Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa ni
miongoni mwa wilaya saba nchini, zilizochaguliwa na shirika la
kimataifa lianaloshughulikia mazao ya viazi (CIP) kutekeleza mradi wa
uzalishaji wa viazi lishe vyenye asilimia kubwa ya vitamini “A” ukilinganisha
na aina nyingine ya vyakula kama Mboga, Matunda na Mizizi.
Kauli hiyo imetolewa Jana na Ofisa habari na Mawasiliano wa
Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi. Ndimmyake Mwakapiso, wakati akizungumza na
Nipashe ofisini kwake.
Alisema kuwa viazi lishe hivyo ni aina ya viazi vitamu
vyenye rangi ya chungwa vikiwa na asilimia 90 ya vitamini “A” vinavyohitajika
katika mwili wa binadamu ili kuwezesha kuwa na uwezo mzuri wa kuona, kujenga
ubongo wa watoto chini ya miaka mitano pamoja na kuimarisha afya ya wajawazito.
Alisema, mradi huo umeanza kutekelezwa katika vikundi vya
wakulima kwa kuotesha mbegu kwenye maeneo yenye miundombinu ya umwagiliaji yaliyopo
katika viijiji vya Igomaa na Lugolofu pamoja bustani ambazo hutambulika kwa jina
la vinyungu kwa wakazi wa wilaya hiyo zilizopo kwenye vijiji vya Lugema,
Mabaoni na Makungu.
Pia, aliongeza kuwa mbegu zitakazozalishwa zitagawiwa kwenye
vijiji 18 ambayo vimechaguliwa kuanza kutekeleza mradi huo mara baada ya msimu
wa mvua kuanza.
“Vijiji vitakavyo pata mbegu hizo ni Makungu, Mabaoni,
Lugema, Lugolofu, Iramba, Ikimilinzowo, Nyigo, Nyanyembe, Maguvani,
Idetero, Mkangwe, Ikangawani na Idumulavani, Igomaa, Utosi, Kibada,
Ugenza na Ikweha”, alisema Mwakapiso.
Aidha, alisema viazi vikizalishwa kwa wingi na kuongezwa thamani
ya zao hilo vitamwongezea mkulima kipato kwani, soko lake linapatikana kwa
urahisi huku vikiwa na uwezo wa kuzindikwa kwa kutengeneza Kripsi, Mikate,
Chapati, Biskuti, juisi na Unga wa lishe.
“Wakulima wataopata mbegu hizo, wazitumie vizuri kuweza
kuzalisha zao viazi kwa wingi ili liweze kujikwamua kiuchumi na kuondokana na
umasikini”, alisema.
Mbali na Wilaya ya Mufindi kuchaguliwa kutekeleza Mradi huo,
Wilaya nyingine zinazotekeleza Mradi huo, ni pamoja na Iringa, Ulanga, Mbozi,
Chunya, Wanging’ombe na Gairo.
No comments:
Post a Comment