Thursday, 16 July 2015

MAMBO MATANO YALIYOMPA KIJITI MAGUFULI




Watanzania wengi na hata wagombea wa CCM walipigwa na butwaa kubwa baada ya kuona Dk John Magufuli anachaguliwa kuwa mgombea urais wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Ni watu wachache walimshtukia Dk Magufuli tangu awali na kuona uwezekano wa kiongozi huyo kufika happ alipo leo. Nataka tujadili mambo matano ambayo nayaona kama sababu za CCM kumpa kijiti “Tingatinga” huyu.

1. Kura za kanda ya ziwa

Hili ni jambo la kwanza ambalo liliwafanya wapanga mikakati wa CCM kumvusha Magufuli. Ukiachilia mbali kufahamika kwake nchi nzima, lakini Magufuli anatoka kanda ya ziwa ambako kuna wapigakura wengi lakini kukiwa na ‘hatihati’ ya majimbo mengi kuelekea upinzani. Kanda ya ziwa si salama kwa CCM na lazima chama hicho kingehitaji mkakati wa kudhibiti wapigakura kwa kuwaletea kitu kitakachowaamshia matumaini mapya.

Kanda ya ziwa inaundwa na mikoa ya Simiyu, Mwanza, Shinyanga, Kagera, Mwanza, Geita na Mara na kuna jumla ya wakazi 11,832,857 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012. Nusu ya wapigakura walioko Kanda ya Ziwa, yaani watu milioni tano wanaweza kuwa wapigakura, hiyo inamaanisha kuwa hii ni idadi inayolingana na kura alizopata Rais Kikwete mwaka 2010.

Nataka ifahamike kuwa kwa namna nchi yetu ilivyo, Kanda ya Ziwa ndiyo inaamua nani aongoze Taifa hili na watu wa kanda hiyo wana tabia ya kujitokeza kupiga kura. Kama tungekuwa tunafanya sensa za kiteknolojia na zinazokusanya taarifa sahihi, naamini kanda ya ziwa ingeweza kujenga zaidi ya theluthi moja ya wakazi wa taifa hili na jambo hilo linadhihirisha mantiki kuwa hii ni ngome ya ushindi kwa chama chochote kile.

Hivi karibuni, CCM imepoteza majimbo mengi kwenye kanda hii na kumtoa mgombea urais eneo hili kuna maana nyingine ya kuwafanya wapigakura warudishe imani kwa “mtu wa kanda yao” hata kama wasingependa kukichagua chama chake. Mkakati wa namna hii unatumika duniani kote na umefaulu maeneo mengi na ili uudhibiti, njia ya haraka huwa ni chama cha upinzani kinachotaka dola nacho kutoa mgombea eneo hilohilo kama ilivyofanya NARC mwaka 2002. Umoja huo wa Kenya ulimsimamisha Mwai Kibaki (Mkikuyu) ili kuvunja nguvu ya chama tawala cha Kenya wakati huo (Kanu) ambacho kilimsimamisha Uhuru Kenyatta (Mkikuyu) kwa lazima kikijua kuwa kitapigiwa kura nyingi kutoka eneo hilo. Uwepo wa Mwai Kibaki kutoka kabila moja na Kenyatta ulifanya Wakikuyu kugawanyika na Kibaki akashinda kushika dola kutoka upinzani. Natumaini kwamba CCM inaijua karata hii muhimu na imeamua kuitumia.


2. Kuvunja makundi CCM

Jambo la pili lililofanya Dk Magufuli akapewa kijiti ndani ya CCM kwa ajili ya uchaguzi huu ni kuwa mtu “asiye na upande”. Kiongozi huyu katika hatua zote za utendaji wake alijiweka kando kutoonyesha kuwa ana nia ya urais wa nchi. Alisimamia majukumu yake kiutendaji zaidi kuliko kisiasa na hali hiyo ilimfanya akae mbali na mivutano ya kimakundi.

Hata alipochukua fomu alikataa kuzungumza na vyombo vya habari juu ya vipaumbele vyake, alipokuwa mikoani akikusanya sahihi za wadhamini hakusikika, hakuwa na mabasi makubwa na hakutaka vyombo vya habari vimfuatilie.

Kubwa kuliko yote, hata mara moja hakuwahi kusikika akiwatishia wenzake au kuwanyooshea vidole na kutoa misimamo. Hii ilimfanya aonekane yeye peke yake ndiye anayeweza kukubalika na pande zote zinazovutana. Ukiachilia mbali sifa nyingine, CCM ilihitaji kuwa na mgombea ambaye walau anaweza kutopingwa sana na wenzake na katika hili naweza kusema kuwa wamefanikiwa.

Nadhani kimkakati ilikipasa chama hicho kumuondoa Lowassa na kumuacha Membe kwenye tano bora ili wajumbe wanaomuunga mkono Lowassa (ambao naambiwa ni nusu ya Halmashauri Kuu) wasisuse kuhudhuria vikao kwani wangekuwa na kiu ya “kumshughulikia” Membe (hasimu mkuu wa Lowassa). Mkakati huu ulifanikiwa vilivyo na kumbe aliposhughulikiwa Membe ndiyo mwanzo wa kumpata Magufuli ambaye pande zote mbili (Membe na Lowassa) hazikuwa na budi kumuunga mkono.3. Kufahamu utendaji ndani ya Serikali na kutokukifahamu chama vizuri

Hili ni jambo la tatu ambalo lilimvusha Dk Magufuli. Nadhani chama hicho kilihitaji kuwa na mgombea ambaye anaitambua Serikali vizuri na anaweza kuisimamia ipasavyo lakini akiepuka kuyumbishwa na mambo ya ndani ya chama chake.

