Msambatavangu alithubutu kuwatumia wapambe wake kwa kugawa fedha, na kuwashawishi kuondoka kwenye mkutano mara tu yeye anapomaliza kuhutubia jambo linalowafanya watia wenzake hao kukasirika na kukosa sera za wanachama wengine.

Tamko hilo lililodaiwa linahusisha wagombea waliofika kwenye kikao walikuwa sita ambao ni Mahamoud Madenge, Frederick Mwakalebela, Peter Mwanila, Frank Kibiki, Michael Mlowe na Dk Yahya Msigwa.

Akizungumza Mahamud Madenge ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauari kuu ya CCM Taifa alimtuhumu Jesca kuwa amekuwa akijihusha na vitendo vya rushwa tangu walipoanza harakati za kujitambulisha huku akiwataja wapambe wa mgombea huyo kuwa Hosea Kaberege na Clara Shirima kuhusika na vitendo vya utoaji wa rushwa.

Katika mkutano uliofanyika juzi kwenye tawi la CCM eneo la Don Bosco, Madenge alisema Jesca katoa rushwa kwa wanachama na kusema sisi watia nia wengine tulipata taarifa hizo na kufanya uchunguzi ndipo walipomkuta mpambe wake akitoa fedha hizo kwa wanachama.

“Yaani sisi tuliamua kutumia walinzi wetu wa chama (Green Guard) na kufanikiwa kumkamata Kaberege akiwa na Sh 100,000 alizokuwa akizigawa,alipoulizwa alisema fedha hizo ni za mafuta lakini alipohojiwa zaidi alitupa chini na kukimbia,” alisema Madenge.

Alisema kufuatia tukio hilo walilazimika kutoa taarifa Ofisi ya kupambana na rushwa mkoa wa iringa (Takukuru) ambao walifika eneo la tukio kwa ajili yakufanya uchunguzi wa tukio hilo.

Katika hatua nyingine Madenge alimtuhumu Clara Shirima kuwa amekuwa akigawa madela ya CCM kwa wakinamama ambao hufanya kazi ya kumshangilia Mgombea huyo anapozungumza kwenye mikutano hiyo ya kujitambulisha huku akihusika kuwashawishi wanachama kuondoka mara tu anapomaliza kuhutubia yeye.

Alisema vitendo vyote hivyo vinakiuka katiba na kanuni za chama hicho na kwamba ikiwa vitaachwa viendelee vitawezesha chama kupata mgombea asiyekubalika na wananchi hivyo kuwiwa vigumu chama kulikomboa Jimbo la Iringa mjini ambalo linamilikiwa na Mchungaji Peter Msigwa Chadema.

Alipoulizwa mwenyekiti huyo na wanahabari alisema "Mimi sijawahi kufanya kitu kama hicho na ninajua mtu aliyefanya huo mchezo, amemhumu kijana mmoja kutoka Ipogolo,... ndio sababu huyo wanayedai alikamatwa na hizo fedha wanazo wao, mimi Kaberege si mpambe wangu tu bali ni kijana anayefanya kazi kwangu"alisema Jesca.

Kwa upande wake Hosea Kaberege ambaye alituhumiwa kugawa rushwa na kukamatwa na Takukuru alikanusha madai hayo na kudai kamba wanaofanya hivyo wameamua kumchafua kwa kuwa yeye ni mtia nia wa nafasi ya udiwani kata ya Mtwivila na pia anamuunga mkono Jesca katika harakati zake za Ubunge.

Naye Clara Shirima aliyedaiwa kugawa Madela ya chama hicho kwa wananchama alikanusha tuhumu hizo mbele ya waandishi wa habari na kuwataka wanaomtuhumu kwenda kuwahoji wakinamama waliovaa madela hayo kama wamepatiwa na yeye.

Kwa upande wake Kamanda wa Takukuru, Mkoa wa Iringa Eunice Mmari alithibitisha kuwapo kwa taarifa hizo na kuongeza kuwa ofisi yake inaendelea kuzifanyia uchunguzi ili kupata ukweli wake.

"Labda nikueleze sisi kama takukuru tumezipata hizo taarifa na tutaendelea kuzifanyia uchunguzi wa kina kubaini kama ni kweli.”alisema Mmari.

Naye mtia nia Frederick Mwakalebela ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe  aliitaka vyombo vya dola ikiwamo taasisi ya kupambana na Rushwa (Takukuru) kufanyia kazi mambo jambo hilo na kuwachukulia hatua kali za kisheria kwa wale wote watakaobainika wanahusika matukio kama hayo.

“Mimi binafsi ninashangaa sana kuona watu wanatoa rushwa sisi tunataka uchaguzi huu uwe wa amani na upendo kuanza kuchafuana chama hakitapata mgombea makini jambo ambalo si kitu kizuri na kufanya hivyo tutakuwa hatujawatendea wananchi haki yao ya msingi.”alisema Mwakalebela.

Kwa upande wake Frank Kibiki ambaye ni mmojawapo kati ya watia nia hao alisema kuwa kitendo hicho kinakiuka kanuni na sheria za chama hicho zinazokataza rushwa.

Hata hivyo Dk Yahya Msigwa ambaye ni katibu mwenezi wa CCM mkoa wa Iringa alisema vitendo hivyo vinahatarisha chama ni vikiachwa viendelea vinaweza kuleta mgombea asiye na sifa na kuwawia vigumu wao kumuunga mkono mgombea anayepita kwa hila hata vinaweza kusababisha amani kwa wakazi wa jimbo hilo.

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...