Rose Tweve
Ritta Kabati
Lediana Mng'ong'o
wajumbe
Zainabu Mwamwindi
wagombea
UMOJA wa Wanawake wa Tanzania (UWT) mkoa wa Iringa umekataa kumuongezea kipindi kingine cha miaka mitano bungeni, Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa, Lediana Mng’ong’o (58) katika mkutano wake wa kura za maoni uliofanyika juzi, mjini Iringa.
Mng’ong’o ambaye pia alikuwa mmoja wa wenyeviti wa bunge la 10 linalomazima muda wake amekuwa mbunge wa viti maalumu mkoa wa Iringa kwa miaka 15.
Akitangza matokeo ya uchaguzi huo, Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alisema kura 375 zilipigwa huku kura tano zikiharibika.
Alimtaja mshindi wa kwanza na wa pili ambao kwa kiasi kikubwa wanajihakikishia kuingia katika bunge lijalo kuwa ni Rose Tweve aliyezoa kura 240 na Ritta Kabati, mbunge anayemaliza awamu yake ya kwanza ya ubunge huo wa viti maalumu mkoa wa Iringa, aliyepata kura 199.
Rose Tweve ni mgombea pekee kati ya wagombea tisa walioshiriki kinyang’anyiro hicho anayetokea wilayani Mufindi.
Masenza aliwataja wengine na kura zao kwenye mabano kuwa ni Lediana Mng’ong’o (162), Shakira Kiwanga (89), Esta Chaula (21), Emma Mwalusamba (14), Hafsa Mtasiwa (10), Farida Ninje (4), na Agnes Nyakunga (4).
Baada ya matokeo hayo Mng’ong’o aliwashukuru wajumbe wa mkutano huo kwa kura walizompatia akaupongeza uchaguzi huo ulivyokuwa huru na haki na kuahidi kushirikiana na jumuiya na CCM kupitia majukumu yake mengine.
“Nimeyapokea kwa mikono miwili matokeo haya, uchaguzi ulikuwa huru na wa haki; naahidi kutoa ushirikiano wangu wa dhati kwa washindi, jumuiya na chama katika shughuli zake mbalimbali nikiwa natekeleza majukumu mengine,” alisema.
Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Iringa, Zainabu Mwamwindi alisema; “uchaguzi wa leo umetoa fursa pekee ya kuimarisha jumuiya yetu kwa miaka mitano ijayo.”
Alisema UWT ina matarajio makubwa kutoka kwa washindi hao wawili katika kuihudumia jumuiya na kusaidia shughuli mbalimbali za chama.
Aliitaja kauli mbiu ya umoja huo mwaka huu kuwa ni “Kura zaidi, Viti Zaidi.”
No comments:
Post a Comment