na fredy mgunda, iringa
WAKATI joto la uchaguzi nlikiendelea kupanda katika jimbo la Iringa mjini, mamia ya vijana, wanawake, walemavu na wazee katika jimbo hilo wanaendelea kuchangishana fedha ili kumuwezesha mwanahabari Frank Kibiki kuchukua fomu ya kuomba ateuliwe kupeperusha bendera ya CCM, kwenye jimbo hilo.
Zoezi hilo linaloendeshwa na baadhi ya vijana waliomtaka Kibiki ambaye ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM taifa, kutotoa rushwa badala yake atumie hoja kuelezea sera zake, walisema wameamua kuchangishana fedha ili kumuwezesha kijana huyo kuchukua fomu.
Wakizungumza na wanahabari, tayari vijana hao walisha mkabidhi Kibiki zaidi ya Sh 200,000 miezi mitatu iliyopita.
“Bei ya fomu ni 100,000 pamoja na michango inafikia 500,000 kwa kuwa tunahitaji kijana kutoka miongoni mwetu, tumeamua kumuwezesha Kibiki ili atuwakilishe kwenye jimbo letu kupitia CCM, hatutaki atoe rushwa kununua uongozi, kwa sababu sisi ndio tunamuajiri kuwa mtumishi wetu,” alisema Salum Mwinami, kada wa CCM.
Michango hiyo inaendelea katika maeneo ya stendi kuu ya mabasi, stendi ya daladala ya miyomboni, Kihesa, Mtwivila, Kitwiru, Ipogoro na chuo kikuu cha Iringa.
Tangu Kibiki atangaze nia ya kuwania jimbo la Irnga mjini, hali ya upepo wa jimbo hilo imebadilika huku wananchi wakiitaka CCM itende haki badala ya kuwakumbatia wanaotumia rushwa, kutaka
madaraka.
Mpaka sasa wanachama wa CCM wanaotajwa kuomba ridhaa ya CCM kuwania jimbo hilo wanafikia 10, akiwemo Mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu na Mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM ya jimbo hilo, Mahamud Madenge.
Akizungumza na waandishi wa Habari, Kibiki aliwashukuru wananchi wanaomchangia fedha hizo ili achukue fomu na kuahidi kuwa atafuata kanuni na taratibu za chama hicho ili asikose sifa za
kuteuliwa kupeperusha bendera ya CCM kwenye jimbo hilo ikiwa atashinda.
“Nawashukuru sana wana Iringa mnaonichangia fedha ili kuniwezesha kuchukua fomu, nathamini utu wenu nachowaomba mniombee,” alisema.
No comments:
Post a Comment