Dhana hii nadhani inafanywa na CCM kama mbinu ya kuwaonyesha wapigakura kuwa chama hicho kinatambua matatizo ya masilahi ya chama kuingizwa katika uamuzi wa utendaji wa Serikali kila mara na njia pekee ya kulifanya jambo hili ni kumpata mtu ambaye hajajishughulisha na masuala ya ndani ya chama ili kama akija, aje na mipango mipya na labda awaweke katika mstari, viongozi waandamizi ndani ya chama na wale watendaji wa kawaida.

Sijui CCM itafanikiwa kiasi gani katika eneo hili lakini ninachotaka kusisitiza hapa ni kwamba chama hicho kilihitaji mtu anayeweza utendaji na usimamizi wa Serikali na ambaye huenda anaweza akahamishia kasumba hiyo ndani ya chama. Kuwa na mantiki na mtizamo huu ni jambo moja na uwezo wa kusimamia masuala haya yatendeke ni jambo jingine lakini yote haya ndiyo yanayomkabili Dk Magufuli kwa sababu amechaguliwa na chama chake kwa kulenga shabaha hiyo.

4. Uwepo wa Ukawa

CCM inaweza kuwa imeshabadili mtizamo wake wa kufanya mzaha na upinzani hasa baada ya Ukawa kuishi mwaka mzima na miezi kadhaa bila kuvunjika. Huko nyuma “miungano ya vyama vya upinzani” ilionekana kama “safari ya panya”, kwamba wakiparaganyishwa kila mtu anapita njia yake na wanaachana. Kama kusingekuwa na Ukawa ni lazima CCM ingekuja na mkakati wa kawaida na mgombea yeyote yule. Lakini uwepo wake, kuungwa mkono kwa umoja huo na wananchi, vimeilazimisha CCM itafute mgombea mbadala ambaye ataonekana “anathubutu” kama wanavyofanya viongozi wa Ukawa ili kujaribu kuwajengea wananchi taswira kuwa “...mlitaka mtu ambaye anasimamia mambo bila mchezo na bila woga, sasa tumewaletea mtu huyo”.

Sauti hii ambayo CCM inajaribu kuipandikiza kwenye mioyo ya Watanzania hata hivyo, inatofautiana kabisa na hali halisi ambayo inabaki kuwa umakini, utendaji na usimamizi wa upinzani ungeweza kufanywa vizuri zaidi kwa sababu ya kutokuwa na mibinyo kutoka ndani ya watu waliozoea mfumo wa kukaa ndani ya Serikali. Hata hivyo, kwa kiasi fulani dhana hii ya CCM itafanikiwa.

5. Kura za vijana, wanawake

Aina ya watu ambao huvutia kura za wanawake na vijana huwa siyo lazima wawe vijana au wanawake, hata wazee na watu wa makamo wenye mtizamo wa kifikra na wanatenda mambo yao haraka kama vijana huchukuliwa kwenye kundi hili.

Vijana wengi wanaweza kuwa mashabiki wa “Magufuli” kutokana na tabia yake ya kuwajibisha watendaji wake hadharani na papo kwa papo. Vijana wengi huishi maisha ya kutegemea maisha ya “fasta fasta” yaani matokeo ya papo kwa hapo. Vijana hutaka “mwizi akiiba auawe hapohapo”, hawataki apelekwe mahakamani wala asikilizwe. Magufuli ana tabia za kufanya maamuzi papo kwa hapo na haiba hii inaweza kuwavutia vijana maana wanategemea kuwa na Rais ambaye anaweza kufika mahali akatoa maamuzi ya papo kwa papo. Ila pia ana mtihani wa kuhakikisha kuwa analinda na kuzingatia haki za binadamu.

Hitimisho

Mambo haya matano yaliyompa Magufuli tiketi ya kugombea urais kupitia CCM yanaweza kabisa kuzuiwa na uimara wa UKAWA. Umoja huo ukipata mgombea thabiti na akajikita pia katika kudhibiti kura za kanda ya ziwa, kuonyesha uthubutu na mipango inayotekelezeka na anayewavutia vijana na wanawake lazima CCM itakuwa kwenye wakati mgumu kwenye uchaguzi wa mwaka huu na Magufuli atakutana na vizingiti vinavyoweza kumkwamisha na hivyo kuondoa kabisa matumaini ya CCM kuongoza dola.Kama UKAWA ikishindwa kufanya kazi pamoja kwenye uchaguzi wa mwaka huu, wananchi hawatafikiria mara mbili – watamchagua Magufuli kwa kishindo na hakutakuwa na mtu wa kulaumu mwingine. UKAWA ndiyo ngao pekee ya kudhibiti uimara wa mgombea wa CCM na kudhibiti imani ya wapigakura wa maeneo yenye watu wengi kama kanda ya ziwa.

Julius Mtatiro ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii. Ana Shahada ya Uzamili na anatarajia kuhitimu Shahada ya Sheria hivi karibuni. +255787536759, juliusmtatiro@yahoo.com – (uchambuzi ni maoni binafsi ya mwandishi).

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...