Saturday, 12 September 2015

MWANZO BORA WAANZISHA PROGRAM YA LISHE MKOANI IRINGA

Na Friday Simbaya, Iringa

IMEELEZWA kuwa uelewa mdogo wa matumizi sahihi ya chakula pamoja na kutokula chakula mchanganyiko na kutumia nafaka kutengenezea pombe za kienyeji, ndio sababu za kuwepo kwa tatizo la utapiamlo katika Mkoa wa Iringa.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza wakati wa kufungua mkutano wa kamati za lishe za halmashauri na mkoa kuhusu masuala ya lishe ya mama na mtoto jana.

Mkutano huo wa uhamasishaji masuala ya lishe kwa watendaji ngazi ya mkoa na halmashauri uliaandaliwa na Mradi wa Lishe wa Mwanzo Bora (Mwanzo Bora Nutrition Program) kwa ufadhili wa serikali ya Marekani kupitia Shirika lake la maendeleo ya kimataifa (USAID).

Mkuu wa mkoa huyo alisema kuwa matatizo mbalimbali ya utapiamlo yanaendelea kudumaza, kulemaza na hata kuua watoto na wanawake hasa wajawazito na wanaoyonyesha.

Pia jamii kwa ujumla imekuwa ikiathirika kwa njia moja au nyingine kwa kuwepo kwa utapiamlo. 

Alisema kuwa tataizo la lishe duni linaendelea kuathiri uchumi na kuchangia kuwepo kwa umaskini.

“Lishe duni pia huathiri ukuaji wa maendeleo ya mtoto kimwili na kiakili, hivyo kufifisha mchango wake katika maendeleo ya jamii na taifa,” alisema.

Aliongeza kuwa sababu nyingine mojawapo inayopelekea kuwepo kwa tatizo la utapiamlo katika Mkoa wa Iringa ni pamoja na hali ya umaskini katika ngazi ya kaya inapelekea pia kushindwa kumudu kupata mlo kamili.

Aidhi, alisema kuwa serikali kwa kushirikiana na wadau imekuwa ikichukuwa hatua mbalimbali za kukabiliana na tatizo la lishe duni nchini.

Hatua hizo zinajumuisha utoaji wa elimu na uhamasishaji wa njia sahihi za ulishaji wa watoto, utoaji wa matone ya vitamin A na dawa za kutibu minyoo, uwekaji wa madini joto kwenye chumvi na utoaji wa tiba kwa watoto wenye utampiamlo.

Aidha, alisema kuwa wanawake wajawazito wanapatiwa vidongo vya kuongeza damu- yaani vidongo vya madini ya chuma na vitamini ya foliki aside.

Pia wajawazito hupatiwa dawa za kutibu malaria na minyoo, sambamba na elimu na hamasa kuhusu matumizi ya vyandarua vya kuzuia mbiu.

Nayo, mtaalamu wa lishe ya watoto kutoka taasisi ya chakula na lishe Tanzania (TFNC), Neema Joshua alisema kuwa takwimu za mwaka 2010 zinaoyesha kuwa asilimia 42 ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano nchini ni wadumavu, yaani wameshindwa kurefuka ili kufikia urefu unaotakiwa kulingana na umri wao.

Aidha, hali ya lishe ya wanawake nayo siyo nzuri ambapo asilimia 40 ya wanawake walio katika umri wa kuzaa (15-49) nchini wana upungufu wa wekundu wa damu.

Vile vile, watoto wa umri wa chini ya miaka mitano asilimia 59 wana upungufu wa damu na asilimia 53 ya wanawake wajawazito wana upungufu wa wekundu wa damu.

Alisema kuwa takwimu za Mkoa wa Iringa zinaonyesha kuwa hali ya lishe katika mkoa hairidhishi pamoja na kuwa Iringa ni kati ya mikoa yenye kuzalisha chakula kini nchini.

Mtaalamu wa lishe ya watoto kutoka taasisi ya chakula na lishe Tanzania (TFNC) huyo alizitaja baadhi ya athari zinazotokana na lishe duni kuwa ni udumavu (stunting) ambapo Mkoa wa Iringa unashika nafasi ya tatu kitaifa kwa kuwa asilimia 52, ambayo ni sawa na watoto 52 kati ya watoto 100 ni wadumavu.

Mkoa wa Dodoma unaongoza kwa kuwa na asilimia 56 ukifuatiwa na Mkoa wa Lindi kwa asilimia 54.

Ili Tanzania iweze kukabiliana na tatizo la utapiamlo inatakiwa kuwe na mipango thabiti.

Kwa kulitambua umuhimu huo, serikali ina mkakati wa taifa wa lishe wa miaka mitano uliozinduliwa na waziri mkuu Mizengo Pinda tarehe 20 Septemba, 2011 na utamalizika hadi juni 2016.



Katika ngazi ya halmashauri,kwa kutambua kuwa lishe ni suala mtambuka, serikali imeweka shughuli za mpango na kazi za lishe kwenye uratibu wa kamati za lishe za halmashauri (council nutrition steering committee).

No comments:

WATOTO WAITAKA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KALI ...

Na Friday Simbaya, Mufindi  Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Mufindi mkoani Iringa wameiomba serikali kwa kush...